Nyenzo-rejea ya 2: Maswali ya kutumia wakati wa usomaji wa kitabu – usomaji wa kwanza, wa pili na wa tatu

Nyenzo-rejea ya mwalimu kwa ajili kupanga au kurekebisha ili kutumia na wanafunzi

Hapa pana maswali machache unayoweza kuuliza kabla ya kusoma hadithi na wanafunzi na pia mifano ya maswali ya kuuliza baada ya usomaji kumalizika. Aidha pana maswali ya kuwauliza wanafunzi baada ya kuwa wamesoma kitabu mara ya pili au zaidi.

KIPINDI CHA KWANZA CHA USOMAJI

Kabla ya usomaji

  1. Je, jalada linakufanya upende kusoma hiki kitabu? Kwa nini? au kwa nini hapana? Unafikiri jalada linakuambia kitabu kinahusu nini? Kwa vipi?
  2. Niambie kuhusu kile unachokiona katika ukurasa wa kwanza wa hadithi.

Wakati wa kusoma

Uliza maswali kuhusu jinsi hadithi ilivyoundwa na jinsi maneno na picha yanavyochangia katika muundo wa hadithi hii.

Baada ya kusoma

  1. Umependa nini na hukupenda nini kuhusu hiki kitabu?
  2. Je, kuna kitu kilichokushangaza kuhusiana na kitabu hiki? 
  3. Je, kuna ruwaza zozote ambazo umezigundua?
  4. Picha gani unayoipenda zaidi? Unaweza kuniambia unaona nini katika picha hii?
  5. Unafikiri jalada linafaa kuhusiana na kile kilichotokea katika hadithi hii?
  6. Je, maneno au picha zinasisimua? Je maneno yanaeleza hadithi kwa njia mbalimbali? Je, maneno yangekuwa mazuri bila picha? Je, picha zingeendelea kuwa nzuri bila maneno?
  7. Je, hadithi imesimuliwa kwa picha au vyote viwili? Je, hali hii ndivyo ilivyo kwa kitabu kizima?

KIPINDI CHA PILI NA CHA TATU

(Angalizo: Hivi ni lazima viwe vimepishana kwa wiki kadhaa )

Kabla ya kusoma

  1. Umeshafikiri kuhusu kile kitabu tangu tulipokisoma kwa mara ya mwisho?
  2. Ungependa kukisoma tena?
  3. Nisimulie unachokumbuka zaidi kuhusiana na kile kitabu.

Wakati wa kusoma

Uliza tena maswali kuhusu muundo wa hadithi na jinsi maneno na picha vinavyochangia katika muundo huu.

Baada ya Kusoma

  1. Umegundua kitu chochote wakati huu ambacho hukukigundua kabla? 
  2. Unajisikiaje kuhusiana na hadithi hii baada ya kuisoma tena?
  3. Unapofikiria kitabu hiki sasa, ni kitu gani muhimu kuliko vyote kwako kuhusiana na kitabu?

Baada ya kuwa umekisoma kitabu hiki zaidi ya mara moja, je, ungependekeza wanafunzi wengine pia wakisome zaidi ya mara moja na mwalimu wao?

Imechukuliwa kutoka: Swain, C. Gazeti Msingi la Kiingereza (The Primary English Magazine)

Nyenzo-rejea ya 1: Kitu ambacho waandishi na wasomaji wafanisi wanatakiwa kukijua

Nyenzo-rejea 3: Hadithi