Somo la 3

Sehemu hii ya mwisho inahusu kuchunguza na kutafsiri data baada ya kuwasilishwa. Itakusaidia kupima ufanisi wako katika kufundisha. (kwa maelezo zaidi angalia Nyenzo Rejea Muhimu: Kupima kujifunza ).

Kwa kutumia taarifa kutoka kwa mwalimu wa sayansi au mwalimu wa somo lingine, onyesha kuwa ukusanyaji na uchambuzi wa data ni muhimu katika mtaala; inakusaidia kufanya kazi na walimu wengine na kupata msaada wao. Uchunguzi Kifani 3 na Shughuli Muhimu ziaonyesha jinsi wanafunzi wanavyoweza kutumia data mpya na jinsi unavyoweza kuzitumia kupima ufahamu wao.

Unaweza kutumia dodoso lililoandaliwa (angalia Nyenzo rejea 3: Maswali yaliyoandaliwa ) kwa upimaji, ili ufahamu kiasi ambacho kila mwanafunzi amejifunza.

Uchunguzi kifani ya 3: Kupima ufahamu wa kushughulikia data

Mwalimu Lekani alitaka kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanajiamini katika kushughulikia na kutafsiri data. Alitaka pia kuwaonyesha taarifa wanazoweza kupata kwenye chati.

Alimwomba mwalimu wa sayansi, Mwalimu Kimaryo, ampatie data za mvua za eneo hilo kwa kipindi cha mwaka uliopita. Aliwaelekeza wanafunzi kutumia data hizo kuchora chati ya kuziwasilisha vizuri.

Data zilizotolewa na Mwalimu Kimaryo zinapatikana kwenye Nyenzo –rejea 4: Kiasi cha Mvua Dar es Salaam .

Mwalimu Lekani aliwataka wanafunzi wafanye kazi wawili wawili ili waweze kusaidiana. Wote walitakiwa wakubaliane juu ya aina ya chati ya kutumia.

Vilevile aliwataka wazingatie kichwa cha habari, vipimo vilivyotumika, maudhui, alama ya juu na chini pamoja na mambo mengine kwenye chati, na kuandika maelezo mafupi kufafanua chati imeonyesha nini.

Mwalimu Lekani alifurahishwa na majibu aliyopata na akahisi kuwa somo lilieleweka vizuri. Alibandika chati za wanafunzi kwenye ukuta wa darasa.

Shughuli muhimu: Kupima uchambuzi na tafsiri ya data

Ili kupima jinsi wanafunzi wanavyoweza kuchambua na kutafsiri data, unaweza kutumia dodoso la maswali yaliyoandaliwa ambayo ugumu wake unaongezeka. Hii ina maana kuwa unaanza na maswali rahisi yanayoweza kujibiwa na wote, halafu unaendelea na maswali magumu kiasi yatakayojibiwa na wengi wao, na mwishowe maswali magumu yatakayojibiwa na wale wenye uwezo tu.

Andika data kwenye chati ubaoni au kwenye karatasi. Andika maswali kwenye karatasi nyingine.

Onyesha chati na maswali darasani. Waeleze watakavyofanya kazi wenyewe, wakichora chati na kisha kujibu maswali mengi itakavyowezekana.

Lipe darasa kipindi kimoja kukamilisha shughuli hii. Kusanya kazi na kuisahihisha.

Kipindi kijacho lipatie darasa mrejesho wa jinsi walivyofanya kazi, sehemu wanayohitaji msaada na jinsi utakavyowasaidia.

Nyenzo-rejea ya 1: Chati ya mlinganisho