Somo la 1

‘Kufikiri juu ya kufikiri’, au tafakuri-meta, ni njia kuu ya kuwasaidia wanafunzi waelewe na kugundua tabia za ndani za aina fulani ya maswali na jinsi ya kufanya maswali haya.

Hatua ya kwanza kwa aina hii ya kufikiri ni kuwapatia wanafunzi nafasi ya kuzungumza kuhusu maswali wanayojaribu kuyafanya na jinsi wanavyojaribu kuyafanya. Wanafunzi wanapoelezea kufikiri kwao, ni muhimu kuwasikiliza na kutopuuza wazo lolote. 

Kuna njia nyingi sana za kufanya maswali ya hisabati (angalia Nyenzo-rejea 1 ). Unaweza kushangazwa na idadi ya njia nyingine walizozipata wanafunzi, mbali na njia ambazo ulitarajia wazitumie.

Uchunguzi kifani ya 1: Kusikiliza kauli za wanafunzi katika hisabati

Mwalimu Nomonde nchini Afrika Kusini aliwakumbusha wanafunzi wake kwamba, wanaporudi nyumbani baada ya kutoka shule, hakuna njia moja tu ya kuwafikisha nyumbani: kuna njia nyingine nyingi. Baadhi ya njia hizo ni fupi sana, baadhi ndefu sana, nyingine ni salama zaidi, na nyingine zinapendeza zaidi. Aliwaambia njia hizi ni kama ilivyo katika maswali ya hisabati –mara nyingi kuna njia zaidi ya moja za kufikia jibu, na kuangalia njia hizi mbalimbali kunaweza kuwa kwa kufurahisha.

Nomonde aliandika maswali haya ubaoni.

Sipho ana mawe 24. Alimpatia rafiki yake mawe 9. Alibakiwa na mawe mangapi?

Thembeka hula pipi 7 kila siku. Ana pipi 42. Atazila hizi pipi kwa siku ngapi?

Mwalimu hununua pakiti 25 za rangi. Kila pakiti ina rangi 12. Jumla ana rangi ngapi?

Kisha aliwaambia wanafunzi wajibu maswali kwa kutumia njia yoyote waliyoipenda. Aliwapatia wanafunzi wake dakika kumi za kujibu maswali haya. Alikagua majibu yao na kisha kumwambia mwanafunzi mmoja au wanafunzi wawili waeleze jinsi walivyofanya kila swali.

Nomonde aliorodhesha njia hizi za kutafuta majibu na kunukuu zile njia zilizozoeleka zaidi. Aliwakumbushia wanafunzi wake kuhusu njia mbalimbali za kufika shuleni.

Shughuli ya 1: Kuwasaidia wanafunzi katika kufikiri

Kwanza jaribu Shughuli hii mwenyewe, inashauriwa uijaribu na wenzako wawili au zaidi. Kisha jaribu na wanafunzi wako.

Waambie wanafunzi wako wajaribu kujibu maswali matatu ya

Nomonde kwa kuyafanya wenyewe.

Ligawe darasa katika vikundi vya wanewane au watanowatano na wapeane zamu ya kuelezana hatua kwa hatua jinsi walivyopata majibu yao. 

Kisha viambie vikundi viandae orodha ya mbinu zilizotumika, kisha waulize maswali haya:

Nyote mlikuwa na jibu la aina moja/la kufanana? Nyote mlitumia njia moja/inayofanana?

Kikundi chako kinaweza kuzitumia njia hizo katika kupata jibu sahihi kwa kila swali? 

Orodhesha njia hizi ubaoni.

Eleza ni jinsi gani ilivyo muhimu kwa wanafunzi wako kujaribu njia mbalimbali katika kufanya maswali kunavyosaidia katika kufikiri kihisabati.

Sehemu ya 3: Njia za kufanya maswali ya namba