Somo la 2

Bruno Bettelheim (1976), mtaalamu wa saikolojia ya watoto, anaamini kwamba kama watoto watakutana na ‘maajabu’ katika hadithi, kwa hakika watapenda kujifunza kusoma. Anatoa hoja kuwa kama watoto anaamini hasa kwamba kuweza kusoma kutafungua dunia yenye uzoevu na welewa wa ajabu, watafanya jitihada kubwa kujifunza kusoma na wataendelea kusoma.

Kusoma pamoja hadithi za kufurahisha na wanafunzi ni njia moja ya mwalimu ya kufanya usomaji uwe ni jambo lenye mvuto. Kitu kingine ni kuchochea udadisi na ubunifu kwa kuwahimiza watafute miisho mbadala ya hadithi (na wakati mwingine mianzo) na kushirikishana mianzo na miisho hii na wanadarasa wenzao. Uchunguzi kifani 2 na Shughuli 2 vinaeleza jinsi unavyoweza kuwasaidia wanafunzi wako wawe watunzi wa hadithi kwa ajili ya wenzao.

Uchunguzi kifani ya 2: Usomaji wa hadithi; uandishi wa miisho mipya ya hadithi

Bibi Miriam Pharouk hufundisha Kiingereza Darasa la 6 katika shule ya Tanga. Siku moja aliwaambia wanafunzi wake wafikirie hadithi ambazo wameshasoma naye na wamwambie ni mwisho upi wa hadithi waliupenda sana na upi waliuona si mzuri au haukuwaridhisha. Aligundua kuwa walikuwa na hadithi tofautitofauti walizozipenda. Hata hivyo, kulikuwa na hadithi moja ambayo wanafunzi wengi hawakuipenda kwa sababu hawakujua kilichotokea kwa wahusika watatu ambao ‘walitoweka’ kwenye hadithi. Miriam aliwaambia wapendekeze nini kinaweza kuwa kiliwatokea wahusika hawa na aliandika mawazo yao ubaoni. Baadaye aliwaambia

wanafunzi wamchague mhusika mmoja kati ya hawa watatu na waandike sehemu ya mwisho ya mhusika huyu katika hadithi hii. Aliwahimiza wanafunzi kutumia mawazo yao wenyewe, na pia yale yaliyoandikwa ubaoni, na waingize michoro kwenye uandishi wao. Kisha alisoma tena ile hadithi ili kuwakumbusha mandhari, wahusika na matukio makuu.

Ingawa Miriam aliwaambia wanafunzi kila mtu aandike mwenyewe, pia aliwahimiza kusaidiana kwa mawazo, msamiati na muenelezo wa maneno. Alizunguka darasani huku wanafunzi wakiwa wanaandika na kuchora, akitoa msaada palipohitajika. Alifarijika alipogundua kuwa wengi wa wanafunzi wake wanapenda kwa dhati wazo la kuwa watunzi na la kuiandikia hadhira halisi (wanadarasa wenzao). Aling’amua kuwa walikuwa waangalifu sana katika kufanya kazi yao kwa sababu wanadarasa wenzao wangesoma kazi zao.

Katika somo lililofuata, wakati wanafunzi wanasoma mwisho wa hadithi ya mwenzao, mwalimu aligundua kuwa wengi wa ‘wasomaji wake waliokuwa wanasitasita’ walikuwa makini kusoma kile ambacho wanadarasa wenzao walikuwa wamekiandika na kuona kile walichokuwa wamekichora.

Shughuli ya 2: Uandishi wa mianzo na miisho mipya ya hadithi

Andika kwenye ubao wako hadithi fupi katika Nyenzo-rejea 3: Hadithi . Futa kichwa cha hadithi na sentensi mbili za mwisho.

Soma hiyo hadithi wewe na wanafunzi wako. Jadilini maneno yoyote magumu.

Waambie wajibu maswali kama yaliyoko kwenye Nyenzo-rejea 3.

Panga darasa katika vikundi vya wannewanne –wawili waandike mwanzo wa hiyo hadithi na wawili waandike mwisho wa hiyo hadithi. Wanafunzi wawiliwawili wachore mchoro wa kufafanua sehemu yao ya hadithi. (Zoezi hili linaweza kuchukua zaidi ya kipindi kimoja.)

Kiambie kila kikundi kisome hadithi yao yote na kuonesha michoro yao kwa darasa zima. Jadilianeni na wanafunzi kitu wanachokipenda katika hadithi za wenzao.

Mwishoni, wasomee wanafunzi wote kichwa cha hadithi ya awali na zile sentensi mbili za mwisho. (Huenda wakashangaa kwamba inahusu soka!)

Tafuta hadithi nyingine ili kurudia zoezi hili.Shughuli hii ilifanikiwa vizuri kwa kiasi gani? Wanafunzi walizipokeaje hadithi za wenzao?