Somo la 3
Katika shughuli zilizotangulia, wanafunzi wako wamejua zaidi kuhusu kazi na ajira kwa kazi za vikundi na pia wameelezwa uzoevu wa kimaisha wa watu walioajiriwa au wanaopata riziki.
Katika Shughuli Muhimu , unawapa wanafunzi fursa ya kuhusika katika kazi itakayopanua stadi zao na ambayo wanaweza kutumia ili kuchuma kipato.
Uchunguzi Kifani 3 unaonesha jinsi mwalimu mmoja alivyoanzisha biashara ndogo ili kuwapatia wanafunziwake uzoevu wa kazi na ajira.
Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia nyenzo za kienyeji zilizocheuzwa katika ushonaji na upataji wa kipato
Bibi Ngetu ni mwalimu wa mafunzo stadi wa shule ya msingi katika mji mdogo Tanzania. Karibu na shule kuna maduka matatu ya ushonaji. Eneo kuzungukia maduka ya ushonaji lilitapakaa vipande vidogovidogo vya nguo ambavyo mafundi ushonaji huvitupa. Bibi Ngetu na darasa lake waliwaza kwamba wangeweza kuvitumia vipande hivi kutengenezea vitu vya manufaa wakati wa masomo yao ya ushonaji. Aliwaomba mafundi ushonaji wamkusanyie vipande vyote vya nguo badala ya kuvitupa.
Bibi Ngetu alitumia vipande vya nguo kufundishia wanafunzi jinsi ya kushona. Walivikata, wakavipinda kwa unadhifu na kuvishona kutengeneza vitambaa vya mkono, skafu na vitambaa vidogo vya mezani. Kwa kuwa wanafunzi wengi hawakuwa na kitambaa cha mkono au skafu,
kila mwanafunzi alipewa kimoja. Vitambaa vya mkono na vitambaa vidogo vya mezani vilivyobaki viliuzwa kwa bei nafuu shuleni na kijijini.
Msichana na mvulana mmoja walichaguliwa kuweka rekodi ya kiasi cha fedha waliyolipwa. Walipaswa pia kulipia sindano na nyuzi walizotumia. Faida ilitumiwa kununulia sukari ya kutia katika uji wao. Wanafunzi walifurahi kwa sababu hapakuwa tena uchafuzi kutoka kwa mafundi ushonaji na sasa wanaweza kunywa uji wenye sukari.
Shughuli muhimu: Kuifanyia kazi shule yetu
Sasa ni wakati wa kuweka maarifa yote ya wanafunzi wako juu ya kazi na ajira kwenye jaribio kwa kufanya shughuli ambayo itanufaisha shule au nyumbani kwao.
Jadili na ubainishe shughuli ambazo wanaweza kuzifanya kama kazi-miradi ili ziwasaidie kukuza stadi, wakati huo huo zikiwa na manufaa kwa shule au nyumbani. Amueni pamoja mawazo mawili bora yanayoweza kutekelezwa. Mifano yaweza kuwa: kutengeneza vikapu, mikeka, kamba au fagio, au kukusanya mifuko na chupa za plastiki kwa ajili ya kuzicheuza. Aina ya shughuli itategemea mazingira ya shule.
Wanafunzi wanachagua kufanyia kazi mmojawapo wa miradi miwili iliyoteuliwa. Utahitaji kuwasaidia kupanga mradi na kukusanya nyenzo. Wataalamu wa mahali hapo na wana-jumuiya wanaweza kusaidia na kushauri juu ya nini cha kufanya.
Jadili na wanafunzi wanachoweza kufanya na mazao ya mradi wao (kama yanaweza kutumika shuleni, nyumbani au kuuzwa ili wachume fedha).
Jadili na wanafunzi manufaa ya miradi yao na stadi ambazo wamezipata.
Unaweza kutaka kupanga siku ya kuuza baadhi ya mazao na kutumia faida kununua vitu ambavyo vitalinufaisha darasa zima.
Waeleze wanafunzi kuwa shughuli wazifanyazo nyumbani na shuleni kama kazi zinaweza kuwasaidia kukuza stadi wanazoweza kutumia baadaye kupatia ajira.
Somo la 2