Somo la 2
Kuchora ni njia nzuri ya kutambua mawazo ya wanafunzi kuhusu mada yoyote. Inawawezesha kuonesha mawazo yao bila kulazimika kuzungumza kwa sauti au kuweza kuandika. Ni njia nzuri kwa vijana wadogo na huwapatia njia ya kuzungumza maoni yao. Si lazima michoro iwe ya kiwango cha juu bali isimulie hadithi au ioneshe wazo. Kwa kutumia hadithi ni njia nyingine ya kuwaham asisha wanafunzi kufikiri kwa kina kuhusu tatizo. Inaondoa hali ya kumlenga mtu mmoja na badala yake inawawezesha wanafunzi kuzungumza kwa uwazi zaidi. Hadithi zinaweza pia kutoa taswira kubwa zaidi kwa wanafunzi na kuwahamasisha. Uchunguzi-kifani 2 na Shughuli ya 2 vinaonesha jinsi unavyoweza kutumia mbinu zote mbili katika darasa lako.
Uchunguzi kifani ya 2: Hadithi na masuala ya mazingira
Mwalimu Ngede aliwasomea wanafunzi wake Nyenzo-rejea 3: Hadithi ya mkulima mwenye ubinafsi ili kuhamasisha mawazo yao kuhusu ulimwengu na rasilimali zake.
Baada ya hapo aliwapa karatasi na kuwataka wachore picha ya ‘kwa nini mkulima alikuwa mbinafsi’.
Aliwaelezea wazo hili kwa makini na kuwahamasisha wasinakili, bali kufikiria juu ya mawazo yao. Baada ya wanafunzi kumaliza kuchora, walibandika picha zao ukutani. Mwalimu Ngede aliwataka baadhi ya wanafunzi kueleza picha zao zilihusu nini na alijaribu kukisia zingine zilihusu nini. Wanafunzi walifurahia sana zoezi hili.
Baadaye, aliongoza majadiliano kuhusu umuhimu wa kila mmoja kutunza ardhi. Waliorodhesha pamoja ubaoni jinsi watu katika jamii yao walivyotumia ardhi na jinsi walivyoitunza.
Baadaye aliwauliza maswali, ambayo waliyajadili katika vikundi. Kwa mfano:
Watu walitumiaje ardhi? Waliitunza? Ni kwa njia ipi mkulima angeitunza ardhi hii? Nani alifanya kazi? Je, ardhi ilikuwa na rutuba? Kama ndivyo kwa nini? Kama sivyo, kwa nini? Wanaweza kuboresha jinsi wanavyoitunza ardhi?
Mengi yanaweza kupatikana katika Nyenzo-rejea 4: Maswali kuhusu matumizi ya ardhi.
Kama darasa walifikiria maswali haya na kutoa mawazo yao.
Mwishoni mwa siku, Mwalimu Ngede aliwataka wanafunzi wakati wakiwa wanaelekea majumbani kwao waangalie njia mbalimbali za matumizi ya ardhi na kesho yake waje na mawazo yoyote ambayo yanaweza kuongezwa katika orodha yao.
Shughuli ya 2: Viongozi na mazingira
Shughuli hii inazingatia kwa upana zaidi umuhimu wa kutunza mazingira.
Nyenzo-rejea 5: Sebastian Chuwa anasimulia habari za Mtanzania mmoja aliyehamasisha jamii kujiunga pamoja kutatua matatizo ya mazingira. Soma habari hii kabla hujaanza kutayarisha somo.
Wasimulie habari hii wanafunzi wako. Andika ukutani tahajia za maneno, kwa mfano, ‘hifadhi’(ya mazingira).
Baada ya kusoma hadithi, jadili maneno hayo na maana zake.
Watake wanafunzi wako, wakiwa wawili wawili, wajifikirie kama Sebastian Chuwa. Ni masuala yapi ya mazingira ambayo wangependa kuyafanyia kazi? Wangefanyaje? Zunguka darasani na waulize wanafunzi walio katika vikundi vya watu wawiliwawili wenye mawazo mazuri kuyaeleza kwa wenzao darasani.
Watake wachunguze mazingira yao wakati wa kurejea nyumbani na waone kama kuna masuala mengine ambayo hawakuyaona kabla na wayazungumzie kesho yake. Orodhesha masuala matano wanayoyapendelea.
Somo la 1