Somo la 1

Ufundi wa jadi wa jamii utakuwa na maana zaidi kwa wanafunzi wako kama utawahusisha katika kufanya baadhi ya hizi kazi za ufundi. Sehemu hii inaibua kile wanafunzi wako wanachoelewa juu ya ufundi wa mahali hapo pamoja na watu wanaotengeneza zana hizo katika mazingira ya vitendo. Inakupa wewe nafasi ya kujenga ujuzi wa kuuliza maswali, na inakuonyesha njia ya kuwasaidia wanafunzi wako kuuliza maswali yao wenyewe.

Uchoraji ni njia moja ambayo jamii nyingi zinaweza kurekodi matukuio ambayo yametokea. Vilevile ni njia ambayo hutumia kufikiria sana, hivyo ni nzuri kwa wanafunzi kuelezea mawazo na hisia zao.

Uchunguzi Kifani 1 unaelezea jinsi mwalimu mmoja alivyowahimiza wanafunzi wake kupaka rangi na kuchora. Katika Shughuli 1, unatumia majadiliano ya vikundi vidogo kuibua nini wanafunzi wanaelewa juu ya ufundi wa mahali hapo, matumizi yake na jinsi zinavyotengezwa. Hii inaweza kuwa ni hatua ya mwanzo ya kufanya utafiti zaidi juu ya ufundi katika shughuli itakayofuata.

Uchunguzi kifani ya 1: Kuangalia michoro

Bi Moyosola kutoka kusini-magharibi mwa Nigeria alikuwa anafundisha upakaji rangi. Alitaka kulihimiza darasa lake kupaka rangi na kuchora. Aliamua kuanza kwa kuwaambia wanafunzi wake watazame baadhi ya picha zilizochorwa na wachoraji wa kisasa wa Nigeria kutoka katika eneo lao.

Alikuwa na nakala moja kwa kila picha aliyoaibandika ubaoni. Aliwaambia wanafunzi watazame hizo picha na waseme ni kitu gani walikipenda na kipi hawakukipenda. Aliwauliza kama mmoja kati yao aliwahi kupaka rangi au kuchora, na kama ndivyo, alipaka rangi au kuchora nini na lini. Wengi hawakuweza kuwa na karatasi na kalamu, lakini walisema huchora picha mchangani nje ya nyumba wanazoishi. Walisikitika kwa kuwa picha hizi hazikuweza kudumu.

Bi Moyosola aliwaambia wanafunzi wake wafikirie kitu ambacho wangependa kupaka rangi au kuchora. Aliwapa karatasi na penseli, na kuruhusu vipindi viwili vya sanaa wavitumie kwa kuchora na kupaka rangi. Wengi walichora picha zao wenyewe na wengine walifuatishia zile picha za kisasa za Nigeria.

Bi Moyosola alizionyesha hizi picha ili kila mmoja achangie mawazo.

Shughuli ya 1: Kuuliza maswali juu ya ufundi wa mahali hapo

Kusanya baadhi ya mifano ya ufundi wa mahali hapo. Ungeweza kutumia mifano hiyo hiyo kwa makundi yako yote, au mfano tofauti kwa kila kundi.

Pangilia darsa lako katika makundi madogo ya wanafunzi wanne/watano.

Waambie kila kundi wajadili kitu wanachofahamu katika ufundi wa aina moja. Waambie waanze kwa kujibu maswali yafuatayo (yaandike maswali haya ubaoni).

Ni kitu gani? Kinatumikaje?

Kilitumikaje siku za nyuma? Kinatengenezwaje?

Wape wanafunzi dakika 10–15 kujadili haya maswali na kufikiria swali moja zaidi la kuuliza kuhusu ufundi. Ungeweza kuwaambia wanafunzi wakubwa wachore na kuandika mawazo yao kwenye mchoro.

Halafu, waulize baadhi ya majibu yao. Unaweza kukuta kuwa hawakujibu maswali yote, hivyo waeleze kuwa wataenda kufanya utafiti ili kukusanya habari zaidi katika Shughuli 2.

Sehemu ya 2: Kuandaa Shughuli za Sanaa kwa Vitendo