Somo la 2

Mimea na wanyama hubadilika kulingana na viwango mbalimbali vya hali za nchi. Ukweli huu huunda mada inayosisimua ya kujifunza.

Unaweza kupata mengi ya kushughulikia toka kwenye picha na sampuli za mimea na wanyama zihusuzo jinsi gani wanavyoishi na mahali gani wanakoishi. Madokezo ni:

umbo lote la mwili;

aina ya mwonekano wa nje;

uwiano wa sehemu za mwili;

maumbo au mipangilio yoyote ya sehemu ambayo si ya kawaida. Tunafanya hivi katika michakato ya upunguzaji. Shughuli 2 inaonesha

jinsi unavyoweza kuhimiza ukuaji wa ujuzi huu kwa kuchunguza wanyama

wadogo waliopo katika maeneo ya shule. Kama una vitabu vinavyofaa, unaweza kuendeleza zoezi hili kwa kutumia picha za wanyama wengine au kwa kutafakari kuhusu wanadamu.

Katika Uchunguzi-kifani 2 , mwalimu anawasaidia wanafunzi wake kuendeleza tafakuri zao za kisayansi kwa kuzingatia uchunguzi wa mwanafunzi mmoja. Soma sehemu hiyo kabla ya kufanya shughuli ya hapo juu na darasa lako.

Unaweza kuliuliza darasa lako kuhusu jinsi wanyama wanavyobadilika katika mazingira yenu wenyewe.

Uchunguzi kifani ya 2: Mimea katika maeneo makavu

Alias Morindat alikulia, na anafundisha katika mkoa mkavu wa Dodoma. Kila baada ya miaka michache, huliambia darasa lake la mchanganyiko, darasa la kilimo la shule, kuorodhesha mbinu mbalimbali ambazo mimea ya mahali hapo imeumbwa ili iendelee kuishi katika mazingira makavu.

Mara zote hufurahishwa na kiwango tu cha maarifa wanafunzi wanachotoa, namna wanavyorekodi chunguzi zao na mahitimisho kwenye wazo elekezi shirikishi. Katika kutathmini kazi yao, wanafurahia kuilinganisha kazi yao na kazi za miaka michache iliyopita (ikiwa ni pamoja na kazi za kaka na dada zao wakubwa). Hapa kuna mfano mmoja wa jinsi kazi hii inavyoweza kuwahamasisha wanafunzi kuunda mihtasari toka kwenye chunguzi zao. Mwaka mmoja, mwanafunzi alifanya uchunguzi huu ‘Hapa katika mkoa wa Dodoma, mimea mingi ina miiba kuliko mimea iliyo karibu na Tanga (pwani).’ Kitu gani kinaweza kufupishwa kutokana na uchunguzi huu? Je, miiba ni muhimu katika ukabilianaji wa mimea iliyo kwenye eneo kavu – kwa nini?

Alias aliwaambia wanafunzi watafakari kuhusu jambo hili. Wengi walikubaliana kwamba kuna faida kuwa na miiba kwa sababu mimea iliyo katika sehemu kavu haiwezi kurudishia kwa urahisi sehemu za kijani zilizoliwa na wanyama. Mtoto mmoja aligundua jinsi watu katika maeneo oevu zaidi wanavyohimiza uoto mpya kwa kukata matawi. Baadhi waligundua kwamba mimea mingine inachanganya pia miiba na ladha chungu au majimaji yanayowasha. Tabia hizi huizuia mimea hiyo kuliwa. Walifupisha kwamba lazima iwe muhimu sana kwa uhai wa zerofita (mimea ambayo huishi, au hata kustawi, katika maeneo yenye unyevu kidogo sana) kutohitaji kurudishia sehemu zilizoliwa/zilizopotea.

Shughuli ya 2: Wanyama wadogo –uhai hapo nje ya darasa

Shughuli hii inahitaji mifuko mitupu ya plastiki laini. Lipe kila kundi la wanafunzi watatu/wanne mfuko mmoja. Kisha, liambie kila kundi kwenda nje (chini ya usimamizi wako) na kukamata aina moja ya wanyama wadogo tofauti –sio wale wanaong’ta au kuchoma au wenye sumu –panzi, kwa mfano. Wakirudi darasani, makundi yachunguze mnyama wao mdogo, ambaye anaonekana kwa urahisi na amewekwa kwa usalama pamoja na hewa ya kutosha kumwezesha kuishi mpaka atakapoachiliwa.

Wanarekodi chunguzi zao zote kwenye karatasi ya wazo elekezi.

‘Alichukuliwa toka wapi’ na ‘Alikuwa anafanya nini’ zinarekodiwa juu kulia. Taarifa zihusuzo jinsi anavyoonekana zinarekodiwa kwa uangalifu upande wa chini kulia. Upande wa chini kushoto, waorodheshe kile ambacho tayari wanakijua kuhusu kiumbe huyo; na upande wa juu kushoto utumike kwa maswali watakayoyaibua.

Katika darasa la mchanganyiko, unaweza kuwaambia wanafunzi wakubwa kushirikiana na wanafunzi wadogo kwa kuwasaidia wanafunzi wadogo kurekodi chunguzi na maswali yao.

Makundi yabadilishane chunguzi na maswali, na kuongezea taarifa kutoka kwa wanafunzi wengine kwenye mawazo elekezi yao. Kisha, watafakari kwa makini kuhusu kitu cha ziada wanachoweza kuongezea kwa kutumia rangi nyingine kwa kila uchunguzi au swali waliloliandika. Tendo hili litawasaidia kukuza tafakuri yao.

(Angalia Nyenzo-rejea 3: Wanyama wadogo kwa mifano.)