Somo la 1

Huenda unakabiliwa na changamoto mbili mahsusi unapoandaa masomo ya VVU na UKIMWI. Ya kwanza ni kujiamini katika welewa wako na ya pili ni kwamba mada yenyewe ni nyeti na inaweza kuwa ngumu kuifundisha. Kama kuna shaka yoyote katika akili yako kuhusu kama elimu ya VVU na UKIMWI ifundishwe mashuleni au la, unatakiwa kujadili suala hilo na Mwalimu Mkuu wako. Hata hivyo, ni muhimu kwamba kila mtu afahamu kuhusu VVU na UKIMWI.

Ni muhimu sana ujiandae vizuri kabla hujaanza kuifundisha mada hii kwa wanafunzi wako. Lazima uzijue taarifa zinazohusika na ujiandae kujibu maswali ambayo yanaweza kuwa magumu kwako. Sehemu hii itakusaidia kujiandaa vizuri kwenye ufundishaji wa VVU na UKIMWI.

Aidha, ni lazima utafakari kuhusu wanafunzi kwenye darasa lako na jinsi gani kila mwanafunzi anaweza kuielewa mada hii. Utakachozungumzia, kwa kiasi kikubwa, kitatokana na umri wa wanafunzi wako na kwa kiasi gani unafikiri tayari wanafahamu kuhusu mada hii.

Uchunguzi kifani ya 1: Mpango wa kufundisha kuhusu VVU/UKIMWI

Bibi Shikongo wa nchini Tanzania alikuwa anajiandaa kufundisha Darasa lake la 4 kuhusu VVU na UKIMWI; na alikuwa amechanganyikiwa kidogo. Itakuwaje kama wanafunzi watamwuliza maswali ambayo atashindwa kuyajibu? Alifahamu ilikuwa ni muhimu kujiandaa vema na alitafakari kuhusu namna atakavyotekeleza jukumu hili. Aliandika madokezo ya mambo atakayohitaji kuyafanya.

  1. Kuzungumza na mwalimu wa Darasa la 5. Alihudhuria warsha ya VVU na UKIMWI iliyofanyika Nairobi. Uliza ikiwa ana madokezo yoyote ya warsha au nyenzo-rejea zozote ambazo zinaweza kuazimwa.
  2. Angalia katika maktaba ya shule ili kuona kama kuna vijarida vyovyote au habari nyingine za VVU/UKIMWI kwa ajili ya walimu na wanafunzi.
  3. Mwulize Mwalimu Mkuu kama kuna mwalimu mshauri wa VVU na UKIMWI katika sehemu yetu na wasiliana naye kwa ajili ya kupata taarifa za msingi.
  4. Chunguza kama kuna Asasi Zisizo za Kiserikali au kliniki zozote hapo mjini ambazo zina taarifa zinazohusiana na VVU na UKIMWI.
  5. Kusanya pamoja nyenzo-rejea, kisha panga muda wa kuzipitia na andaa madokezo kuhusu taarifa muhimu. Soma nyenzo-rejea huku ukizingatia umri wa wanafunzi wako na angalia kama unaweza kuzitumia.
  6. Tafakari jinsi ya kuwarahisishia wanafunzi wako kujifunza kuhusu mada hii na kuweza kuijadili kwa maoni yao wenyewe. Unawezaje kuhakikisha kwamba kujifunza kwao hakuzuiwi na aibu?
  7. Je, tunahitaji ‘kanuni’ maalum ambazo tutazitumia kujadili mada makini kama hii?

Fikiria jinsi ya kutathmini ni kwa kiasi gani wanafunzi wamejifunza.

Baada ya kumaliza maandalizi yake, Bibi Shikongo alifundisha somo lake la kwanza kuhusu VVU na UKIMWI. Darasa lake lilichanganyikiwa mwanzoni lakini jinsi darasa lilivyokuwa likiendelea wanafunzi walisikiliza na kushiriki vizuri. Wengi kati yao walizungumza kuhusu somo hilo wakati wa mapumziko. Wengine walimwuliza maswali ambayo alisema angeyajibu kwenye kipindi kitakachofuata

Shughuli ya 1: Maandalizi ya kufundisha VVU na UKIMWI

Jiandae kwa kutafiti taarifa zihusuzo VVU na UKIMWI na kutafakari kuhusu namna utakavyozifundisha kwa wanafunzi wako. (Tazama Nyenzo-rejea 1: VVU na UKIMWI katika Afrika kwa taarifa na mitandao faafu ya tovuti unayoweza kuitumia.)

Andika madokezo, ukitafakari kuhusu mambo yafuatayo:

Wasiliana na Mwalimu wako Mkuu kama anaridhia ufanye somo hili.

Utapata wapi taarifa?

Kuna mtu anayehusika na nyenzo-rejea katika shule yako? Mji? Wilaya?

Kuna Asasi Zisizo za Kiserikali au vituo vya afya vinavyoshughulika na elimu kuhusu VVU na UKIMWI?

Ni kwa namna gani utakusanya taarifa hizi?

Utaamuaje kuwa taarifa zipi zinawafaa wanafunzi wako?

Tafakari kuhusu umri wa wanafunzi na ukubwa wa darasa.

Ni jinsi gani utalipanga darasa na wanafunzi wako?

Je, wanafunzi wako wangefaidika kwa kuwa na mtaalamu wa kijumuia ambaye anakuja na kuzungumza nao ili kuendeleza ulichokiandaa kwa darasa lako? Wataalamu waje mwanzoni mwa kazi hii au baadaye?

Unaweza kupata nyenzo-rejea gani nyingine? Je, kuna chumba cha kompyuta katika shule yako ambako darasa linaweza kuunganishwa kwenye mtandao wa tovuti au ambako unaweza kukusanya taarifa?

Je, kuna wanafunzi wowote ambao wanaweza kuonesha hisia kali dhidi ya mada hii? Utakabiliana vipi na tofauti za uoneshaji wa hisia?

Panga utangulizi wa somo lako.

Sehemu ya 5: Mbinu makini za kukabili wu na ukimwi