Nyenzo-rejea ya 4: Sheria na taratibu za kuendesha mdahalo

Usuli/taarifa ya mwanzo/uelewa wa mwalimu

Mdahalo ni mashindano, au, labda, ni kama mchezo ambapo wazungumzaji wawili au zaidi hutoa hoja zao kwa nia ya kushawishiana...

Kwa nini tunafanya midahalo?

Kwa kujitayarisha na kushiriki katika midahalo wanafunzi wanajifunza kutumia taarifa kuunga mkono hoja zao. Wanajifunza namna ya kuwasilisha mawazo yao kwa uwazi na kwa ushawishi mkubwa.

Kwa kushiriki katika midahalo, wanajifunza kuelewa mawazo ambayo ni tofauti na yao kwa sababu, wakati wa kufanya mdahalo, wanaweza kujadiliana kwa kutoa hoja kwa jambo ambalo hawakubaliani nalo kikamilifu, na wanapaswa kuelewa mawazo ya wenzao wa timu ya wasiokubali hoja zao.

Matayarisho

Wafanya midahalo wazuri wanajitayarisha vizuri. Mdahalo unaofanya darasani unaweza usiwe rasmi, lakini unaweza kuwajenga wanafunzi katika hali inayowafanya wanafunzi wako wafanye mdahalo rasmi katika mashindano.

Kabla ya kuandaa hotuba, wafanya midahalo wanakusanya taarifa nyingi kwa kadri iwezekanavyo, kutoka katika maktaba, magazetini, na kwa kujadiliana na watu.

Wanafikiria hoja zote zinazounga mkono mada yao, na zile zinazopinga hoja yao. Kwa maana nyingine ni kuwa, wanaelewa hoja za wapinzani wao pamoja na hoja zao. Wanajitayarisha kwa maswali yoyote wanayoweza kuulizwa na wapinzani wao, na changamoto zozote zinazoweza kutolewa.

Wafanya midahalo wazuri wanatayarisha hoja zao katika muundo mzuri wa ushawishi. Wanawasikiliza watu wengine wanaofanya mdahalo, ili wajifunze ufundi na stadi za kufanya mdahalo. Wanajiunga na vyama vya kufanya midahalo, na kufanya midahalo mara kwa mara.

Mchakato

Kuna timu mbili, kila timu ina wazungumzaji wawili au watatu. Timu moja (chanya) inaafiki hoja, na timu nyingine (hasi) inapinga hoja.

Kuna mwenyekiti, ambaye anaendesha utaratibu.

Hotuba na muda wa hotuba hizo unagawanywa sawasawa kwa timu zote mbili.

Kila mzungumzaji anatoa hotuba upande wake umeandaa kuunga mkono hoja zao.Pande zinazungumza kwa zamu, wakianza na anayependekeza hoja (chanya, hasi, chanya, hasi). Kila mzungumzaji ana muda maalum wa kuzungumza (k.m. dakika tatu au tano)

Baadaye mdahalo unaweza kufunguliwa kwa washiriki wengine, kwa wasemaji kusimama na kutoa hoja zao za kuunga mkono au kupinga mada ya mdahalo. Kila mzungumzaji kutoka upande wa wasikilizaji anapewa muda maalum wa kuzungumza ( k.m. dakika moja au dakika tatu).

Kila timu inaweza pia kuzungumza kwa kujibu hoja za wapinzani wao, baada ya kila timu kupewa muda kidogo wa mashauriano. Hii ina maana kuwa wana nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wapinzani wao. Kila timu inaweza kupewa nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wenzao mara moja au zaidi. Nafasi ya kwanza ya kupinga hoja wanapewa wale wanaopinga mjadala na nafasi ya mwisho inatolewa kwa wanaunga mkono mjadala.

Kanuni muhimu

Timu inayounga mkono mjadala haitakiwa kubadili hoja zao. Aidha ile inayopinga mjadala nayo pia hairuhusiwi kubadili hoja zao. Wanapaswa kupinga kabisa mjadala licha ya maoni yao binafsi).

Ikiwa mzungumzaji anatoa tamko, wanatakiwa kutoa ushahidi au sababu za kuunga mkono tamko hilo.

Taarifa zinazotolewa katika mdahalo lazima ziwe sahihi.

Wazungumzaji hawaruhusiwi kuleta hoja mpya wakati wa kujibu/kupinga hoja za wenzao.

Hoja ya utaratibu na hoja ya taarifa

Yeyote anayehusika na mdahalo anaweza kuingilia kati wakati msemaji akizungumza kwa kunyoosha mikono na kusema kuwa ‘anataka kutoa hoja’. (Hii ni ‘hoja ya utaratibu’). Hii ina maana kuwa anataka kueleza kuwa moja ya kanuni za mdahalo imevunjwa (k.m. mzungumzaji amezidisha muda wake wa maongezi, au hana ushahidi wa kuthibitisha hoja zake).

Wana-mdahalo wanaweza pia kunyoosha mikono yao wakitaka kutoa ‘hoja ya taarifa’ (swali au taarifa za ziada wanazoweza kutoa). Msemaji anaweza kuamua kumruhusu mwanachama kuzungumza, lakini halazimiki.

Uamuzi

Timu inayoshinda katika mdahalo inaamuliwa na jaji au majaji kwa kutegemea ubora wa mjadala.

Aidha inaweza pia kuamuliwa kwa kupigiwa kura.

Vyanzo vya asili: Trivium Pursuit, Website.

Nyenzo-rejea ya 3: Muundo wa hotuba za mdahalo

Nyenzo-rejea ya 5: Mfano wa barua- iliyoandikwa na darasa la mwalimu Mariam