Somo la 3

Njia mojawapo ya kutathmini jinsi wanafunzi wako walivyojifunza kuelewa na kutumia lugha katika kueleza maumbo ni kwa kutumia ‘mifuko ya kuhisi/feely bags’ (angalia Nyenzo-rejea 1 kwa ufafanuzi zaidi). Mwanafunzi mmoja lazima atoe maelezo kwa makini kuhusu kitu kilichofichwa ndani ya mfuko. Mwanafunzi huyo lazima atumie maneno maalum ambayo wamejifunza, na wanafunzi wengine lazima wajaribu kukisia ni kitu gani kinachoelezwa.

Kwa namna hii, wanafunzi wanatakiwa wajenge taswira ya umbo lililomo kwenye mfuko, na kwa usahihi watumie istilahi rahisi za kijiometri walizojifunza, ikiwa wanataka ‘washinde’ katika mchezo huu wa mfuko wa kuhisi. Jinsi utakavyouandaa mchezo ili wanafunzi wote washirikishwe katika tendo hili, ni muhimu kwa sababu kama utafanyika vizuri, ujifunzaji wa wanafunzi wengi utakuwa umeboreshwa.

Uchunguzi kifani ya 3: Kucheza mchezo wa mfuko wa kuhisi katika kufanya mazoezi ya istilahi za hisabati

Bibi Chizoza alitengeneza baadhi ya mifuko ya nguo, mikubwa kiasi cha kutosha mkono wa mwanafunzi kuingia, ambayo ilikuwa na kamba ya kufungia sehemu ya juu, kwa ajili ya kuufunga mfuko kwa juu.

Alitia ndani ya kila mfuko, kimoja kati ya vitu kutoka kwenye fungu lake, baada ya kuchagua kwa makini vitu ambavyo vilikuwa vinatofautiana.

Bibi Chizoza aliufafanua mchezo kwa wanadarasa wake na alichagua mwanafunzi ambaye atafanya kazi ya kuhisi na kueleza umbo la kitu kutoka kwenye mfuko wa kwanza. Mwanafunzi huyu alitakiwa kueleza kitu hicho kwa kutumia maneno mapya waliyojifunza. Wanafunzi wengine walitakiwa kunyoosha mikono kama walifikiri wanafahamu kitu hicho kilikuwa ni nini.

Mwanafunzi ambaye aliweza kukisia kitu hicho kwa usahihi, alipata zawadi ya nafasi ya kuhisi na kueleza kitu kilichomo katika mfuko wa pili.

Alipokuwa akifanya shughuli hii, Bibi Chizoza alihakikisha kwamba wanafunzi wake wote walisikiliza kwa makini, huku akimruhusu mwanafunzi mmoja tu kuzungumza kwa wakati ili wanafunzi wengine waweze kutafakari kuhusu kinachozungumzwa na kila mmoja.

Shughuli muhimu: Kutumia mfuko wa kuhisi katika kufikiri kuhusu maumbo

Kwanza, andaa mfuko au boksi lako la kuhisi. Unahitaji mfuko au boksi ambamo utaweka kitu na mwanafunzi anaweza kuingiza mkono ili kukihisi kitu hicho bila kukiona (angalia Nyenzo-rejea 1 ).

Unaweza kuwa na mfuko wa kuhisi mmoja kwa darasa zima au, kama darasa lako ni kubwa, uwe na zaidi ya mmoja ili makundi kadhaa yaweze kufanya kazi mara moja. Hii itasaidia wanafunzi wengi kushiriki.

Kisha endelea na mchezo.

Mwanafunzi mmoja lazima ahisi kitu ndani ya mfuko/boksi na, bila ya kukitoa nje, akieleze kwa makini kwa wanafunzi wengine. Mwanafunzi huyo asitaje jina la kitu hicho.

Wanatakiwa waseme maneno kama, ‘kina sura zote bapa, kina kona nyingi sana, kina sura bapa nyingi sana’, nk.

Mchezo huu uendelee mpaka mwanafunzi mmoja afikiri kuwa wanaweza kutaja jina la kitu hicho.

Kama ni jibu sahihi, kitu hicho kitolewe nje ya mfuko, na mwanafunzi aliyefanikiwa afuatie katika kuhisi kitu kingine (lakini kwa kumpa nafasi moja tu kila mwanafunzi).

Wahimize wanafunzi wako watumie msamiati waliojifunza katika shughuli zilizopita za kueleza vitu vyao. Waambie waongezee kwenye kamusi zao za hisabati.

Nyenzo-rejea ya 1:  Kutumia mifuko ya kuhisi