Somo la 1

Katika maisha yetu ya kila siku, tunaona mifano mingi ya maumbo ambayo yamebadilishwa au yamegeuzwa.

Sehemu hii itakusaidia kukuza welewa wako mwenyewe wa somo kuhusu jiometri na ugeuzi, pamoja na ujuzi wako katika kukuza welewa wa wanafunzi wako. Kwa hiyo, sehemu kubwa ya nyenzo zilizopo katika sehemu hii, zina lengo la kusaidia welewa wako wa somo ukiwa mwalimu wa hisabati.

Katika jiometri, ‘ugeuzi’ unamaanisha kubadili baadhi ya tabia za kijiometri za umbo, (kama vile kukizungusha au kutembeza sehemu zake kwenye ukurasa) wakati huo huo kuziacha tabia nyingine za umbo hilo kubaki kama zilivyo (tunasema kwamba maumbo yana ‘ulingano’).

Njia bora zaidi kwa wanafunzi ya kuumba ugeuzi ni kwa kutumia vitu halisi au kuchunguza maumbo yaliyoko katika maisha ya kila siku, na jinsi yalivyogeuzwa, mfano, katika mitindo ya vitambaa. Wakati wanafunzi wanapofanya zoezi hili, washawishi wazungumze nawe na miongoni mwao kuhusu kitu wanachochunguza. Kuzungumza kuhusu jinsi wanavyojaribu kuunda vitu halisi kutaboresha welewa wao wa jiometri na lugha inayohusiana na jiometri.

Uchunguzi kifani ya 1: Kuandaa somo la jiometri na mwenzako

Bibi Ogola, mwalimu katika shule ya msingi iliyoko Masindi, Uganda, alikuwa anajadiliana na mwenzi mwandamizi Bibi Mwanga, kuhusu uzoefu wake wa kuwafundisha wanafunzi wake jiometri. Alilalamika kwamba wanafunzi hawapendi mada hii. Wanafunzi walinung’unika kwamba jiometri ni somo dhahania sana, linalohitaji kufikiri kwingi. Mbali ya hapo, lina uhusiano kidogo au haupo kabisa na maisha halisi. Kwa hiyo, yeye mwenyewe Bibi Ogala, hakuwa na shauku ya kulifundisha.

Bibi Mwanga alikiri kuwa na uzoefu kama huo pia, lakini alimshawishi Bibi Ogala atumie mkabala wa kiuchunguzi kwa vitendo na kwa kuwahimiza wanafunzi wake wazungumze kuhusu kitu wanachotaka kukifanya katika somo hilo. Kwa pamoja waliandaa somo ambalo wanafunzi wangetenda shughuli hatua kwa hatua kwa kutumia sampuli za vitambaa vyenye mitindo ambayo inaonesha uhamishaji na tofauti za maumbo (angalia Nyenzo-rejea 1: Baadhi ya mitindo ya vitambaa vya Kitanzania ). Shughuli hii inaweza kuwaongoza wanafunzi kugundua dhana ambazo wanajifunza wenyewe.

Bibi Mwanga na Bibi Ogola wote wawili walifundisha somo hilo katika madarasa yao na kisha, baadaye walikutana kujadili jinsi lilivyokwenda. Bibi Ogala alishangazwa na kiwango cha kufikiri cha wanafunzi wake na jinsi walivyotaka kuzungumza zaidi kuhusu kitu walichokuwa wanakifanya. Bibi Mwanga alikubali kwamba kuwaruhusu wanafunzi wazungumze kuhusu kazi zao sio tu kuliwasisimua, lakini pia kuliwapa hali ya kujiamini katika uwezo wao wa kufanya hisabati.

Shughuli ya 1: Kuchunguza maumbo yanayolingana

Kukamilisha shughuli hii, utahitaji kipande cha kadibodi na penseli na rula kwa kila jozi au kundi dogo la wanafunzi, na mikasi kadhaa. Waambie wanafunzi wako wachore maumbo matatu tofauti yenye pande zilizonyooka kwenye kadi zao, na halafu, yakate maumbo yao. Wanatakiwa kuweka namba 1, 2 au

3 kwenye kila moja kati ya kadibodi zao za maumbo.

Kisha, kwenye kipande kingine cha karatasi, waambie wanafunzi wako wachore kuzuka kila umbo; halafu watembeze maumbo hayo katika mwelekeo wowote waupendao bila kupishanisha kile ambacho tayari wameshakichora, na wachore kuzunguka maumbo hayo tena. Rudia zoezi hili mpaka ukurasa ujae maumbo, kasha weak alama ndani ya kila mstari wa umbo kwa herufi (mfano, a, b, c…). (Kazi iliyokamilika lazima ilingane na Nyenzo-rejea 2: Mifano ya maumbo yanayolingana .) Waambie wanafunzi wako wabadilishane kazi zao na makundi mengine. Je, wanaweza kutafuta mistari ya maumbo iliyotengenezwa kutokana na maumbo hay ohayo? (Wanafunzi wadogo wanaweza kuhitaji kutumia maumbo ya kadibodi ili kuwasaidia.) Waambie waandike wanachofikiri kuwa ni jibu – mfano, umbo la 1, mistari ya umbo a, b, d, g.

Kwa kutumia maumbo yaliyokatwa, je, wanaweza kukuonesha kitu gain kitatokea wakiyatembeza kutoka kwenye mstari mmoja hadi mwingine? Je, wanaweza kueleza hivyo kwa maneno yao wenyewe? Watakaomaliza mapema wanaweza kutia rangi maumbo yao, watumie rangi ya aina moja kwa mistari ya umbo moja. Unaweza kutundika maumbo hayo kwenye kuta za darasa, yakiwa na kichwa cha habari, ‘Maumbo yanayolingana’.

Sehemu ya 5: Kufundisha Ugeuzi