Somo la 2

Aina zote za michezo zinaweza kutumika kwa kujifunzia na unahitaji kufikiri kiubunifu jinsi ya kuitumia michezo darasani (angalia Shughuli 2). Inasaidia kama unaweza kushirikiana na wenzako pamoja na rafiki zako, na pia kushirikiana na wanafunzi wako, katika kubuni mawazo mapya ambayo yanaweza kufanya ujifunzaji darasani kwako uwe wa kufurahisha na wenye mafanikio.

Katika sehemu hii, wewe na darasa lako panueni utafiti wenu kwa kuwauliza wanajumuiya kuhusu michezo waliyokuwa wanaicheza walipokuwa wadogo.

Uchunguzi kifani ya 2: Michezo na mikarara/viitikio katika kadi za kusoma

Kuna ongezeko la kupenda lugha nyingi za nyongeza katika mitalaa kote Afrika. Hii ina maana kuna ujifunzaji wa awali unaotumia lugha mama, na lugha nyingine za nyongeza (bila kuchukua nafasi ya ile lugha mama). Mtalaa unalenga kuingiza lugha zote ambazo watoto wanazijua wakati wa masomo yao.

Bwana Maleke mkoani Lindi hutumia shughuli ifuatayo, ambayo hujumuisha lugha nyingi za nyongeza, pamoja na wanafunzi wake wa darasa la 5. Humpatia kila mwanafunzi kipande cha kadi. Wanafunzi huchora picha katika upande mmoja wa kadi. Kwa upande mwingine, huandika nyimbo, michezo, mikarara/viitikio au mashairi, ambayo wanayapata nyumbani.

Kila siku, wana kipindi cha kusoma ambapo wanafunzi wanasoma (au wanaimba!) kile kilichoandikwa kwenye zile kadi. Wakati mwingine, msomaji bora husoma kadi na msomaji anayesoma polepole zaidi. Wakati mwingine, mzungumzaji wa lugha moja, humsaidia mwanafunzi mwingine kusoma lugha yake na kuingiza sauti. Wakati mwingine, wanaigiza hayo mashairi au wanacheza michezo hiyo. Bwana Maleke amegundua jinsi darasa lake linavyokuwa na furaha na jinsi wanafunzi wanavyoshirikiana vizuri katika mazungumzo na wanavyochanganyika vizuri zaidi tangu waanze kufanya hivi.

Shughuli ya 2: Michezo na nyimbo kutoka kwa wanajumuiya ambao ni watu wazima

Waambie wanafunzi wako wamwombe mtu mzima (mzazi, babu/bibi, jirani n.k.) awafundishe mchezo, wimbo au mkarara ambao walikuwa wakiufurahia wakati wa utotoni. Wanatakiwa wajue kanuni za maneno na nyenzo zozote ambazo zinahitajika.

Siku inayofuata, orodhesha michezo na nyimbo ambazo wanafunzi wamezileta toka nyumbani.

Waweke pamoja wanafunzi wanaojifunza mchezo au wimbo wa aina moja. Waambie wajiandae kufundisha darasa mchezo au wimbo huo.

Waambie waandike huo wimbo au huo mkarara au wacheze mchezo wa kwenye kadi.

Darasa litakapomaliza kujifunza mchezo au wimbo huo, jadilianeni kitu ambacho wanaweza kujifunza kutokana na mchezo au wimbo huo. Andika tini kama ulivyofanya hapo awali.

Kwa masomo yatakayofuata, wahamasishe wanafunzi wasome magazeti ili kutafuta nyimbo, michezo, vitendawili na mizaha kama msingi wa kuandika vitu vyo wenyewe.