Somo la 2

Katika sehemu hii, utawasaidia wanafunzi kupanua uelewa wao kwa kubadili uono wa masanduku yaliyo wazi na masanduku yaliyofungwa. Hii ina maana ya kuongeza mfuniko katika sanduku na kueleza mabadiliko yanayohitaji kufanywa katika neti.

Kwa kutumia vikundi vilevile kufanya kazi pamoja, ina maana kuwa wanafunzi wanaweza kuendeleza mawazo yao ya pamoja. Kuwaweka wanafunzi katika vikundi vipya, itamaanisha kuwa warejelee katika mawazo yao ya awali kwanza na hii itawapunguzia kasi ya kuendeleza mawazo mapya.

Katika sehemu hii, inawaonesha wanafunzi wako kuwa hakuna jibu moja tu sahihi bali kuna uwezekano wa majibu mengi. Kwa kutowaambia mengi, bali kuwauliza maswali kuongoza kufikiri kwao, utakuwa unawapa furaha

ya kugundua vitu wenyewe. Wataimarisha uwezo wao wa kujiamini na hamasa ya kujaribu mawazo mapya.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutengeza neti kwa ajili ya masanduku yaliyofungwa

Bwana Chakubanga alifurahia maendeleo ya wanafunzi wake katika shughuli ya 1 . Alieleza kuwa katika Hesabu, kwa mfano, baadhi ya maneno yana maana maalum. Kihesabu, kwa mfano, neno ‘neti’ wakati mwingine lina maana ya umbo tambarare (umbo tambarare la V2), ambalo linaweza kukunjwa kutengeneza kitu kigumu chenye umbo la V3.

Aliwataka wanafunzi wake kuongeza neno hili katika kamusi yao ya Hesabu na kutoa ufafanuzi. Kama walivyofanya mwanzoni wakati wanatengeneza neti kwa ajili ya masanduku yaliyo wazi, aliwataka watengeneze neti ya sanduku lililofungwa. Aliwashauri waangalie neti walizochora kwanza na wafikirie jinsi watakavyoongeza mfuniko. Kwa kutumia vikundi vilevile, Bwana Chakubanga, aliwataka wanafunzi kujadili pamoja namna ya kuongeza mfuniko na kuchora neti mpya. Aliwapa wanafunzi dakika kumi na kisha kuwataka kila kikundi kuchora walichokikuta ubaoni.

Halafu alikiuliza kila kikundi kuangalia neti tofauti na kukubaliana kama zote zinafanya kazi.

Shughuli ya 2: Ni neti zipi zinakunjika kutengeza mchemraba?

Hakikisha kuwa kila mwanafunzi anaelewa mchemraba ni nini, kisha waambie wanafunzi wawili wawili watafute neti nyingi tofauti kwa ajili ya mchemraba kwa kadri inavyowezekana. Kwanza wanapaswa kuchora kila neti, halafu waikate na kuhakikisha kuwa inaweza kutengeneza mchemraba, kabla ya kuanza kujaribu kuchora wavu tofauti. (Unaweza kuwaonesha mfano mmoja au zaidi kama ioneshwayo hapa chini ili waanze.)

Ungependa kulifanya hili kama shindano, likiambatana na zawadi kwa kikundi ambacho kitatengeneza neti nyingi kwa ajili ya michemraba (angalia Nyenzo rejea 2:11 neti kwa ajili ya mchemraba ).

Tena, usiingilie chochote au kuzungumza sana wakati wa somo hili; wape nafasi wanafunzi wajadiliane mawazo yao na kufurahia shughuli hiyo. Wasikilize kwa makini na pambanua jinsi wanavyoweza kufumbua matatizo yao.

Onesha michemraba iliyo tayari na, kama kuna muda, waruhusu waipambe ili kufurahia mafanikio yao.

Jadili ni neti ngapi tofauti walizopata. Watake wachore chati ya ukutani ya njia 11 zinazowezekana za neti ya mchemraba.