Somo la 1
Vijana na watu wazima hufanya shughuli mbalimbali kama kazi na ajira. Katika sehemu hii, tunapendekeza utumie mkabala wa ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kuwasaidia wanafunzi wako watalii maana na umuhimu wa kazi na ajira.
Kuchunguza ni wapi pesa inayotumika kununulia vitu nyumbani inakotoka ni mwanzo mzuri kwa mada hii.
Katika Shughuli 1 uwatake wanafunzi kufikiria aina mbalimbali za kazi na ajira katika jumuiya yenu na mjadili tofauti baina ya kazi na ajira. Uchunguzi kifani 1 unaonesha mawazo ya baadhi ya wanafunzi juu ya aina mbalimbali za ajira.
Uchunguzi kifani ya 1: Kikundi kikifanya kazi na mdahalo
Darasa la 5 la Bwana Petro huko Afrika Kusini lilikuwa likifanya kazi kwenye ajira mbalimbali nchini. Sasa alitaka wafanye kazi kwenye jumuiya ya mahali walipokuwa.
Bwana Petro aliligawa vikundi viwili. Alikitaka kikundi kimoja kubainisha waajiri wa mahali hapo na kuandaa hoja iungayo mkono kwa nini ni bora kuajiriwa. Alikitaka kikundi kingine kibainishe njia mbalimbali zisizo rasmi za kuchuma fedha na kiandae hoja iungayo mkono kwa nini ni bora kuchuma fedha kwa njia hii. Baada ya dakika 20 za maandalizi, kila kikundi kiliwasilisha orodha yake na Bwana Petro aliiandika ubaoni –akihakikisha kuwa harudii mawazo (tazama Nyenzo-rejea 1: Njia za kuchuma fedha kutoka kwenye orodha yao). Walijadili orodha hizi na kung’amua kuwa kazi ni ile ile katika baadhi ya mifano, iwe rasmi au si rasmi, iwe ya kulipwa au isiyo ya kulipwa.
Katika somo lililofuata, walifanya mdahalo, kila kundi likimteua msemaji kuwasilisha hoja yao. Mwishowe, walipiga kura kuhusu kama ajira rasmi au isiyo rasmi ni bora. Hata baada ya kupiga kura, wanafunzi waliendelea kujadili mawazo haya, jambo lililomfurahisha Bwana Petro.
Shughuli ya 1: Kutumia ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kutalii shughuli za kazi
Tumia mkabala wa ‘fikiria-wawiliwawili-badilishana mawazo’ kuwasaidia wanafunzi kutambua njia mbalimbali za kuchuma fedha na kutalii fursa za ajira za wanafunzi.
Uwatake wanafunzi kila mmoja afikirie njia mbalimbali zilizopo za kuchuma fedha. Mpatie kila mwanafunzi dakika tano.Kisha, waweke wawiliwawili kwa msingi wa ujirani na watake wabadilishane mawazo. (Kama wanafunzi wako wameketi watatuwatatu kwenye dawati, tumia kikundi cha watatu badala ya wawili). Wanaunganisha mawazo yao kufanya orodha ya wawiliwawili au watatuwatatu. Wape dakika kumi.
Kitake kila kikundi kiseme mawazo yao na kuyaorodhesha ubaoni.
Jadili tofauti baina ya kazi na ajira. Hakikisha wanaelewa kwamba watu lazima wafanye kazi majumbani na kwenye mashamba, na hili ni tofauti na kazi wanazofanya kama ajira ambazo ni za kulipwa.
Watake wanafunzi wabadilishane mawazo jinsi wanavyotaka kufanya kazi katika siku za usoni.
Sehemu ya 3: Kuchunguza kazi na ajira