Nyenzo-rejea 5: Igizo kifani kwa masomo ya VVU na UKIMWI

Usuli / dokezo kwa mwalimu

Unapofikiria matatizo kwa ajili ya maigizo kifani, hakikisha unawapa nafasi wanafunzi kulenga miitikio au mienendo chanya. Utafiti umeonesha kuwa ujumbe hasi na unaoogofya hauhimizi badiliko chanya la tabia mara zote. Katika igizo kifani, wanafunzi huigiza hali kwa msukumo wao wenyewe. Hii ina maana kwamba huchukua nafasi na kuamua watakachofanya na kusema papo kwa papo. Hawafanyi mazoezi au kutumia andiko. Huwezi kubashiri kwa hakika namna nafasi itakavyoendelezwa. Maigizo kifani yanaweza:

  • kusaidia kupambanua mitazamo ya watu tofautitofauti;

  • kusaidia wanafunzi kutalii mienendo ya vikundi au watu binafsi;

  • kusaidia wanafunzi kuona kuwa watu wana matatizo yanayofanana;

  • kusaidia wanafunzi kukuza stadi za jinsi ya kuhusiana baina ya mtu na mtu;

  • kutoa fursa ya kushughulikia matatizo nyeti;

  • kusaidia wanafunzi kuona mambo kutumia mitazamo ya watu wengine;

  • kusaidia wanafunzi kufanya mazoezi ya kutenda na kusema kwa uthabiti;

  • kuwapa nafasi wanafunzi kutalii hali zinazowahusu bila kufichua jambo lolote binafsi kuhusu maarifa yao, imani zao, uzoevu au hali zao.

Vidokezo kwa ajili ya maandalizi na uendeshaji wa maigizo kifani

  • Andika tatizo ubaoni au kwenye karatasi.

  • Wape nafasi wanafunzi wasome na kuifikiria hali.

  • Mpe kila mwanafunzi ‘kadi ya nafasi’ ikieleza nafasi yao na wape nafasi wafikirie watasema nini. Maandalizi haya yanaweza kufanywa katika vikundi vya wanafunzi wenye ‘nafasi’ ile ile. (Njia hii inawafanya wanafunzi walenge ‘nafasi zao’ na si hali nzima na hivyo inaweza kutoa igizo kifani lililo changamani zaidi.)

  • Mvulana anaweza kucheza nafasi ya msichana, na msichana ile ya mvulana.

Toa muda kwa ajili ya majadiliano, yatakayohimizwa na maswali kama: Mhusika fulani (…) angetendaje tofauti na alivyotenda? Ni sababu zipi zilizomfanya fulani (…) atende kama alivyotenda? Wahusika wengine walijihisije?

Nyenzo-rejea 4: Uambukizo