Somo la 3

Ukiwa mwalimu, unahitaji kuwasaidia wanafunzi wako kuelewa majukumu yao kuhusu mazingira katika hali ambayo inawahamasisha na kuendeleza mtazamo wa kuyatunza. Katika Shughuli Muhimu , bango linatumika kama kichocheo na katika Uchunguzi-kifani 3 , mradi mdogo umeelezwa ambao unaonesha jinsi vikundi tofauti vinavyoweza kushirikiana ili kuleta mabadiliko.

Wakati wanafunzi wanaendelea kushughulikia mradi huo, kazi yako ni kuwa umejitayarisha kutarajia baadhi ya mahitaji yao na kuwapa nyenzo ili kusaidia kujifunza kwao. Kama una darasa kubwa, unahitaji kufikiria jinsi utakavyowashirikisha wanafunzi wako wote na labda kugawanya kazi katika makundi. Kwa wanafunzi wa umri mdogo, utatakiwa kufanya shughuli za kiwango kidogo na washirikishe baadhi ya wanajamii wakusaidie zaidi.

Uchunguzi kifani ya 3: Upangaji na utekelezaji wa kampeni ya usafi

Darasa la shule ya Ngombe, Iringa, liliamua kampeni ya usafi. Mwalimu wao aitwaye mama Mboya amekuwa akiufanyia kazi mtaala mpana wenye kichwa cha habari ‘kulinda ardhi yetu’.

Baada ya kuzungukia shule asubuhi nzima na maeneo yanayoizunguka, Mwalimu Mboya na darasa lake walijadili waliyoyaona. Waliorodhesha mambo yote waliyoyapenda katika sehemu hizo na sehemu au mambo waliyotaka kubadili au kuboresha.

Waliamua kufanyia kazi sehemu ndogo mbili kwa kuzisafisha - uwanja wa shule wa michezo na kijito kilicho karibu na shule. Darasa liligawanywa katika makundi mawili yakiwa na timu mbili zikifanya kazi katika kila sehemu. Timu zilijadili wanachoweza kufanya halafu zilishirikiana mawazo na timu nyingine. Walikubaliana nani atafanya kazi gani na kila timu ilitekeleza mipango yake kwa muda wa juma zima, wakati wa saa za shule.

Darasa lilifanya usafi kwa muda wa wiki nzima. Baadaye walifanya maonesho katika ukumbi wa shule ambayo yalionesha:

Wingi na aina za takataka zilizokusanywa wakati wa kufanya usafi; Mipango ya kuendeleza hali ya usafi na kutokuwa na takataka katika siku zijazo; Jinsi ya kushughulikia takataka, ikiwa ni pamoja na kuzitumia tena kwa shughuli nyingine baada ya kuzipitisha katika mchakato mwingine au kuzifukia au kuzichoma;

Maonesho yalifanikiwa na wanafunzi wa madarasa mengine walifurahia kazi iliyofanywa na kusaidia kuweka shule safi zaidi.

Shughuli muhimu: Kuchukua hatua kuhusu masuala ya mazingira

Shughuli hii ni mwendelezo wa uhamasishwaji wa wanafunzi wa kushughulikia masuala ya takataka na inachukua mbinu ya hatua kwa hatua ya kujifunza kwa vitendo.

Hatua ya 1 –Watake wanafunzi (labda katika vikundi vya wawiliwawili) kutambua masuala ya takataka shuleni na karibu na shule. Chagua kipengele (labda kile kilichotajwa mara nyingi). 

Hatua ya 2 –Shirikiana na darasa kutayarisha ‘mpango wa utekelezaji’. Ili kufanya shughuli hii, kitake kila kikundi kupendekeza njia za kutatua matatizo. Hakikisha kuwa mpango wa utekezaji uliokubalika ni halisi na unaweza kutekelezwa na darasa. Wape wanafunzi katika vikundi kazi za kufanya. Uandike mpango wa utekelezaji katika bango likionesha mwisho wa utekelezaji, bango hilo linaweza kuwekwa katika ukuta wa darasa.

Hatua ya 3 –Chukua hatua: hii inaweza kuwa kazi ya siku au miezi mingi lakini hakikisha kuwa kila kikundi kinaweka kumbukumbu za kila wanachokifanya, lini na kwa utaratibu upi.

Hatua ya 4 –Wakiwa wanakamilisha kila sehemu ya mpango huo wa utekelezaji, watake warekodi maendeleo yao katika bango.

Hatua ya 5 –Wakati wakimalizia, tafakari mafanikio ya mpango pamoja na darasa. Wamejifunza nini? Kulikuwa na matatizo gani? Watafanya nini kuendeleza wazo hili? Je, sehemu imeendelea kuwa safi?

Nyenzo-rejea ya 1: Matatizo ya upatikanaji wa maji