Nyenzo-rejea 5: Sebastian Chuwa
Nyenzo rejea za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi
Sebastian Chuwa ni mtu mwenye ndoto kwa nchi yake, watu wake na vizazi vijavyo ambao watarithi urithi wao. Kwa miaka 30 amekuwa mstari wa mbele kusomea matatizo ya mazingira katika ardhi yake ya nyumbani Tanzania, Afrika ya Mashariki, na majawabu aliyoyapata yanatoa matokeo yanayonufaisha si ardhi peke yake, bali watu wote wanaotegemea ardhi kwa maisha na maendeleo yao. Mbinu zake ambazo zimejikita katika malengo ya msingi mawili ya uhamasishaji kwa vitendo katika jamii - kuratibu zoezi la watu kueleza matatizo yao katika ngazi ya mtaa, na elimu kwa vijana – ili kuhamasisha ufundishaji wa uhifadhi wa ardhi mashuleni, kuanzia ngazi ya shule za msingi.
Ametoa msukumo kwa makundi makubwa ya vijana wa kujitolea wa kijumuia kukaa pamoja na kutatua sio tu matatizo yao ya kimazingira, bali pia matatizo yao ya kupunguza umasikini, kuwawezesha wanawake na maendeleo ya vijana katika eneo la Mkoa wa Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania. Juhudi zake, kwa niaba ya shirika la African blackwood, zimeunda mpango wa kwanza wa kiwango cha juu wa kupanda upya wa spishi za mimea. Kwa sababu ya uanzishwaji wa bustani nyingi za miche ya miti za kijumuia na miradi kadhaa ya ushirika inayokusudia kuboresha kupanda upya kwa miti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, mwaka 2004 ABCP na makundi ya vijana walioshiriki katika kazi ya Sebastian, walisherehekea upandaji miti milioni moja.
Aina ya kazi yake, ambayo inapanuka kila wakati, imempa yeye na jumuia yake hadhi ya kuwa viongozi katika uwanja wa hifadhi ya Tanzania.
Historia ya Mradi wa Hifadhi wa African Blackwood (African Blackwood Conservation Project- ABCP)
Mwaka 1996, James Harris, mtaalamu wa kutengeneza mapambo kutoka Texas, USA, na Sebastian Chuwa walifadhili Mradi wa Hifadhi wa African Blackwood (ABCP), ili kuanzisha mpango wa elimu na upandaji upya wa miti, hasa kwa ajili ya spishi ya mmea uitwao mpingo (Dalbergia melanoxylon) katika eneo lake la nyumbani lililoko mashariki mwa Afrika. Mti wa mpingo unatumiwa sana na wachongaji wa Kiafrika na watengenezaji wa vifaa wa Ulaya kwa ajili ya kutengeneza zumari, filimbi, na vifaa vingi vingine vya muziki. Kwa sababu ya kuvunwa kupita kiasi, na kukosekana kwa juhudi zozote zinazoelekezwa kwenye kupanda upya kwa spishi hii, kuendelea kuwepo kwake kuko hatarini.
Mwaka1995, James Harris, ambaye anatumia mpingo katika sanaa zake za mikono, aliona filamu ya The Tree of Music huko Marekani na alidhamiria kufanya jambo kuhusiana na uhifadhi wa spishi hii. Aliwasiliana na Sebastian kwa barua pepe na alipendekeza washirikiane: angezindua mpango wa kuchangia mfuko miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa za miti, wanamuziki, wahifadhi misitu wa nchi za magharibi, na kisha kutuma fedha zitakazopatikana kwa Sebastian ili aanzishe bustani ya miti nchini Tanzania. Mradi uliidhinishwa na Bwana Chuwa kwa shauku kubwa. Tangu wakati wa mawasiliano hayo ya awali, ABCP imekuwa ndiyo nguvu inayoongoza uhifadhi wa mpingo kaskazini mwa Tanzania, inayofadhili bustani za mimea kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa miche ya mpingo na inayohamasisha kuhusu umuhimu wa spishi ya mpingo kimataifa.
