Nyenzo-rejea ya 2: Uzazi katika mimea itoayo maua

Nyenzo ya Mwalimu kwa kupanga au kubadili nyenzo ili zitumike na wanafunzi.

Maua yana sehemu za uzazi za mmea- yanatoa mbegu ambazo mmea mpya hutokea. Mimea itoayo maua huzaliana kwa seli mbili maalumu za jinsia zikiungana pamoja. Seli ya jinsia ya kiume (poleni) huunganika na seli ya jinsia ya kike (ovamu) kuwa seli ya kwanza ya kiumbe kipya. Seli hii baadaye hugawanyika na kuwa mbili, nne, nane….na kuendelea hadi kunakuwa na mamilioni ya seli kwenye mbegu. Baadaye mbegu huota na kukua kuwa mmea mpya.

Mchoro unaonyesha sehemu za ua:

Stameni ni sehemu za ua za kiume.

Chavulio, juu ya stameni, lina maelfu ya chembe chembe za poleni. Kila chembe ya poleni ina seli ya jinsia ya kiume.

Kapeli ni sehemu ya kike ya ua. Chini ya kapeli kuna sehemu iliyovimba- hii ni ovari.

Ovari ina ovuli kadhaa.

Kila ovuli ni seli ya jinsia ya kike na inaitwa seli ya yai.

Ovuli ni kubwa kuliko chembechembe za poleni- wakati mwingine unaweza kuziona kwa kutumia lenzi ya mkononi.

Mimea inahitaji msaada kupata chembechembe za poleni kutoka kwenye stameni hadi juu ya kapeli ya ua jingine la aina hiyo: hii inaitwa uchavushaji mtambuka (Uchavushaji—nafsi ni pale ambapo inatokea kwenye ua hilo hilo).

Katika mimea ya uchavushaji mtambuka, stameni kwa kawaida huiva na kutoa poleni kabla kapeli hazijawa tayari ili uchavushaji-nafsi usitokee.

Baadhi ya mimea hutumia wadudu kusaidia uchavushaji. Mdudu, anatafuta chakula, anavutiwa na ua. Poleni inajigusisha kwenye mwili wa mdudu na kung’ang’ania. Mdudu anaenda kwenye ua jingine na baadhi ya poleni itaangukia kwenye kapeli ya ua hilo la pili.

Maua yanayotumia wadudu kusaidia uchavushaji kwa kawaida yana petali angavu, harufu nzuri na poleni zinazojishikiza.

Baadhi ya mimea hutumia upepo kusaidia uchavushaji. Mimea hii kwa kawaida ina sehemu za kike na za kiume ambazo ziko nje ya ua. Kwa kawaida hayana rangi angavu na chembechembe zake za poleni ni ndogo na nyepesi.Nyasi huchavushwa kwa njia hii.

Baada ya uchavushaji, neli hutokea kwenye poleni na kushuka hadi kwenye ovari. 

Kwenye ovari, nyuklia ya seli ya jinsia ya kiume huungana na seli ya jinsia ya kike- huu ni utungisho.

Ovuli zilizotungishwa hukua kuwa mbegu na ovari hubadilika na kuwa tunda.

Mifano ya uchavushaji

Uchavushaji wa wadudu

Nyenzo-rejea ya 1: Kuangalia mimea

Nyenzo-rejea ya 3: Kuandaa ufuatisho wa mimea ya asili