Somo la 3

Tunapendekeza uwapange wanafunzi kufanya kazi katika vikundi, wanafunzi watatu au wanne katika kila kikundi hufanya kazi vizuri. (Tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia kazi ya vikundi darasani kwako ili ikusaidie kuamua jinsi utakavyopanga vikundi.) Unaweza kupanga vikundi vyako kwa kuchanganya wasiofanya vizuri na wale wanaofanya vizuri.

Wahimize wanafunzi walete vifaa kwa ajili ya modeli zao. Wanapokuwa wakiunda modeli, zungukazunguka darasani, ukizungumza na vikundi; kwa wanafunzi wadogo zaidi uwatake wataje sehemu za mnyama wanayemuundia modeli - nyayo, mikia, masikio na kadhalika. Kwa wanafunzi wakubwa zaidi, uwaulize maswali juu ya maumbo na kazi za sehemu mbalimbali za wanyama –zinamasaidiaje mnyama kujongea? kula? kuhifadhi joto? kupoa? kuhisi kuwa mnyama mla wanyama yuko karibu?

Fikiria jinsi unavyoweza kuwahamasisha wanafunzi wako kutafakari kazi yao. Unaweza kuvitaka vikundi mbalimbali kutoa maoni juu ya modeli za vikundi vingine? Hakikisha unatoa muda kwa wanafunzi wazungumzie kazi zao na kuziboresha.

Shughuli hii imeenda vizuri?

Umeshangazwa na tondoti za modeli za wanafunzi? Je, tondoti za modeli za wanafunzi ni sahihi?

Kipi kingeweza kuboreshwa?

Imewasaidia wanafunzi kuona ufanano na tofauti baina ya wanyama?

Katika sehemu hii tumekuwa tukitalii sulubu za viumbe hai. Kuna sulubu za msingi kwenye duru ya maisha ya viumbe hai wote. Kuna urutubishaji na ukuaji wa kiinitete katika mbegu/yai/mimba. Kisha kuna mchakato wa uzaliwaji/uanguliwaji/uotaji. Baada ya hapo kuna ulaji na ukuaji kupitia hatua kadhaa. Kwenye upevukaji, hatua ya mwisho ya uzaaji inaweza kutokea na duru inaanza tena.

Katika Uchunguzi Kifani 3 walimu hutumia magurudumu ya hadithi kuwasaidia wanafunzi kuelewa sulubu hii katika duru za maisha.

Magurudumu ya hadithi ni zana zinazofaa za kutumia kwa sababu: huonesha hatua katika duru ya maisha ya mmea au mnyama; husaidia wanafunzi kupanga mawazo yao kuhusu duru za maisha;

huwasaidia wanafunzi kutoka kwenye mambo wanayofahamu kwenda kwenye mambo wasiyoyafahamu –kutoka kwenye picha kwenda kwenye lebo za istilahi za kisayansi.

Soma uchunguzi kifani kwa maelezo zaidi juu ya jinsi magurudumu ya hadithi yanavyoweza kutumiwa na wanafunzi.

Unaweza kujaribu magurudumu ya hadithi na madarasa yako; kuna lebo na michoro kadhaa ya kukusaidia katika Nyenzo-rejea 6: Gurudumu la hadithi la duru ya maisha ya harage .

Aina zote za viumbe vyenye uhai zina sulubu ya duru ya maisha iliyo tofauti waziwazi. Wanafunzi watavutiwa kufahamu jinsi viumbe tofautitofauti vyenye uhai vilivyobadili duru zao za maisha vyenyewe. Baada ya kujadili sulubu ya msingi ya maisha darasani, na labda kufanya magurudumu ya hadithi, wanafunzi wako watakuwa tayari kufanya miradi ya utafiti ya duru za maisha yao wenyewe katika Shughuli muhimu . Shughuli hii imejikita juu ya uchunguzi wa viumbe vyenye uhai katika mazingira yao. Wanafunzi huwajibika kwa kupanga, kufanya, kuripoti na kutathmini ujifunzaji wao yenyewe kuhusu mnyama waliomchagua. Mwishoni mwa shughuli, ni muhimu kuchunguza duru zote za maisha na kujadili jinsi zilivyo na sulubu ileile ya msingi.

Unaweza kutaka kusoma Nyenzo-rejea muhimu: Kufanya utafiti darasani ili ikusaidie kupanga shughuli hii.

Uchunguzi kifani ya 3: Magurudumu ya hadithi –sulubu za duru za maisha ya mmea

Bibi Mputa alilikusanya darasa lake kumzunguka, akainua ganda la kijani la harage na kutoa hadithi ya duru ya maisha ya harage. Alitumia maneno mche, umeaji, ukuaji, na mmea mpevu ili wanafunzi wajifunze maneno sahihi.

