Nyenzo Rejea 6: Kufikiria kiumwengu- kutenda kimahali

Mfano wa kazi za wanafunzi

1. Kutana

Wapeleke wanafunzi nje kwa matembezi manne mafupi. Waeleze kuwa unawataka watumie aina zote za ufahamu. Wanahisi nini, kuona, kunusa nini?

Tumia shule kama msingi/chanzo. Tembea kutoka shuleni kuelekea mashariki. Tembea kiasi cha mita 500 hadi sehemu salama kusimama. Mtake kila mmoja kusimama kimya akiangalia mashariki kwa dakika chache huku wakiwa wamefumba macho, na uwe makini kama wanahisi,wanasikia na wananusa.

Halafu, wakiwa macho wazi, waamuru kuchunguza kwa uangalifu vitu vyote vinavyoonekana mashariki mwa shule. Wanaona nini katika mazingira? Halafu watake kufikiri juu ya rasilimali, rasilimali zilizo nje ya upeo wao lakini ziko upande huo huo. 

Waambie kuwa kadili wanavyotembea taratibu kurudi shuleni unataka wafikiri kuhusu nini wamekifahamu. Wakiwa darasani wape nafasi kuandika mawazo yao kwenye daftari au kwenye bango

Rudia hatua hii, tembea kuelekea upande wa kaskazini, kusini, na maghariki.

2. Rasimu ya kwanza

Unahitaji kuamua au kujadili na wanafunzi namna mnavyoweza kupata matokeo ya hisia juu ya mazingira.

Mnaweza kusafisha meza, weka kiberiti katikati kuwakilisha shule, na halafu andika majina ya rasilimali mbalimbali juu ya kadi. Kadi zinaweza kuwekwa katika sehemu kuwakilisha uelekeo na umbali wa kila sehemu au umbo. Unaweza kupaka rangi kusudi kadi moja ya rangi fulani iwakilishe umbo asili, na rangi nyingine iwakilishe umbo la kutengenezwa. Labda kama kuna barabara, mto au mkondo wa maji, unaweza kutumia utepe au kipande cha nguo, kamba, uzi, au sufu kuonyesha umbo na uelekeo.

Unaweza kuchora mchoro ubaoni, au unaweza kutumia kipande cha karatasi uwe na kumbukumbu ya kazi hii. Unaweza kwenda nje na kutambua maumbo kwenye eneo wazi. Unaweza kutumia mawe kushikizia jina lolote lililoandikwa kwenye karatasi. Kuna namna nyingi.

Matokeo ya mwisho yawe yale ambayo wewe na wanafunzi mna taswira ya juu juu/ kielelezo /ramani ya mahali mnayorithia.

Wewe na wanafunzi wako sasa mko tayari kwa hatua inayofuata. Hii itakuwa ni kuorodhesha na kujadili matatizo au hatari wanazozijua kwa watu au mazingira yenyewe.

3. Uwasilishaji wa tafiti

Kama kazi imefanyika vizuri, wanafunzi watahitaji kuanzisha mradi fulani. Hii inaweza kuwa kutengeneza picha ya kudumu katika ukuta wa shule juu ya kile tunachoweza kupata kutoka mazingira.

4. Kukubaliana na mpango

Umeanza mchakato wa kuongeza ufahamu juu ya mazingira na wanafunzi wamekuwa wakifanya baadhi ya utafiti. Hii itapelekea kuwa na uelewa wa matatizo au changamoto za mazingira.

Tumia muda fulani na wanafunzi wako kujadili matatizo au changamoto za mazingira na njia zinazoweza kutumika kutatua au kukabiliana na changamoto hizo. Shirikisha mawazo yote mbadala. Tumia dakika chache kutoa maoni yako na hisia zako kadili unavyoshirikiana na wanafunzi katika kukubaliana na kile kinachotakiwa kufanywa, na njia mojawapo zinazoweza kutumika. Panga muda kwa kipindi kinachofuata na waombe wanafunzi kuendelea kutafakari kwa muda wao, na hata kuwashirikisha watu wengine majumbani kwao kile wanachofikiria.

5. Kubuni mpango wa utekelezaji

Katika kipindi kinachofuata, mtakuwa mnabadili mawazo yenu kuwa mapendekezo na kutoa maoni ya kujenga juu ya mawazo yaliyotolewa. Hatua hii ni muhimu sana. Zingatia namna mawazo yanavyoboreshwa na changamoto zake. Hakikisha wanafunzi ambao hawaongei wanashirikishwa kikamilifu.

Matokeo ya kipindi hiki yawe ni makubaliano ya mpango yaliyowekwa kimaandishi. Waambie wanafunzi kwamba mpango utawekwa katika utekelezaji.

Kabla hujamaliza, tumia muda kidogo na wanafunzi wako kutathmini mchakato wa kutengeneza mpango wa utekelezaji. Nini kimeenda vizuri? Nini kingesaidia vitu viende vizuri? Ni vipengele vipi vinaweza kuhitaji marekebisho?

6. Utekelezaji

Hatua hii itategemea wanafunzi na aina ya mradi. Jukumu lako litakuwa kuwahamasisha, kuwasifu na kuwasaidia. Utafanya hili kwa kurahisisha njia, kuhakikisha kuwa wapo salama kwa chochote wakifanyacho na kuwapa mrejesho chanya na ushauri mzuri.

Kumbuka kwammba hatua ya utekelezaji wa baadhi ya miradi inaweza kuchukua majuma kadhaa hata miezi lakini unahitaji kuhakikisha kuwa unatunza vizuri kumbukumbu za maendeleo (nini kimetokea) kusudi uweze kutoa ripoti ya maendeleo ya kazi kwa kila hatua.

7. Kutathmini matokeo na ripoti

Ijapokuwa hii inaweza kuonekana ni shughuli ya mwisho, inaweza isiwe hivyo. Mchakato endelevu wa kutathmini maendeleo lazima uwepo. Muda maalumu lazima upangwe kutoa ripoti juu ya namna vitu vinavyoenda na ‘mafanikio’ na ‘matatizo’ ya mradi.

Imenukuliwa kutoka: Umthamo 39, Chuo Kikuu cha Fort Hare, Mradi wa Elimu ya Masafa.

Nyenzo-rejea 5: Dhana wanayoweza kuwa nayo wanafunzi juu ya kufanya kazi katika makundi