Somo la 2

Igizo kifani linaweza kuwa mbinu madhubuti sana katika kufundisha na kujifunza –hasa unaposhughulikia mada nyeti zinazohusu stadi za maisha au masomo ya uraia. Ni mbinu zinazofaa hasa unapochunguza masuala ya kijinsia pamoja na wanafunzi wako. Inaweza kuwasaidia wanafunzi kuzungumza kwa uhuru zaidi kwa sababu igizoni wanazungumza kuhusu tabia za watu wengine, na si tabia zao wenyewe. (Angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia igizo kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani .)

Ni muhimu kuchunguza mahali mtazamo pogofu kuhusu jinsia unapotokea. Wanafunzi wanahitaji kutambua ni wapi tabia ya mtazamo pogofu inashadidiwa. Mingi kati ya mitazamo hii inatokea katika familia, ni vema kuchunguza tabia yako mwenyewe. Je, unashadidia mitazamo pogofu ya kijinsia kwenye darasa lako? Je, mitazamo pogofu ya kijinsia ilishadidiwa kwenye familia yako mwenyewe? Uchunguzi-kifani 2 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyotumia uzoefu wake mwenyewe kuchunguza masuala ya kijinsia katika darasa lake.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia uzoefu wa utotoni katika kujadili jinsia

Bwana Awadh alitaka kufanya kazi na darasa lake kuhusu masuala ya kijinsia. Alitumia muda kutafakari kuhusu kitu cha kufanya. Alikumbuka kwamba alipokuwa mdogo, baba yake alikuwa akimwambia ‘tenda kama mwanaume’. Vilevile, anakumbuka kwamba dada zake wawili waligombezwa kwa ‘kutokuwa kama wanawake’. Aliamua kutumia mifano hii kutambulisha somo lake.

Aliandaa karatasi mbili zenye vichwa vya habari vifuatavyo: ‘Tenda kama mwanaume ’ na ‘Kuwa kama mwanamke’. Aliwaambia wavulana kueleza inamaanisha nini kutenda kama mwanaume. Wavulana walipomaliza kutoa mawazo yao, aliwauliza na wasichana. Alifanya hivyo hivyo kwa wasichana, akiwauliza wana maelezo au maneno gani wanaposikia mtu fulani anatenda kama mwanamke. Aliandika mawazo yao yote kwenye karatasi.

Alichora masanduku kuzunguka maneno fulani katika orodha zote mbili na akaeleza kwamba kuwa na tabia hizo kutazuia wanafunzi wanaotaka kufanikiwa. Walizungumza kuhusu jinsi ilivyo sawa kwa wavulana kupenda mitambo na michezo na kwa wasichana kupenda kupika na kutunza watoto, lakini tatizo linakuja tunapojihisi kuwa ni lazima tutimize majukumu haya ‘ili tukubalike’. Wasichana wengine wanaweza kutaka kufanya kazi za mitambo, n.k. na wavulana wengine wanaweza kutaka kutunza watoto au kuwa wapishi, lakini hawasemi wanavyotaka kwa sababu wanaweza kuchekwa.

Katika makundi madogo, wanafunzi walijadili kuhusu wakati walipojisikia kushurutishwa kutenda namna fulani ingawa wao hawakutaka. Walijadili kitu wanachoweza kufanya ili wakubalike kama walivyo, na pengine wafanye vitu tofauti na walivyofanya wazazi au walezi wao.

Shughuli ya 2: Igizo kifani kinyume

Katika shughuli hii, tunakutaka uandae maigizo kifani ambapo majukumu ya ‘kawaida’ yamebadilishwa (angalia Nyenzo-rejea 3: Igizo kifani kinyume kwa mfano). Hii itakusaidia kufikiri kuhusu mazingira mbalimbali ambamo unaweza kubadilishana nafasi kati ya majukumu ya kimapokeo yanayofanywa na wanaume na ya wanawake. Soma Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia igizo kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani .

Eleza darasa lako kuhusu shughuli hizi na madhumuni yake na kuhusu kutowacheka watu, bali kutafakari kuhusu masuala yanayoibuliwa wakati wakitazama. Baada ya kila igizo kifani, waambie wanafunzi wajadili, katika makundi ya jinsia changamano, maswali yafuatayo:

Unafikiri nini kuhusu hali hii? Ulijisikiaje ulipokuwa unaangalia igizo kifani hili, na kwa nini? Hisia zako zinaashiria nini kuhusiana na jinsi tunavyoyachukulia majukumu ya wanaume na wanawake katika jamii? Kama igizo kifani lingekuwa kinyume na lilivyooneshwa, je, ungejisikia tofauti?

Kama una wanafunzi wadogo, utatakiwa kuyafanya maigizo kifani yako rahisi kabisa. Vile vile, itakubidi baadaye, uwaongoze katika majadiliano yao, kuliko kuwaambia wajadili maswali katika vikundi.