Nyenzo-rejea 5: Jinsi Igizo kifani Lilivyopokewa
Usuli / dokezo kwa mwalimu
Soma simulizi lote juu ya mwitiko wa jumuiya kuhusu igizo kifani, na kisha fikiria miitiko muhimu ilikuwa ipi. Kungeweza kutokea miitiko gani badala ya hii?
Fikiria kama jumuiya hii ingekuwa yako – unafikiri miitiko ipi ingeweza kutokea? Ungeshughulikiaje hali yoyote ambayo ingetokea?
Jinsi jumuiya ilivyolipokea igizo kifani
Baada ya darasa la Bwana Sele kuigiza igizo kifani lake kwa jumuiya, kulikuwa na mwitikio mkubwa. Chama cha Wazazi na Walimu kiliamua kuandaa mdahalo juu ya suala hili, na kulikaribisha darasa liwasilishe mawazo ya watoto.
Wiki iliyofuata, Bwana Sele aliongoza darasa lake hadi kwenye ukumbi wa mikutano wa shule, mahali pa mkutano wa viongozi wa jumuiya na wawakilishi wa makundi ya wataalamu wa eneo hilo. Mwenyekiti wa kijiji alikuwa mwenyekiti wa mkutano, afisa wa ustawi wa jamii alikuwa mwandishi.
Kila kundi liliwasilisha msimamo wake kuhusu tatizo la unyanyasaji wa watoto, kundi moja baada ya jingine.
Wanafunzi walisema kwamba wanataka unyanyasaji wa watoto upigwe marufuku kwa sababu unavuruga elimu ya watoto na mchango wao kwa maendeleo ya taifa.
Mwalimu mkuu wa shule hii alisema kwamba unyanyasaji wa watoto umesababisha upunguaji wa watoto wanaoandikishwa kusoma shuleni na kwa hiyo shule yake haiwezi kutimiza wajibu wake wa kuandaa viongozi wa siku zijazo.
Askari polisi alisema kwamba wasichana wadogo wachuuzi huingia kwenye ajira ya ngono na kuwa changu-doa. Wavulana huishia katika uhalifu wa aina mbalimbali, pamoja na udokozi na ujambazi.
Rai ya afisa wa afya ilikuwa kwamba wafanyakazi wengi wa mitaani, pamoja na watoto, hawali chakula cha kutosha na cha kufaa, na huelekea kuvutika na utumizi wa madawa ya kulevya, ambayo huwasababishia matatizo makubwa ya kiakili na kimwili.
Wazazi na wachuuzi walitoa hoja kwamba huwatumia watoto wao kutafuta kipato kwa ajili ya familia, na kwamba bila kufanya hivyo, hawawezi kuishi.
Mwakilishi wa serikali na mwenyekiti wa kijiji walisema kuwa kijiji jirani hakina tatizo kama hili lililokuwa linawakabili. Waliuliza kwa nini.
Wanafunzi walipendekeza kuwa serikali itoe msaada wa kifedha kwa wachuuzi ili waanzishe maduka yao majumbani kwao, na kwa wakulima ili waajiri vibarua.
Wajumbe wengine waliona pendekezo la wanafunzi kuwa ni zuri, na wakalikubali.
Wanafunzi walirudi darasani kuchora picha ya mkutano wa viongozi wa jumuiya, wakizingatia makundi mbalimbali yaliyokuwa yamewakilishwa. Wanafunzi waliandika waliyojifunza kuhusu jinsi kila kikundi kilivyohusiana na kingine, na jinsi mahusiano yanavyoweza kukuzwa zaidi.
Nyenzo-rejea 4: Kutafiti mambo ambayo wanafunzi wanafahamu kuhusu mahusiano