Somo la 1

Raia wote, pamoja na watoto, wana haki na majukumu, lakini yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Ili wanafunzi walielewe hili, wanahitaji kutambua haki na majukumu yana maana gani kwao. Wanahitaji kuelezana waliyoyatambua na kufikiria tofauti zao. Ili kutimiza hili, wanahitaji kuzungumza wakiwa darasa zima au wakiwa wawili wawili au wakiwa katika vikundi.

Uraia ni wazo gumu kwa wanafunzi wadogo na wanaweza wasilielewe mwanzoni. Ni vyema basi kulihusisha na kitu wanachokijua - kama kazi wanazozifanya wakiwa nyumbani. Kwa wanafunzi wakubwa, utaweza kutalii mada hii kwa undani na kuendeleza welewa wao kwa kufikiria wajibu na majukumu yao katika muktadha mpana zaidi wa jamii.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia makundi ya wanafunzi kama walivyokaa katika madawati kujadili haki na wajibu wa familia

Mwalimu Ngwinda ni mwalimu katika Shule ya Msingi Malbena katika jimbo la Eastern Cape Afrika ya kusini . Anafundisha darasa la 4 lenye wanafunzi 62 ambao hukaa katika vikundi vya wanafunzi watano watano wakizunguka madawati yao. Si rahisi kuwahamisha wanafunzi hao au kupangua madawati, kwa hiyo anatumia vikundi kufuata mpangilio wa madawati kujadili wajibu wa wanafunzi katika shughuli za nyumbani. Alitumia mbinu ya vikundi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi ya kuchangia mawazo yao.

Wakati wakijadili wajibu wao kwa muda wa dakika kumi, mwalimu Ngwinda huzunguka darasani akihakikisha kuwa hakuna anayetawala majadiliano na kukikumbusha kila kikundi kufikiria majukumu matatu ambayo watawaelezea wenzao.

Wanafunzi waliliona zoezi hili kuwa jepesi . Wakati wanafunzi wanawasilisha majibu yao mwalimu Ngwinda alikuwa anayaandika ubaoni. Anafurahishwa kuona kuwa wasichana wengi wanawasaidia mama zao majukumu ya nyumbani, kama kuosha vyombo na kupika na kuwaelea wadogo zao. Vijana wa kiume wanawasaidia baba zao na wajomba zao kuchanja kuni na kuchota maji, na wengine hufanya kazi katika bustani na mashambani. Walijadili mgawanyo wa kazi za nyumbani kwa msingi wa kijinsia.

Mwalimu Ngwinda aliwauliza kama wangesema mambo ambayo walikuwa huru kuyafanya katika familia zao. Wanafunzi waliliona zoezi hilo kuwa gumu, kwa hiyo aliwahimiza wajadili katika vikundi kabla ya kuwasilisha maoni yao. Mwalimu Ngwinda aliandika majibu yote ubaoni na kuwaeleza kuwa haya yote ambayo wako huru kuyafanya ni ‘haki’ yao. Alihakikisha wanaelewa tofauti kati ya wajibu na haki.

Tazama Nyenzo-rejea 1: Haki na wajibu wa watoto kwa ajili ya orodha ya haki na wajibu wa watoto nyumbani.

Shughuli ya 1: Vikundi vya wanafunzi wawili wawili kujadili haki na wajibu katika familia.

Waulize wanafunzi katika makundi yao ya wanafunzi wawili wawili, kujadili na kuorodhesha majukumu wanayopaswa kutekeleza nyumbani.

  • Baada ya dakika kumi kila kikundi , kwa zamu kieleze jukumu tofauti na uyaorodheshe majukumu yao ubaoni (wengi watakuwa na majukumu yanayofanana). Hakikisha kuwa wote wanaelewa kuwa haya ni majukumu yao. Mwambie kila mwanafunzi kurekodi orodha yao ya wajibu wao katika madaftari yao.

  • Baadaye, waulize wanafunzi katika makundi yao mambo ambayo wako huru kuyafanya katika familia zao (kama vile kusoma vitabu, kwenda kanisani/msikitini, kwenda shuleni, kucheza ndani au nje).

  • Orodhesha maoni yao ubaoni na talii welewa wao kuwa hizi ni ‘haki’ zao.

  • Watake kuorodhesha na kuchora mambo ambayo hupendelea sana kufanya -wajibu au haki. 

Je, umegundua kuwa kufanya kazi wawili wawili ni rahisi kutekeleza? Kama hivyo ndivyo, kwa nini? Kama sivyo, kwa nini?

Utabadilishaje shughuli hii ili kuiboresha wakati mwingine?

Maarifa na mawazo ya wanafunzi yanakushangaza?

Sehemu ya 1: Kubainisha uraia mwema