Somo la 1

Wakati wewe na wanafunzi wako mnasoma hadithi, unaweza kuwasaidia kutambua nani amehusishwa katika hadithi na amehusishwaje, na nani hakuhusishwa.

Unaweza kuwasaidia kuona jinsi mandhari ya hadithi (shule, kijiji, mji, n.k.) yanavyoelezwa. Unaweza pia kuwasaidia wanafunzi kwelewa mtazamo au msimamo wa mwandishi, kufikiria kama kunaweza pia kukawa na maoni mengine na, kama yapo, ni yapi.

Unapofanya hivyo na wanafunzi, unawasaidia kuendeleza stadi za kufikiri na stadi za kuuliza maswali makinifu. Utajifunza pia wanafunzi wanapendelea nini na misimamo yao ni ipi. Unaweza kutumia njia hii kutimiza zaidi matakwa yao.

Uchunguzi kifani ya 1: Kusimulia hadithi kutokana na misimamo tofauti

Mwalimu Pinkie Motau wa Soweto, Afrika ya Kusini ana makasha matatu ya vitabu vya hadithi darasani mwake. Wakati mwingine anasoma vitabu hivi kwa darasa lake la 4 na wakati mwingine wanafunzi wanasoma wenyewe. Hadithi zinahusu watoto na familia, zinahusu wanyama na zinahusu viumbe vya kufikirika kama vile mazimwi.

Siku moja alipokuwa akisoma hadithi kuhusu mamba, Sizwe alisema alijisikia vibaya kuhusu mamba kwa kuwa kila wakati mamba alionekana ‘mbaya’. Wengine walisema kuwa hii ilikuwa sahihi kwa kuwa mamba ni mnyama hatari, lakini wengine walisema hii haikuwa halali kwa sababu mamba wanapaswa kujilinda kama wanyama wengine wanavyofanya. Hali hii ilimpa wazo mwalimu Motau. Aliwataka darasa kutoa maoni ya jinsi hadithi ingesimuliwa kutokana na msimamo wa mamba mwenyewe. Wanafunzi walikanganyikiwa, kwa hiyo akasema, ‘Jifikirie kuwa wewe ni mamba katika hadithi hii. Unataka kuwaambia nini wanyama wengine kuhusu hali yako?’ Swali hili liliwasaidia wanafunzi kutoa maoni. Baada ya majadiliano darasani, mwalimu Motau aliwataka kufanya kazi katika vikundi vya watu watanowatano, kuchora na kuandika hadithi ambayo itaonesha kuwa mamba ni mnyama ‘mzuri’.

Kwa kubadilishana mawazo, waliandika hadithi na kuchora picha na vielelezo kuhusu hadithi hizo zenye ubunifu wa hali ya juu.

Wakati mwalimu Motau alipokuwa akisoma hadithi hizo, alifikiria maneno na michoro ‘vilimwambia’ nini kuhusu uwezo wa wanafunzi wa kubuni hadithi kutumia msimamo wa mamba mwenyewe. Siku iliyofuata, alisoma hadithi za kila kikundi kwa sauti na kuonesha picha na vielelezo. Baada ya kusoma kila hadithi, aliliambia darasa zima kikundi kimefanikiwa katika mambo yapi, na pia aliwataka wanafunzi kutoa maoni yao kuhusu maandishi na picha za kila kikundi.

Mwishowe, hadithi hizo zilitengenezwa kitabu kwa ajili ya maktaba ya darasa.

Shughuli ya 1: Kuwa msomaji makinifu wa hadithi

Tafuta hadithi ambapo wahusika, mandhari na matukio vimeandikwa na kuchorwa kutokana na msimamo mmoja (k.m. wanyama wazuri, wazazi wa mwanafunzi mtukutu).

Isome hadithi hii kwa wanafunzi darasani, ukihakikisha kuwa umewaonesha michoro.

Waulize maswali yanayowachochea kufikiri kimakinifu kuhusu hadithi ilivyoandikwa na vielelezo vilivyochorwa. (Angalia Nyenzo-rejea 1: Uulizaji wa maswali kwa mifano ya maswali ambayo ungetumia.)

Baadaye, watake wanafunzi kufanya kazi katika vikundi vya wawiliwawili kwa kuandika barua kwa mhariri, wakifafanua wanachotaka/wasichotaka kuhusu jinsi barua waliyosoma ilivyoandikwa na vielelezo vilivyochorwa. Andika barua ubaoni na jadili mawazo na wanafunzi kabla ya wanafunzi katika vikundi vyao kuanza kuandika barua (angalia Nyenzo-rejea 2: Vidokezo vya barua kwa mwandishi ) au kwa watoto wadogo iandike rasimu hiyo pamoja.

Wanafunzi wamefanikisha nini katika masomo haya ya usomaji na uandishi makinifu? Umejuaje? Una ushahidi gani?

Wamefanya kitu chochote kilichokushangaza, kilichokupendeza au kilichokuchukiza? Kuna kitu ambacho ungefanya tofauti kama ungekuwa unafundisha masomo haya tena?

Sehemu ya 5: Njia za kuwa msomaji na mwandishi makinifu