Somo la 3
Ni muhimu kwa wanafunzi kukuza njia za kufikiria jinsi mahusiano mbalimbali yanavyofanya kazi ili waweze kupata marafiki na kujilinda wasipatikane na madhara.
Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kuwasaidia wanafunzi wafanye kazi na jumuiya kushughulikia suala mahususi. Shughuli kama hizi huwaunganisha wanafunzi na jumuiya ili kutatua tatizo la kijumuiya. Wanafunzi hujifunza kuhusu mahusiano kwa kufanya kazi na wengine, kwa:
kubadilishana maarifa na wataalamu wa mahali husika; kujifunza jinsi vikundi vinavyofanya kazi; kujifunza jinsi ya kukubali na kutimiza majukumu; kujifunza jinsi ya kutendeana ifaavyo; kuunganisha mawazo mbalimbali ili kusaidia kutatua tatizo.
Kupanga na kuandaa shughuli ambapo wanafunzi hufanya kazi na watu wengine katika jumuiya kwaweza kuwa kugumu. Unahitaji kuandaa kazi ambayo wanafunzi wanaweza kuchangia kikwelikweli, na unahitaji kuchagua watu walio tayari kufanya kazi na watoto. Unahitaji pia kupanga nao namna mwingiliano utakavyofanya kazi –unaweza kuhitaji kufanyika kwa zaidi ya wiki mbili au tatu au zaidi. Ni muhimu kwa wote wanaohusika – watu wazima na watoto –wafahamu wanachotakiwa kufanya. Kabla ya kufanya sehemu hii, tunapendekeza usome Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia jumuiya/mazingira husika kama nyenzo
Uchunguzi kifani ya 3: Kampeni ya mazingira ya jumuiya
Bibi Msafiri alikuwa akizungumza na darasa la sita kuhusu jinsi ya kuweka mazingira yao safi. Aliwataka wafikirie vitu katika jumuiya ambavyo vilihitaji kusafishwa.
Jambo moja walilotaja ni mifuko ya plastiki mtaani. Mifuko hiyo ilisababisha matatizo kwa kuwa iliziba mifereji. Mara nyingine, ng’ombe na mbuzi waliila na kuugua.
Darasa la Bibi Msafiri liliamua kuanzisha kampeni ya kijumuiya. Walizungumza na afisa mazingira wa hapo ambaye alikuja kuwasaidia kupanga kampeni yao darasani. Walizungumza pia na kamati ya wafanya biashara wa sokoni na wakaandaa kampeni hiyo pamoja.
Afisa mazingira aliandaa tukio la kijumuiya na alipata udhamini toka kwa AZAKI ya mazingira ya hapo. Wafanya biashara waliwaeleza wateja wao juu ya jambo hilo. Baada ya kujadiliana masuala haya na afisa mazingira, Bibi Msafiri aliwaandaa wanafunzi wake wafanye yafuatayo:
kuchora bango la kampeni;
kutunga tamthiliya na wimbo;
kuandaa mdahalo kwa ajili ya tukio hili;
kuandaa kampeni ya usafi.
Tukio hili lilifanikiwa kabisa. Wafanya biashara walionyesha mabango magengeni, na walifafanua masuala husika kwa wateja wao.
Jumamosi moja, shule nzima iliokota mifuko yote mtaani na kwenye mifereji. Kwa msaada wa wafanya biashara na afisa mazingira, kijiji kilikuwa safi zaidi sasa.
Shughuli muhimu: Kutathimini ujifunzaji wa wanafunzi
Kwanza soma Nyenzo-rejea 6: Mwongozo wa kupanga shughuli yenye msingi wa kijumuiya na Nyenzo-rejea muhimu: Kutathmini kujifunza. Kama unataka kuandaa shughuli yenye msingi wa kijumuiya kwa ajili ya wanafunzi wako, panga jinsi utakavyotathmini watakayokuwa wamefaidi kutokana na uhusiano. Endesha shughuli na darasa lako.
Baadaye, watake wajadiliane na kuandika juu ya shughuli zao, wakieleza:
taarifa walizotumia;
shughuli walizofanya na stadi walizokuza;
walivyoingiliana na watu waliohusika, na nani alifanya nini;
jinsi walivyoandaa kazi yao.
Pindi wakishafanya hivi, unapaswa kuwa na ushahidi wa stadi na maarifa mapya waliyopata. Wahimize kufikiria jinsi tukio lilivyofanikiwa.
Sasa, waulize mambo yapi mapya wamejifunza. Waelekeze wayajadili katika vikundi na kisha andika orodha.
Mwisho, watake waeleze:
wanapanga kutumia vipi stadi zao mpya siku za usoni;
nani wangependa kufanya naye kazi baadaye.
Wanafunzi wameona kuwa shughuli hii yachangamsha? Unajuaje? Unawezaje kuitumia tena aina hii ya shughuli?
Somo la 2