Somo la 2
Kusikia kutoka kwa wengine kuhusu namna wanavyofanya shughuli zao mbalimbali kunaweza kuwasaidia wanafunzi wako kuelewa aina mbalimbali za kazi zilizopo na kazi gani wangependa wenyewe kufanya. Kukaribisha mgeni kuzungumza nao juu ya kazi wanayofanya kunaweza kusaidia wanafunzi kuelewa jinsi kazi mahususi inavyofanywa. Kuongea na wanafunzi nje ya shule kutawasisimua na kuwamotisha na kutilia uzito namna wanavyoziona kazi nyingi.
Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia jumuiya/mazingira ya mahali hapo kama nyenzo inatoa mwongozo kuhus kukaribisha wageni darasani kwako.
Uchunguzi kifani ya 2: Kuzungumzia kazi na ajira
Ili kuwasaidia wanafunzi wake kukuza dhana za kazi na ajira, na kuelewa umuhimu wa kazi, mwalimu wa darasa la 5 Bi. Maria alizungumza na wanafunzi juu ya kazi na siku za usoni. Aligundua kwamba wengi wa wanafunzi wake walitaka kwenda chuo kikuu ili waweze kupata kazi nzuri na kuchuma fedha nyingi. Wengi wao walitaka kuhamia jijini.
Kuwaonesha wanafunzi wake hali za maisha, Maria alimkaribisha mwuza duka wa mahali hapo aje shuleni kuwaeleza jinsi alivyoanzisha biashara yake. Walijifunza kwamba kuanzisha duka na kuliendesha ni kazi ngumu. Kunahitajika pia fedha; alipata mkopo kutoka serikalini kuanzisha bishara yake. Alikuwa karibu amalize kulipa mkopo huo na hivi punde atamiliki biashara yake.
Maria pia alimkaribisha rafiki yake, Jamila, ambaye aliishi kijijini kwao lakini akaenda kusoma chuo kikuu, na sasa alifanya kazi katika benki katika jiji. Jamila alieleza kuwa siku zote alitaka kufanya kazi katika benki na ilimpasa asome kwa juhudi ili aweze kuwa mhasibu.
Baada ya ugeni huo, darasa lilifanya mdahalo juu ya kama ni bora kubaki kijijini na kuendesha biashara yako au kwenda chuo kikuu na kupata kazi. Darasa lilijifunza mengi juu ya jinsi kazi na ajira vilivyohusiana na juhudi zao shuleni na katika jumuiya pana zaidi.
Shughuli ya 2: Kuzuru biashara ya mahali hapo
Lipeleke darasa lako (au katika vikundi vidogovidogo, kwa zamu) kwenye soko la mahali hapo na waache waone kinachotokea hapo. Waweke katika vikundi vya wawiliwawili kwa uangalifu kuhakikisha wanamakinika na shughuli hiyo na wasihangaike na mambo mengine wakiwa nje ya shule. Jitayarishe kwa shughuli hii kwa kupanga na wachuuzi wa sokoni kujibu maswali ya wanafunzi kuhusu biashara zao. Utahitaji kuandaa karatasi-kazi/hojaji kwa ajili ya wanafunzi wako (tazama Nyenzo-rejea 2: Karatasi-kazi ziara sokoni ). Kama huna nyenzo za kutengenezea karatasi-kazi, basi katika somo lililotangulia andika maswali ubaoni na wanafunzi wayanakili katika daftari zao –kwa kuacha nafasi kwa majibu watakayopata sokoni. Kadhalika, waulize wanafunzi wanachotaka kujua na ongeza maswali haya kwenye orodha.
Kama wadhani inafaa zaidi, unaweza kulipeleka darasa lako kwenye benki ya karibu au sehemu nyingine ya ajira, lakini utahitaji pia kupanga shughuli hii na kuwa na maswali au shughuli ambazo wanafunzi watafanya au kuuliza wakiwa huko. Baada ya ziara, wanafunzi wanaweza kuandika na/au kujadili waliyojifunza kuhusu kazi. Andaa muhtasari wa mawazo haya ubaoni.
Somo la 1