Hifadhi ya Ngorongoro
*Kifaru mweusi huzuia magari barabarani katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Wakati wa utoto wake, nyumbani kwa Sebastian Chuwa kulikuwa kwenye mteremko wa kusini mwa Mlima Kilimanjaro katika kimo cha 4900’. Alijifunza kupenda mambo ya asili tangu utotoni kutoka kwa baba na mshauri wake, Michael Iwaku Chuwa, ambaye alikuwa mtaalamu wa mitishamba. Kwa pamoja walianzisha jitihada ya kusafiri na kufanya utafiti katika misitu ili kukusanya mimea ya madawa ambayo baba yake aliyatumia kwa kazi yake. Kutokana na safari hizi, katika kipindi cha miaka mingi alijifunza majina ya mimea na miti miongoni mwa mimea yote iliyosheheni katika eneo la Kilimanjaro. Upendo wake kwa dunia asilia unaendelea mpaka leo na ndio siri inayoongoza kazi yake.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alisoma katika Chuo cha Usimamizi wa Maliasili cha Mweka na baada ya kuhitimu aliajiriwa kama mhifadhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Katika kipindi cha miaka 17 cha ajira yake hapo, alijisomea na kuandika katalogi ya mimea ya sehemu ile, aligundua spishi mpya nne (ambazo kwa heshima yake, mbili kati ya hizo, zimeitwa jina lake) na amekusanya hodhimadawa ya mitishamba yenye aina 30,000 za mimea katika kituo cha wageni kwa ajili ya matumizi ya wageni na watumishi. Kwa sababu ya welewa wake mpana kuhusu mimea mingi ya eneo hilo, anafanya kazi na Mary Leakey katika eneo la jirani la Oldavai Gorge, kuitambua mimea kwenye eneo la ugunduzi wa mtu wa mwanzo la Leakey. Vile vile, katika Hifadhi ya Ngorongoro alianzisha mpango wa kuhifadhi vifaru weusi walio hatarini kutoweka; mpango ambao ulipata mafanikio. Mpango huu ulinakiliwa katika sehemu nyingine za Afrika.
Mbuga ya Ngorongoro ni eneo ambalo linasimamiwa kwa ushirika ambako jamii za Wamasai bado zinaishi na mifugo yao. Wakati wa kipindi chake cha ajira katika Mbuga, Sebastian alifanya kazi kwa karibu na Wamasai, akijifunza madawa yao na kuanzisha bustani za miti kwa ajili ya matumizi yao. Vile vile, alianzisha mpango wa kwanza wa elimu ya hifadhi ya misitu kwa vijana nchini Tanzania, hasa kwa ajili ya watoto wa Kimasai, uliohusu shughuli za kivitendo kama vile uanzishaji wa bustani za miche ya miti na miradi ya upandaji wa miti. Klabu hii ilifanikiwa sana hata ikiwa mfano kwa harakati za upandaji miti za nchi nzima; iliitwa Klabu ya Malihai ya Tanzania iliyoanzishwa mwaka 1985, ikiwa na ofisi katika Makao Makuu ya Mbuga ya Ngorongoro iliyoko Arusha; hivi sasa inafanya kazi nchi nzima na ina klabu zipatazo 1,000.
Ofisi na Tuzo
Mwaka 1999, Sebastian alitunukiwa wadhifa wa kuwa mwenyekiti wa Mfuko wa Dhamana ya Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira Kilimanjaro. na Mamlaka ya Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Ofisi hii, moja kwa moja inamfanya awe mjumbe wa Kamati ya Hifadhi ya Mazingira ya Mkoa. Kutokana na wadhifa huu, michango yake muhimu katika hifadhi ya mazingira itasambaa.
Imetoholewa kutoka: African Blackwood Conservation Project, Website
Nyenzo-rejea 4: Maswali kuhusu utumizi wa ardhi