Somo la 3
Kwa vikundi na watu wanaofanya kazi kwa pamoja, ni muhimu kukuza ufahamu wa nini kinachoweza kusababisha migogoro na jinsi ya kuiepuka.
Shule ni kitovu cha jumuiya yo yote ile, na walimu na wanafunzi huwakilisha sehemu zote za jumuiya hiyo. Kutokana na hili, shule ingeweza kuwa na.jukumu muhimu sana katika kuepusha au kutafuta suluhisho kwa migogoro mipana ya jumuiya.
Shule pia zinaweza kuwasaidia wanafunzi kufahamu zaidi juu ya vyanzo vya migogoro pamoja na masuala yanayoambatana na migogoro hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wako wanaweza kuendelea na kuwa washiriki muhimu katika kusaidia katika migogoro inayohusiana na jumuiya.
Ili kuwasaidia wanafunzi wako wawe raia wanaojiamini unatakiwa:
uhakikishe darasa lako linakuwa na mazingira ya amani;
uwasaidie wanafunzi waelewe faida za kuwa na amani;
Uwapatie stadi za kusuluhisha migogoro.
Jambo muhimu ni kuwasaidia waelewe kuwa ni tabia mbaya isiyotakiwa na si yule mtu anayeifanya tabia hiyo.
Uchunguzi kifani ya 3: Kuwashirikisha wanafunzi katika kutafuta masuluhisho ya mgogoro wa kijumuiya
Abraham anafanya kazi katika shule iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Kulikuwa na mgogoro kati ya vijiji viwili vya jirani, Kitete na Mbulumbulu, uliohusu kugombania sehemu ya ardhi.
Mgogoro huu wakati mwingine ulisababisha matatizo shuleni, kwa sababu kuna wanafunzi walitokea katika vijiji hivi viwili na waliweza kuja shuleni baada ya kusikiliza watu vijijini kwao wakibishana.
Abraham aliamua kushughulikia tatizo hili pamoja na wanafunzi wake. Kwanza, aliwasaidia kubainisha mambo mbalimbali ambayo yanawaunganisha watu wa vijiji hivi viwili. Haya yanajumuisha: kwenda shule na kliniki moja; kutumia usafiri mmoja; kununua vitu katika soko moja.
Kisha aliwaambia wabainishe ni kitu gani ambacho kinakosekana kwa kila kijiji. Kitu kimoja ambacho wanafunzi walikibainisha ni uwanja wa mpira wa miguu pamoja na mchezo wa kukimbia.
Aliwauliza kama kulikuwapo na ardhi yo yote ili kuanzisha eneo la mpira wa miguu. Wanafunzi walipendekeza eneo lililokuwa katikati baina ya vijiji hivi.
Waliandaa wasilisho wakizungumzia sababu za kuhitaji uwanja wa michezo, na kwa nini eneo hili lilikuwa linafaa zaidi.
Walialika Chama cha Wazazi na Walimu (PTA) na kamati za vijiji ili wahudhurie, na baada ya wanafunzi kutoa wasilisho lao, watu walijadiliana.
Kamati zililikubali pendekezo. Vijiji vyote viwili vilipata uwanja wa michezo na jumuiya hizi mbili zilianza kushirikiana katika kujenga uwanja huo.
Shughuli muhimu: Migogoro ya kijamii
Kwa kazi ya nyumbani, waagize wanafunzi wako kila mmoja alete habari inayohusiana na mgogoro toka kwenye gazeti. Nyenzo-rejea 2: Mgogoro wa ng’ombe wasababisha mapambano makali inaonesha makala inayohusu mgogoro wa ardhi nchini Tanzania, lakini pia unaweza kutumia mifano tofauti.
Wanafunzi waelezane hadithi zao kwenye vikundi. Waambie wabainishe sababu za hiyo migogoro.
Waambie waangalie tena hizo habari na wapendekeze yapi yanaweza kuwa ni masuluhisho mbalimbali. Waambie waseme ni nani anawajibika kutafuta suluhisho.
Kisha, kiambie kila kikundi kichague habari moja na kiwasilishe mawazo yao juu ya kusuluhisha mgogoro huo darasani. Waambie wanafunzi wachangie katika mawasilisho ya wenzao na waseme kwa nini wanafikiri suluhisho lililopendekezwa linafaa au halifai.
Andaa orodha ya mapendekezo yaliyotolewa, na liambie darasa liandike kuhusu mapendekezo matatu watakayoyakumbuka na kuyatumia, na kwa nini.
Mapendekezo gani muhimu yaliyotolewa? Uliyataliije na wanafunzi?
Somo la 2