Somo la 3

Shughuli muhimu inajenga mawazo ya kubadilika kwa nishati na hitaji la kukamilisha mzunguko wa nishati. Kwa hiyo, wanafunzi hufanya kazi katika makundi madogo kuchunguza tukio moja la umeme-‘sumaku umeme’. Aina hii ya shughuli huwahimiza wanafunzi kufikiri juu ya michanganuo mbalimbali ya kisayansi- kupanga, kuchunguza na kuweka kumbukumbu. Baada ya shughuli, wanafunzi wanaweza kufikiri juu ya matumizi ya sumaku-umeme (Angalia Nyenzo rejea 5: sumaku-umeme kwa mawazo zaidi).

Uchunguzi kifani 3 unaonyesha jinsi mwalimu mwenye nyenzo chache anavyowasisitiza wanafunzi wake wafikirie juu ya michakato inayojumuishwa katika uchunguzi kama huu.

Uchunguzi kifani ya 3: Kuchunguza sumaku-umeme kwenye nyenzo chache

Bibi Kolimba anafanya kazi kwenye shule ya kijijini yenye vifaa vichache. Hupenda kufanya ufafanuzi kwa vitendo na wanafunzi wake na wakati wote hutafuta vifaa vilivyoharibika kijijini ili kutengeneza vifaa vya kutumia darasani.

Siku moja, aliusambaratisha mtambo wa umeme mkuukuu kama mfano wa sumaku-umeme. Aliuandaa juu ya meza yake na kuwakusanya wanafunzi wake kumzunguka. Aliwaonyesha kuwa alikuwa anatumia umeme kutengeneza sumaku. Halafu aliwaambia kila mmoja ajadili na mwenzake namna ambayo angeweza kuifanya sumaku iwe na

nguvu-angeweza kubadili kitu gani? Wangewezaje kupima nguvu ya sumaku?

Baada ya dakika chache, Bibi Kolimba aliwaambia wanafunzi wachangie mawazo yao na aliandika maoni/ mapendekezo ubaoni. Baadhi ya wanafunzi walidhani kuwa angetumia zaidi betri za tochi, sumaku ingepata nguvu zaidi. Wengine walishauri kutumia vitu mbalimbali katikati. Ushauri mwingine ulihusisha waya mrefu, mizunguko mingi ya nyaya kuzunguka eneo la katikati na kutumia ncha mbili za waya. Bibi Kolimba aliwaambia wanafunzi wawiliwawili kutoka na kujaribu moja kati ya mawazo yaliyopatikana. Waliandika majibu yao kwenye jedwali ubaoni. Kundi lingine lilijaribu wazo tofauti, na kuendelea, hadi walipokuwa wamejaribu mawazo yote. Wanafunzi walinakili jedwali na matokeo yake, halafu, wakiwa na wenzao, walijaribu kuandika sentensi za muhtasari kwa kile walichokiona.

Bibi Kolimba alifurahia sana namna darasa lake lilivyosikilizana, lakini aligundua kuwa wakati mwingine alitakiwa kuhakikisha kuwa idadi sawa ya wavulana na wasichana wanajitokeza kwenye majaribio.

Shughuli muhimu: Kuchunguza sumaku-umeme

Kusanya darasa lako likuzunguke na wachangie mawazo juu ya dhana ya ‘sumaku-umeme’. (Angalia Nyenzo Muhimu: Kutumia ramani ya mawazo na kuchangia mawazo ili kuchunguza dhana .) Wameona wapi sumaku zikitumika? Sumaku ni vitu gani? Tunaweza kutengeneza sumaku kutokana na umeme? Hii inaitwa sumaku-umeme. Andika mawazo yao ubaoni au kwenye karatasi kubwa ukutani.

Liweke darasa lako katika makundi madogo ya wanafunzi kati ya wane mpaka sita. Kwa kila kundi wape: pini ya chuma, betri ya tochi inayofanya kazi 1.5V; pini ndogo au vibanio vya karatasi na sm 50 za waya mwembamba wa shaba.

Yaambie makundi kuwa unayaandalia tatizo. Inabidi watumie vifaa watengeneze sumaku-umeme itakayonasa pini nyingi kadri iwezekanavyo. (Angalia Nyenzo Muhimu : Kutumia uchunguzi darasani .)

Wahimize wanafunzi wachunguze jinsi ya kutengeneza sumaku-umeme kwa kutumia kifaa.

Watakapokuwa wametatua tatizo, waambie wachore mchoro kuonyesha njia suluhisho yao.

Nyenzo-rejea ya 1: Kuangalia balbu ya tochi kwa makini