Somo la 1

Mara nyingi wanafunzi wanapenda kufanyia kazi data walizokusanya wenyewe –wanaelewa tarakimu hizo zinaeleza nini na zimetoka wapi. Ukaguzi unawasaidia wanafunzi kuelewa dhana ya ukusanyaji data, na wanafunzi wanashauriwa kukusanya data hata nje ya mazingira ya shule.

Ni muhimu kugawa darasa katika vikundi ili kila mmoja aweze kuchangia. Majadiliano ya darasa zima yafanyike kujadili data zilizokusanywa na kila kikundi.

Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia uchunguzi/utafiti wa kundi kukusanya data

Mwalimu Msemakweli ameamua kuwa na somo la vitendo kwa kugawa darasa lake katika makundi matatu (ukiwa na darasa kubwa utahitaji makundi zaidi –angalia Nyenzo-rejea: Kufanya kazi na darasa kubwa au zaidi ya darasa moja ). Wanafunzi wake watatumia uchunguzi/utafiti wa kundi kukusanya data . Alichagua uchunguzi/utafiti wa manufaa kwa wanafunzi, kundi moja lilitafiti idadi ya ndugu katika familia, lingine idadi ya herufi katika majina yao na la tatu idadi ya wanafunzi kutoka Wilaya mbalimbali darasani.

Mwalimu Msemakweli alichora jedwali kama lililoonyeshwa kwenye Nyenzo - rejea 1: Chati ya ulinganisho kwenye ubao. Aliwapa wanafunzi muda wa kunakili jedwali kwenye madaftari yao. Baada ya hapo, alizungukia kila kundi akielekeza ujazaji wa jedwali kwa kutumia maswali ya uchunguzi/utafiti.

Mwishowe makundi yalishirikishana data zao na kuzibandika sehemu ya wazi darasani. Mwalimu Msemakweli atatumia data hizo katika vipindi vitakavyofuata.

Shughuli ya 1: Ukaguzi wa darasa zima

Kabla ya kuanza, lielekeze darasa jinsi ya kulinganisha data (angalia Nyenzo - rejea 1 ). Waulize kwa nini wanafikiri hii inaweza kuwa njia bora?

Lieleze darasa kuwa litafanya utafiti juu ya siku za kuzaliwa. Waagize waeleze njia bora ya kuorodhesha miezi mbalimbali katika Mwaka. Baada ya hapo, kila mwanafunzi ataje siku na mwezi wake wa kuzaliwa huku wengine wakinakili data hizo kwenye madaftari yao..

Kisha mtake mwanafunzi mmoja kwa kila mwezi kuhesabu idadi ya siku za kuzaliwa.

Unaweza kupanua zoezi hili kama zoezi la nyumbani kwa kuagiza wanafunzi wakusanye data juu ya mchezo au kinywaji maarufu katika familia au kwa marafiki. Katika somo linalofuata, eleza data hizo zinaonyesha nini. Ili kuimarisha mbinu za kukusanya data, lipe darasa nafasi ya kuchagua data zingine wanazoweza kukusanya.

Je ni njia zipi zingine utakazotumia kuwapanga wanafunzi kufanya kazi hiyo?

Sehemu ya 3: Kujadili data