Sehemu ya 5: Njia za kuwa msomaji na mwandishi makinifu

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuendeleza stadi za umakinifu wa kufikiri wa mwanafunzi wakati wa usomaji na uandishi

Maneno muhimu: usomaji makinifu; uandishi makinifu; maoni/mitazamo; uulizaji (maswali); tathmini     

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • Kutumia maswali kuwasaidia wanafunzi wako kuwa wasomaji makinifu wa matini mbalimbali;
  • Kuwasaidia wanafunzi wako kubuni na kuandika hadithi, matini na barua za taarifa ambazo zinatokana na matini walizosoma kwa umakinifu na hivyo kukuza stadi za kufikiri;
  • Kutumia njia mbalimbali za kutathmini ujifunzaji.

Utangulizi

Waandishi wote - wawe wa hotuba za kisiasa, matangazo ya biashara, makala za magazeti, vitabu vya shule au vyuo (vikuu), hadithi za watoto, au aina nyingine yoyote ya matini - huandika kwa kuzingatia mtazamo fulani na kwa nia fulani. Ni muhimu kuweza kubainisha mtazamo wa mwandishi na kuamua kama unakubaliana nao au hukubaliani nao.

Kufikiria uzoevu wako na imani zako na uliyojifunza katika masomo yako kunaweza kukusaidia kuuliza maswali makinifu kwa kila kitu unachosoma. Itakusaidia kama mwalimu kukumbuka kuwa wanafunzi wako wanaweza kuwa na mawazo ambayo ni halali kama yako. Ukiwafundisha wanafunzi wako kuuliza maswali kuhusu wanachosoma na kufikiria misimamo mbalimbali, utakuwa unawasaidia kuwa raia wanaofahamu kwa makini mambo mengi.

Unaweza kuanza jambo hili hata kama wanafunzi ni wadogo. Ukiwa unawasomea hadithi, wahimize wajadiliane yapi wanayakubali na yapi hawayakubali.

Shughuli tatu katika sehemu hii ni mifano ya njia za kuwasaidia wanafunzi wako kuwa wasomaji na waandishi makini wa matini.

Nyenzo-rejea ya 6: Vifungu vya utoaji hoja