Somo la 2

Kuchunguza sura za mazingira ni hatua ya kwanza katika utengenezaji wa ramani. Ili kuwasaidia wanafunzi wako waelewe ramani, unahitaji kuwabainishia dhana ya alama.

Uchunguzi kifani 2 unaonesha jinsi mwalimu mmoja anavyotumia mchezo ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kuhusu alama. Kwa kupangilia na kubuni mchezo unaohusu mada inayopendwa na wanafunzi, mwalimu huyu amefanya kuwe na uwezekano mkubwa zaidi wa wanafunzi kuja kushiriki katika zoezi hili, na kwa hiyo, kujifunza zaidi. Utumiaji wa mchezo utawahusisha wanafunzi wako katka ujifunzaji hai; itakuwa burudani kwao na itawasaidia kukumbuka mengi zaidi. Soma Uchunguzi Kifani 2 bkabla ya kupanga na kujaribu Shughuli 2.

Uchunguzi kifani ya 2: Alama ya kusaka kitu cha thamani

Bi. Jane Ndekule, mwalimu wa wanafunzi wa Darasa la 5 katika Mkoa wa Ruvuma, alitaka kujenga welewa wa wanafunzi kuhusu uelekeo na mazingira ya mahali hapo kwa kubainisha dhana ya utumiaji wa alama kuwakilisha sura za mandhari. Aliamua kufanya mchezo wa kusaka kitu cha thamani.

Kabla ya somo, alichunguza sura sita za mandhari ya shule, akijumuisha mageti, mti mkubwa na ofisi ya Mwalimu Mkuu. Alitafuta vipande sita vya karatasi ngumu na kuchora alama moja kwenye kila karatasi kuwakilisha sura moja ya kitu (mfano, meza ya ofisini kwa mwalimu mkuu). Halafu aliweka namba kwenye karatasi na kuongeza mielekeo kuelekea kwenye alama inayofuata katika kila karatasi. Aliweka vipande hivyo vya karatasi katika sehemu zake mahsusi.

Darasani, wanafunzi waligawanywa katika ‘vyama vya kusaka’ na kupewa vidokezo vyao vya awali. Walitakiwa kwenda nje ya darasa, na kugeukia upande wa mashariki –mwalimu aliwasaidia kwa kuwaambia maelekezo haya ili waanze. Walipokuta karatasi katika sura ya kitu, hii iliwaongoza kuendelea kwenye mwelekeo mwingine, na kutafuta alama nyingine, na kadhalika.

Wanafunzi waliona mchezo huu unasisimua sana. Walishirikishwa kikamilifu katika kutafakari maana za alama na kuelekea kwenye upande sahihi. Bi. Ndekule aliyafuatilia makundi na alikuwa tayari kusaidia kundi lolote lililokuwa likihangaika kutambua maana za alama au kutafuta upande upi wa kufuata.

Kila mmoja aliifikia karatasi ya mwisho. Bi. Ndekule alifurahi kwa sababu alijua wamemudu kutafsiri alama zote na wameelewa vema uelekeo.

Shughuli ya 2: Utumiaji wa alama

Anza somo lako kwa maelezo mafupi kuhusu matumizi na umuhimu wa alama za ramani. Waambie wanafunzi wakupe mifano ya alama maarufu ambazo wanazifahamu zinazotumika miongoni mwao (mfano barabara) na tumia majibu yao kuunda orodha ya alama mahsusi. (Angalia Nyenzo rejea 1: Alama za ramani kwa mifano zaidi.) Unaweza kuunda orodha kwa muda wa hadi wiki moja na kisha kufanya maonesho kwa darasa zima.

Waulize wanafunzi watafakari kuhusu kwa nini alama zitumike kuliko maneno. Uulizaji wa aina hii utawasaidia kufikiri kuhusu thamani na umuhimu wa alama. (Angalia Nyenzo rejea Muhimu: Kutumia uulizaji katika kukuza tafakuri .)

Sasa mwambie kila mwanafunzi afikirie sura tatu za mandhari anazoziona anapokuwa njiani kwenda shuleni (angalia Shughuli 1) na kisha achore alama kwa kila moja. Baada ya dakika chache, waambie wanafunzi wabadilishane alama zao na majirani. Je, majirani wanaweza kukisia alama zina maana gani?

Waambie baadhi ya wanafunzi kuja na kuchora alama zao ubaoni. Je, wanafunzi wengine wanaweza kutambua zinamaanisha nini?

Maliza somo kwa kuona kama wanafunzi wanaweza kuamua kuhusu kitu gani kinafanya alama iwe nzuri.

Orodhesha sababu zao ubaoni.