Somo la 1

Kujifunza baadhi ya dhana tata kuhusu mazingira kunakuhitaji wewe ukiwa mwalimu kuziweka dhana hizo katika vipengele vidogovidogo na kujenga picha kamili. Wanafunzi wanaelewa zaidi kama watafikiria juu ya mawazo wanayoyajua na kutumia mazingira yanayowazunguka kuwaonesha jinsi mawazo hayo yanavyohusiana na hali yao.

Kuna njia nyingi za kufanya hivi. Sehemu hii inatilia mkazo ukusanyaji wa taarifa kutokana na ujuzi wa wanafunzi kutalii dhana na majukumu na haki zao.

Uchunguzi kifani ya 1: Utafiti kuhusu matumizi ya maji katika jamii

Mwalimu Namhlane wa Nigeria alikuwa anaanza mada na wanafunzi wake wa darasa la pili, kuhusu mazingira akizingatia umuhimu wa maji katika maisha ya kila mmoja wetu.

Ili kuwahamasisha wanafunzi wake kuhusu mada hii, alianzisha mradi wa darasa. Kwanza, aliwataka waunde vikundi vya watu sita hadi wanane wanaoishi katika sehemu moja ya jamii na kuwaeleza kuwa kuna wageni watatu wanakuja shuleni siku inayofuata - mmoja akitoka kila sehemu ya jamii - ili kuzungumzia wanavyopata na kutumia maji. Aliwataka wanafunzi wake kufikiria na kuandika maswali watakayouliza. Makundi haya ya sehemu ya jamii yalishirikiana maswali yao ili kuhakikisha kuwa kila kikundi cha sehemu kingeweza kuona kama limefikiria vipengele vyote.

Kesho yake, kila mgeni alizungumza na wanafunzi wanaotoka katika sehemu yake ndani ya darasa au nje chini ya mwembe. Vikundi viliuliza maswali kwa njia tofauti - katika kikundi kimoja wanafunzi tofauti waliuliza swali moja kila mmoja, na katika kikundi kingine mvulana na msichana waliuliza maswali yote na waliobaki waliandika majibu.

Baada ya wageni kuondoka, wanafunzi walitakiwa kuorodhesha mambo matatu muhimu waliozingatia na kuwaelezea darasa zima. Mwalimu Namhlane alikitaka kila kikundi kwa zamu kuelezea walichogundua lakini bila kurudia jibu lililokwisha andikwa ubaoni.

Baada ya hapo walijadili matatizo yaliyokuwepo kuhusu maji na kufikiria jinsi ya kutatua. (Tazama Nyenzo - rejea 1: Matatizo ya kupata maji)..

Shughuli ya 1: Uwekaji wa kumbukumbu katika ‘shajara ya maji’

Watake wanafunzi wako kuweka kumbukumbu katika shajara kwa muda wa wiki moja. Wataandika (labda karatasi kubwa ya ukutani) kiasi cha maji wayatumiayo na kwa matumizi yapi (Tazama Nyenzo - rejea 2: Shajara ya matumizi ya maji kwa ajili ya kiolezo cha shajara).

Baada ya wiki moja, watake kufanya kazi katika vikundi na kuorodhesha katika yao matumizi yote ya maji na yaorodheshe kwa kuzingatia ni shughuli zipi zinatumia maji kwa wingi zaidi na zipi zinatumia maji kidogo. Bandika orodha hiyo ukutani na waruhusu kusoma kazi za wenzao kabla ya kuwa na majadiliano ya pamoja ya mwisho wakijadili masuala yahusuyo maji katika sehemu zao.

Itakuwa vyema kufikiria maswali kama: Maji yote yanapatikana kutoka wapi? Je, kila mmoja anapata maji? Je, maji yetu ni safi na salama? Huduma zetu za maji zinaweza kuboreshwaje? Tunaweza kusaidiaje?

Unaweza kuhusisha shughuli hii na kazi za tarakimu (kwa kuangalia data - kiasi cha maji kilichotumika), sayansi (kwa nini maji ni muhimu katika maisha yetu) na masomo ya jamii (matatizo ya kupata maji katika baadhi ya sehemu za Afrika).

Sehemu ya 4: Kutalii mazingira