Somo la 3

Ukuzaji wa maarifa na welewa wa alama maarufu ambazo hutumika kwenye ramani ulimwenguni kote utawasaidia wanafunzi wako kutalii sura za mandhari ya sehemu yoyote duniani. Vilevile, ukuzaji huo utawasaidia kuelewa jinsi ramani zinavyochorwa na thamani yake katika maisha ya kila siku, hususan kwa kadri wanavyokua na kusafiri katika maeneo mapya.

Hata hivyo, ni muhimu kutumia mbinu za kufanyia kazi ambazo zitawashirikisha wanafunzi kikamilifu katika kuyatalii maeneo yanayowazunguka na kutafakari kwa kina kuhusu tatizo wanalojaribu kulitatua. Utumiaji wa nyenzo na wataalamu wa mahali hapo unawasaidia wanafunzi kuelewa zaidi kwani mazingira wanamojifunza yanafahamika kwao. Inawezekana ukamtafuta mtu anayefahamu masuala ya ramani za mahali hapo kuja na kuzungumza na wanafunzi kuhusu jinsi ramani za mahali pao zilivyochorwa na kufafanua maana za alama ambazo zinaonesha sura za mandhari ya mahali hapo. 

Uchunguzi Kifani 3 unaonesha namna mbalimbali ambazo mwalimu mmoja alifanya kazi na wanafunzi wake ya kuelewa ramani za mahali hapo. Soma sehemu hii kabla ya kuanza Shughuli ya Msingi .

Uchunguzi kifani ya 3: Uchanganuzi wa ramani ya eneo la mjini la mahali hapo

Bwana Juma ni mwalimu wa shule ya msingi ya mjini katika Mkoa wa Tanga, Mashariki mwa Tanzania. Alitaka wanafunzi wake waweze kusoma ramani na kutambua sura za mandhari za sehemu yoyote.

Bwana Juma aliamua kutumia ramani halisi ya jiji, na kwa hiyo, wiki mbili kabla ya kupanga kufanya kazi hiyo alitembelea halmashauri ya mipango ya jiji ili kupata ramani mbalimbali za mahali hapo. Kwa kufuatisha toka kwenye ramani hizo, alichora kwenye karatasi ya kufanyia kazi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wake. Kwa vile kazi hii ingehitaji alama, alichora pia chati ya alama ambayo alipanga kwenda kuionesha darasani.

Kwa kuwa halmashauri ya mipango ya jiji waliweza kumpa picha au ramani tano tu za mandhari ya nchi, aligawa darasa lake katika makundi matano. Bwana Juma aliwaonesha wanafunzi wake chati ambayo inabainisha alama na alitoa ramani na moja kati ya karatasi zake za kufanyia kazi kwa kila kundi. Alionesha barabara kadhaa, bustani, hospitali, baadhi ya hoteli na kituo cha mafuta, vyote hivi, makundi yalitakiwa kuvitafuta kwenye ramani.

Halafu, aliwaambia wanafunzi wakadirie kipimo. Alifafanua kwamba vipimo vya ramani hulinganisha ukubwa wa ramani na ukubwa halisi wa eneo. Bwana Juma aliwaonesha wanafunzi wake jinsi ya kusoma taarifa zilizooneshwa kwenye maelezo ya vipimo na kielelezo cha vipimo.

Wanafunzi walipomaliza kuchanganua ramani na kukamilisha kujaza karatasi za kufanyia kazi, walibadilishana karatasi hizo na makundi mengine, na kuangalia kama wamepata majibu yaleyale. Mahali ambako hakukuwa na kufanana, Bwana Juma aliwaambia wanakikundi washauriane na kukubaliana kuhusu jibu.

Mwishoni mwa somo, alipitia alama zote pamoja na darasa zima. Mahali ambako wanafunzi walipata majibu tofauti, walijadili sababu za majibu hayo na kukubaliana kuhusu jibu la mwisho.

Nyenzo rejea 2: Ramani Kifani na Nyenzo rejea 3: Maswali kuhusu ramani toa mifano ya aina za nyenzo rejea ambazo zinaweza kutumika.

Shughuli muhimu: Kutengeneza picha kubwa ya mahali hapo

Liambie darasa kwamba utachora ramani kubwa pamoja nao, na njia tofauti tofauti wanazopita wakati wa kuja shuleni na sura za mandhari yanayozunguka shule.

Gawa darasa lako katika makundi manne, kulingana na uelekeo wanaofuata kutoka majumbani hadi shuleni (Ksz, Ksn, Ms na Mgh)

Liambie kila kundi liorodheshe sura za mandhari ambayo huyaona wanapokuja shuleni (Angalia Shughuli 1).

Weka alama kwenye nafasi nne ardhini –au katika kipande kikubwa cha karatasi au kipande cha nguo kisicho na alama yoyote –Ksz, Ksn, Ms na Mgh.

Waambie wanafunzi wajitolee kuwa wa kwanza kuchora sura hizo zilizoko kwenye upande wao katika nafasi walizopewa.

Kisha kila kundi liongezee kwenye kile kilichochorwa na wanafunzi wenzao waliojitolea.

Mara picha kubwa itakapokamilika, jadiliana na wanafunzi jinsi sasa mbele yao walivyo na ramani kubwa ya eneo zima linaloizunguka shule.

Waambie wanafunzi kutoka katika makundi tofauti kuangalia ramani kutoka upande mwingine na kuona kama wanaweza kubainisha alama zilizomo zinamaanisha nini.

Ukiwa na wanafunzi wadogo, unaweza kwanza kujadili alama zitakazotumika na kuzichora ubaoni. Halafu waambie watumie alama hizo kwenye ramani zao.

Mwisho, waambie wanafunzi wachore ramani zao ndogo za shule na mazingira yake, kwa kutumia ramani kubwa kama mfano wa kuwaongoza.

Nyenzo-rejea ya 1: Alama za Ramani