Somo la 1

Inawezekana wanafunzi wako wamekumbana na mgogoro ndani ya familia zao. Wanaweza kuwa wameshakuwa na ugomvi na kaka au dada zao; au kutokubaliana na wazazi wao. Wanaweza kuwa wameshashuhudia ugomvi baina ya ndugu wa familia zao, ukiwemo ugomvi baina ya mama na baba zao, na huu unaweza kuwa ni ugomvi wa maneno na pia mapigano.

Wanafunzi wanaweza kuwa hawahusiki moja kwa moja, lakini kama mwanafunzi anakumbana na mgogoro nyumbani, jambo hili linaweza kuathiri kusoma kwake kwa njia mbalimbali. Linaweza kuvuruga kule kujiamini na kujithamini kwake, anaweza kushindwa kumakinikia kazi yake na kuwafanya wakose raha na hatimaye kufadhaika.

Ni muhimu kwako kutambua jambo hili na kuwapatia wanafunzi wako msaada. Si mara zote itakuwa ni vizuri wewe kujihusisha na hali ya kifamilia, lakini, kama mwalimu wao, kuna mambo kadhaa ambayo unaweza kufanya ili kuwasaidia wanafunzi waendelee vizuri darasani. Kwanza, unaweza kulifanya darasa lako lisiwe katika mazingira ya migogoro ambapo wanafunzi watajiona kuwa wako salama na wanajiamini. Kwa kuanzisha kanuni za kimaadili za kupunguza migogoro, wanafunzi watakuwa na furaha pamoja na usalama.

Pili, unaweza kuwasaidia kihisia wale wanafunzi ambao wamekumbana na mgogoro nyumbani kwao. Msaada huu ni pamoja na wewe kuwa makini na hisia zao na kuhakikisha kuwa wanazungukwa na marafiki.

Tatu, unaweza kuwapatia wanafunzi stadi ili kuepuka migogoro wao kwa wao, na kupatana na kukomesha migogoro baina ya wengineShughuli hii inaweza kuwa changamoto, lakini ndiyo hasa itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Uchunguzi kifani ya 1: Kujadili mgogoro wa kifamilia

Bw. Okitiki nchini Afrika Kusini aliamua kujadili suala la mgogoro wa kifamilia na wanafunzi wake. Alisimulia hadithi sawa na ile iliyopo katika Nyenzo-rejea 1: Mgogoro wa kifamilia.

Aliwaambia wanafunzi wake wafikirie hadithi hii na kubainisha chanzo cha ugomvi huo. Aliwaambia wajadili, katika vikundi, jinsi ubishi ulivyotatuliwa. Baada ya dakika chache, walizungumzia ugomvi huo darasani. Wanafunzi walisema sababu za ugomvi zilikuwa: tabia ya kukopesha fedha kuwa ni tatizo; kwamba baba hakuwa na fedha za kutosha; kwamba mama hakutaka kumsikiliza;kwamba walikuwa hawawasiliani vizuri.

Waliamua kuwa masuluhisho yalipatikana kupitia njia zifuatazo: wanafunzi kuingilia kati;Mama kumsikiliza Baba na kusikia maelezo yake;Baba kumsikiliza Mama na kusikia maelezo yake;wote kusikia na kuelewa mtazamo wa kila mmoja.

Baada ya zoezi hili, Bw. Okitiki aliwapanga wanafunzi katika vikundi vya wanafunzi watatuwatatu ili kuigiza maigizo kifani yahusuyo hali ya mgogoro. Aliridhika na maigizo kifani wakati kila kikundi kilipowasilisha wiki iliyofuata. Kila igizo kifani lilijadiliwa na darasa zima, na walijifunza mengi kuhusu njia za kusuluhisha migogoro.

Shughuli ya 1: Kufasili Mgogoro

Ili kujua kile ambacho wanafunzi wako wanakijua wabunge bongo kuhusu mgogoro, uandike mawazo yao ubaoni au kwenye kipande cha karatasi. (tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia ramani za mawazo na kubunga bongo ili kutalii mawazo.)

Waambie wafikirie mazingira ya mgogoro ambayo nao walijikuta wamo, na, kila mmoja na mwenzake, wafikirie kuhusu maswali haya yafuatayo:

  • Watu wanagombania nini?

  • Nini sababu za ugomvi?

  • Je, kuna wakati mwingine ambao mnapigana?

  • Unapigana na nani?

  • Unapigania nini? Kwa nini?

  • Ugomvi unakufanya ujisikieje? Kwa nini?

  • Unamalizaje ugomvi wako?

Wahimize wanafunzi wafikirie kuhusu mazingira na tabia zao wenyewe. Waambie wanafunzi wawiliwawili waorodheshe mambo mbalimbali ambayo wangeweza kuyafanya ili kuepusha migogoro na familia au na rafiki. Kwa zamu kiulize kila kikundi moja kati ya mawazo yao na uyaandike ubaoni. Zungukia kila kikundi hadi urekodi majibu yote. Waulize wanafunzi: Yapi ni mawazo bora zaidi? Wangewezaje kuyatumia ili kuepusha au kutatua mgogoro?

Sehemu ya 5: Njia za kudhibiti migogoro