Somo la 1

Ni muhimu sana wanafunzi wapewe nafasi ya kufikiria na kutenda kisayansi. Hii inaweza kutokea tu panapokuwa na vitendo, shughuli za mikono. Wanafunzi watapata changamoto na kufurahia kufanya kazi wakiwa kwenye makundi kujadili na kugundua vitu wao wenyewe. Mara nyingi hii huwasaidia wanafunzi wanapotumia mifano na vifaa halisi.

Shughuli 1 inatumia maumbo ya kutengeneza kuwasaidia wanafunzi kuelewa mahitaji ya saketi kamili ya kifaa cha umeme. Uchunguzi kifani

1 unaonyesha jinsi mwalimu mmoja alivyoendeleza shughuli yake na kuwasaidia wanafunzi wake kuchunguza juu ya saketi ya umeme. Aina hii ya mhimizo na ugunduzi ni muhimu sana kwa wanafunzi.

Nyenzo rejea 1: Kuangalia kwa makini tochi ya balbu inakuonyesha namna unavyoweza kuandaa shughuli hii na kuwaongoza wanafunzi kwenye uelewa mzuri kwamba umeme husafiri katika saketi kamili ndani ya balbu ya tochi.

Pia unaweza kupata msaada ukisoma Nyenzo rejea 2: Njia salama za kuchunguza umeme , ambayo inaelezea hatari za umeme lakini inakuhimiza usitishwe na mada hii.

Uchunguzi kifani ya 1: Uchunguzi wa Wanafunzi

Pindi mwalimu Florence wa Uganda alipojaribu Shughuli 1 na darasa lake, aligundua kuwa baadhi ya wanafunzi walienda mbele zaidi kwa uchunguzi. Walitambua kuwa ncha ya metali ya bolpeni itaweza kufanya balbu iwake ikiwekwa kati ya ncha ya juu ya betri na sehemu ya chini ya balbu. Aliwaangalia wakiendelea na uchunguzi wa vifaa vingine; penseli ya mti haikuweza kuwasha balbu, wala kipande cha kadibodi, lakini ncha ya kijiko cha metali iliwasha balbu.

Florence aliwapa nafasi ya kutoa ripoti ya uchunguzi wao na kuwahimiza warudie na kuchunguza zaidi. Baadaye, aliiendeleza shughuli kwa kuchunguza mizunguko ya umeme na swichi.

Aliwaambia wanafunzi wake watumie balbu zao na betri (na vifaa vingine) kutengeneza saketi ili pindi mgeni abonyezapo swichi mwanga unatokea. Wanafunzi walitumia vibanio vya karatasi, vipande vidogo vya mbao, kadi na metali kutoka kwenye makopo ili kutengeneza swichi.

Halafu, baadhi ya wanafunzi wakubwa walitengeneza mifano ya vyumba vya maboksi na vifaa vingine na kuweka taa mbili au tatu na swichi. Kundi moja liliweza hata kuongeza taa ya tahadhari, ambayo iliwaka mara mwizi anapofungua mlango wa chumba cha mfano. Florence alionyesha mifano yote hii darasani kwake na kuwaalika waalimu wengine kuja na kuangalia wakati wanafunzi wakieleza jinsi walivyofanya kazi. Waalimu wenzake walifurahi sana kuona mafanikio ya wanafunzi na kila mmoja aliufurahia mchana huo.

Shughuli ya 1: Kuwasha balbu ya tochi

Kila kundi la wanafunzi linahitaji tochi moja ya kutumia betri, balbu moja ya tochi inayofanya kazi, nyaya mbili za shaba zilizofunikwa kwa plastiki za urefu wa sm 15, maumbo matano ya tochi na balbu tano. (Angalia Nyenzo rejea 3: Kuwasha balbu – vielelezo na majadiliano –inachukua muda sana kutengeneza maumbo, ungeweza kuwaambia wanafunzi wakubwa kukutengenezea maumbo kabla ya somo kuanza.) Vile vile wanahitaji kadi kubwa isiyoandikwa au karatasi na kiasi kidogo cha gundi. (Hakikisha kuwa betri na balbu zinafanya kazi kabla ya somo kuanza).

Kipatie kila kikundi balbu na tochi. Uliza ‘Tunapata nini kutoka kwenye hivi vifaa?’ Wanaweza wakaonyesha? Ni kitu gani zaidi wanahitaji?

Wape maumbo yaliyotengenezwa pamoja na nyaya. Waambie wanafunzi wachunguze mipangilio mbalimbali kuona kama wanaweza kuwasha balbu. Mipangilio inayofanikiwa inarekodiwa kwa kuunganisha maumbo kwa gundi na kuweka sehemu ya waya.

Waambie:’ kuna zaidi ya mpangilio mmoja ambao unaweza kuwasha balbu’. Wahimize watafute mipangilio mingine mitano inayoweza kuwasha balbu.

Mwishoni mwa kipindi makundi yanaeleza kazi zao. ( Nyenzo rejea 3 inajadili shughuli hii kwa undani zaidi na inakuonyesha mipangilio mitano inayoweza kuwasha balbu).

Sehemu ya 3: Kuchunguza umeme