Somo la 2: Kufanya kazi katika vikundi ili kutunga ushairi wa wasifu yaani utenzi

Utenzi na uimbaji ni uzoefu muhimu wa Kiafrika, wa kale na wa sasa. Majina ya Kiafrika huambatanisha nafsi yako na wapi utokako. Huwataarifu watu kuhusu uzoefu wako, furaha na mapambano yako, na jinsi ulivyo, ili watu wakutambuwe. Watu hutunga nyimbo zao wenyewe za sifa. Watunzi wa mashairi huburudisha kwa kuonyeshwa kwenye sherehe, ada za asili na sikukuu ili kutoa wasifu wa mtu au kikundi. Nyimbo za sifa na utenzi zimekuwa sanaa staarabu, ambayo hufanywa na tamaduni nyingi kwa kupitia muziki, dansi na uimbaji.

Utawasaidia wanafunzi kufanya utafiti na kubuni tenzi zao wenyewe au nyimbo, ukilenga mawasiliano ya kujitambulisha na urithi wa ukoo. Hii itawasaidia wanafunzi wako kupata uhusiano baina yao wenyewe na uzoefu wa muziki.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia mashairi ya kusifu kujenga uelewa wa muziki

Ndugu Mtui ni mwalimu wa muziki, sanaa na utamaduni ambaye amekulia Kilimanjaro. Anafundisha shule ya msingi iliyoko mjini, ambako wanafunzi wake wanawakilisha, tamaduni, dini na lugha mbalimbali. Anapiga wimbo wa kichaga wa zamani kwenye gitaa lake anapokuwa anafikiria juu ya somo lake la muziki la mwezi ujao. Atajengaje dhamira ya utambulisho kwa kutumia muziki? Anapoimba, muziki unamrudisha nyuma wakati wa utoto wake, nyumba yao, wazazi na mababu na mabibi. Anakumbuka alivyokuwa anasikia nyimbo za kutaja majina na kujisifu kama mtoto. Anaukumbuka wimbo wake wa majigambo unaoelezea kuzaliwa kwake na ukoo wake. Kumbukumbu zake zinatengeneza mwanzo wa wazo lake kwa darasa lake.

Ndugu Mtui anakusanya baadhi ya mashairi ya kusifu na nyimbo na kuvitungia maswali. Anasikiliza muundo wa nyimbo za kuita na kujibu na anaziunganisha na mchezo wa kujigamba uliozoeleka ambao wanafunzi wake wanaucheza kiwanjani. Anapanga kufundisha somo juu ya mashairi ya kusifu kwa kuanzia kwenye nyimbo zilizozoeleka. Halafu anawahimiza wanafunzi wake kutengeneza na kuimba nyimbo na mashairi ya kusifu rafiki zao. Angalia Nyenzo rejea 4: Kuimba kwa kusifu kwa habari zaidi za kina.

Shughuli ya 2: Nyimbo na mashairi ya kusifu

Kabla ya shughuli hii, tazama Nyenzo rejea 5: Nyimbo za kusifu za mwanafunzi.

Imba wimbo wa kusifu unaofahamu darasani kwako au mwambie mwanafunzi aimbe darasani. Waeleze wanafunzi namna muundo wa wimbo unavyofanya kazi na washirikishe kutoa majibu.

Imba wimbo tena wakati wanafunzi wakitunza mdundo kwa kupiga makofi, kugonga madawati au kutumia zana.

Ongea nao juu ya wazo la nyimbo za kusifu, nani wanaziimba na kwa nini

Imba nao shairi la kusifu, ukifuatilia mapigo ya maneno na kuwasilisha hisia za shairi kwa sauti yako. Ongeza sauti za vifaa zitakazoongeza hisia za shairi kama inawezezekana.

Halafu, ligawe darasa katika makundi ya wanafunzi sita. Waambie kila kundi wafanye kazi watatu watatu na waandike shairi lao la kusifu. Kila wanafunzi watatu waimbe shairi lao kwa wenzao watatu kisha waeleze maana na hisia zilizopo kwenye shairi. Kwa pamoja, kundi zima linachagua kiitikio na kujaribu kuimba mashairi yao mawili. Wanaweza kuongeza sauti nyingine kama wanapenda.

Baada ya siku chache zijazo, waambie kila kundi liimbe shairi lake la kusifu kwa darasa zima.