Somo la 3

Iwapo wanafunzi wanatakiwa kujifunza kwa kuchangamka, basi wanatakiwa wawe wamechangamka ama kimwili au kiakili au vyote viwili! Kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia katika kuhamasisha kujifunza kwa uchangamfu ili kuhakikisha wanafunzi wako wanafaidika katika masomo yao. Kuhusu ni njia gani unazozitumia kufundisha juu ya VVU na UKIMWI kutategemea sana ukubwa wa darasa lako na umri wa wanafunzi wako –na kile unachokijua kuhusiana na njia hiyo ya kujifunzia wanayoipendelea.

Unajua kuwa igizo ni mbinu nzuri ya kutumia katika kuwasaidia wanafunzi kujadili mada ambazo ni nyeti. Kwenye masomo ya VVU na UKIMWI, itawafanya wanafunzi wajadili hali ambazo siyo zao lakini kwa kutafakari jinsi ambavyo hali hizi zinavyohusiana na uzoevu wao wenyewe. Njia hii inatumika kwenye Shughuli Muhimu.

Njia nyingine inayofaa ni jaribio (angalia Nyenzo-rejea 3: Jaribio kuhusu VVU na UKIMWI ). Katika Uchunguzi-kifani 3 , mwalimu mmoja anatumia, jaribio kama shughuli ili kujua ni kwa kiasi gani darasa lake la msingi linavyojua kuhusu VVU na UKIMWI.

Uchunguzi kifani ya 3: Kutumia jaribio kama shughuli ya kujifunzia kuhusu VVU na UKIMWI.

Maria alitumia mtandao ili kujiandaa kwa ajili ya kufanya kazi na wanafunzi wake juu ya VVU na UKIMWI. Ana bahati kwani anaongeza uwezo wake wa kufundisha kwa njia ya elimu ya masafa na anaruhusiwa kutumia chumba cha kompyuta kilichopo katika kituo cha kujifunzia. Alipata tovuti iliyoorodheshwa kwenye Nyenzo-rejea 1 na aliamua kujaribu moja ya shughuli zilizopatikana pale kwenye tovuti. Shughuli hii imepangwa kwenye Nyenzo-rejea 4: Uambukizo. Maria alifuata maelekezo na aligundua kuwa njia hii ilimsaidia sana katika kujua baadhi ya mitazamo potofu waliyokuwa nayo wanafunzi wake kuhusu VVU na UKIMWI. Pia alikuta kwamba njia hii inachukua muda mrefu sana kwa darasa lake kubwa lenye wanafunzi 56, ila alipoitumia kwa mara ya kwanza ilikuwa ni kero kidogo.

Hivyo, kipindi kilichofuata, aliligawa darasa lake katika vikundi viwili na akawa na kikundi kimoja kinachoandika kuhusu vitu walivyovijua au walivyovifikiria kuwa walivifanya kuhusiana na VVU na UKIMWI wakati wengine walikuwa wanafanya shughuli. Somo lililofuata vikundi vilibadilishana. Katikati ya masomo aliweza kutafakari kuhusu kile ambacho wanafunzi walikuwa tayari wanakijua au kufikiri kuwa walikuwa wameshakijua kuhusu VVU na UKIMWI na hii ilimsaidia Maria kupanga somo lililofuata.

Shughuli muhimu: Igizo-kifani kwa ajili ya masomo yanayohusu VVU na UKIMWI

Panga igizo kwa ajili ya baadhi ya masomo yanayohusu mada za VVU na UKIMWI (angalia Nyenzo-rejea 5: Igizo-kifani kwa ajili ya masomo ya VVU na UKIMWI) ambayo yanaendana na umri wa wanafunzi wako. Kama wanajihusisha na ngono, unaweza kulenga kwenye kuzuia. Hapa pana mifano ya vipengele vya kutumia:

  • John anasema kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Mary. Kwenye miadi, wakiwa wenyewe, John anajaribu kumshawishi Mary afanye naye mapenzi.

  • Angela, msichana mzuri na mjanja, hana vitu vizuri kama walivyonavyo baadhi ya wanafunzi wenzake. Mjomba wake alimtambulisha kwa rafiki yake ambaye anampenda Angela na anapenda ‘kumtuza’ Angela–lakini kama atafanya naye mapenzi.

Unaweza kwanza kutumia mpangilio huu wa matukio katika kujadili matatizo na baadaye kuwaambia wanafunzi wako waigize kuhusu njia za kushughulikia tatizo hili.

Ukiwa unafundisha watoto wadogo, unaweza kutunga maigizo yanayohusu fikra potofu kama vile:

  • Precious na Becky wako kwenye vyoo vya shule. Precious anataka kujisaidia lakini anasema kuwa atasubiri mpaka afike nyumbani au kwenye kichaka kwa sababu hataki apate UKIMWI.

Kamilisha mpango wako na endelea na somo hili. Mwishoni, jiulize: mpango umekwenda vizuri kiasi gani? Ulifanya kitu gani vizuri? Unawezaje kuboresha mbinu yako ili kuwasaidia wanafunzi waelewe na wajisikie salama?

Nyenzo-rejea ya 1: VVU na UKIMWI katika Afrika