Kisha akaligawa darasa katika vikundi vinne: Kikundi cha 1 na cha 2 vikapewa michoro mitatu inayoonesha hatua mojawapo katika duru ya maisha ya harage, Kikundi cha 3 kilikuwa na lebo mstatili (zikielezea michoro) na Kikundi cha 4 kilikuwa na lebo za mviringo (zikielezea hatua katika hadithi ya duru ya maisha). Nyenzo-rejea 6 inaonesha lebo na michoro hii.

Kisha Bibi Mputa alichora duara kubwa ubaoni na kuigawa katika sehemu sita zilizo sawa. Akakitaka kikundi chenye mchoro wa kwanza kuja na kuuweka katika gurudumu la hadithi. Akauliza nini kilifuata, na kuwataka wanafunzi kuweka mchoro katika gurudumu la hadithi. Baada ya kila sehemu katika gurudumu kuwa na mchoro, alikielekeza Kikundi cha 3 kuweka lebo za michoro. Mwishowe, Kikundi cha 4 kikaweka lebo zake katika mfuatano kwenye gurudumu la hadithi na kuelezea hatua kwa darasa. Alimalizia kwa kuwataka wanafunzi wanakili gurudumu la hadithi na kuelezea kwa maneno yao wenyewe hadithi ya duru ya maisha ya harage –wangeweza kuanza popote kwenye duru.

Bibi Mputa aliona kwamba somo hili lilienda vizuri, na wanafunzi wake wakataka kufanya magurudumu ya hadithi kwa mimea na wanyama wengine.

Shughuli muhimu: Miradi kazi ya duru ya maisha ya wanyama

Panga darasa lako katika vikundi vya watatuwatatu au wannewanne.

Kwa kushirikiana na wanafunzi wako, andaa orodha ndefu ya wanayama wanaoweza kupatikana katika mazingira ya mahali hapo. Andika orodha hii ubaoni au kwenye kipande kikubwa cha karatasi kitakachobandikwa ukutani.

Ukitake kila kikundi kuchagua mnyama katika orodha; jaribu kuhakikisha kwamba vikundi viwili visichague mnyama yuleyule. Mapendekezo ni pamoja na: senene, kipepeo, chura, kasa, mbu, kombamwiko, tembo, ndege na samaki.

Lipatie darasa mwongozo wa msingi kwa kazi za duru za maisha; wana muda kiasi gani, unatarajia nini kutoka kwao na jinsi wanavypaswa kuonesha kazi zao. Kwa wanafunzi wadogo zaidi, ungewatarajia wachore michoro mitatu/minne katika umbo la gurudumu la hadithi na kuweka lebo za msingi kwenye michoro kwa mfano yai, kifaranga, kiumbe kizima, kichanga na kuwa na michoro katika mpangilio sahihi. Wanafunzi wakubwa zaidi hawana budi kuweza kugundua kitu kuhusu kila mojawapo ya hatua hizi tano:

Dume linakutana na jike

Manii ya dume yanafikia yai la jike

Yai linakuwa mimba

Mnyama mpya anakua

Mnyama mpya anakuwa mkubwa

Hawana budi kuchora michoro ya wazi yenye lebo na maelezo ya wazi. Wanapaswa kuingiza idadi ya vichanga vinavyozaliwa pamoja, wakati kwa kila hatua na jinsi mnyama anavyopata chakula chake kwa kila hatua. Utahitaji kuwaelekeza ili wafanye kazi kwa uhuru wa kutosha kwa kujiamini. Njia mojawapo ya kuwasaidia wanafunzi ni kuwa na orodha ya maneno yanayofaa kwenye ukuta wa darasa; wanaweza kujihisi kujiamini katika kuendeleza maneno hayo.

Kitie moyo kila kikundi kianze kurekodi wanayofahamu kuhusu mnyama wao. Kisha wajue zaidi kwa uchunguaji na utafiti. Wanafunzi wanaweza kutaka kuwauliza watu katika jumuiya hiyo au kutumia vitabu au tovuti (tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kutumia teknolojia mpya) kama hivi vinapatikana.

Katika kufanya kazi kwa namna hii, wanafunzi wako hakika watakuwa wakifikiri na kutenda kisayansi. Wanafunzi wako walionekana kuvutiwa na shughuli hii? Unafikiri wamejifunza nini?

Nyenzo-rejea ya 1: Kielelezo cha Familia ya Kiafrika