Somo la 1

Kama wanafunzi wanasikiliza na kusoma mashairi na hadithi wanazozifurahia, ni rahisi sana wakapenda kuendeleza stadi zao za usomaji na uandishi kwa kutumia lugha zao za asili au lugha wanayoitumia darasani.

Ili kuwa waandishi wenye mafanikio, wanafunzi wanahitaji ‘zana’ mbalimbali. Kwanza, wanahitaji mada ya kuandikia. Katika Shughuli ya 1, utatumia mifano ya mashairi ya majina au ya kusifu au hadithi ili kuwapatia wanafunzi mawazo. Kisha utawaongoza katika kuandika rasimu ya kwanza ya shairi la majina au la kusifu au hadithi. Hii ina maana kwamba itabidi kuandika matoleo kadhaa ya rasimu, ambayo yatazidi kuboreshwa, mpaka watakaporidhika kuwa shairi au hadithi zao ni nzuri na wanaweza kutoa toleo la mwisho.

Uchunguzi kifani ya 1: Kusoma na kuandika mashairi ya majina na hadithi katika warsha ya mwalimu

Katika warsha ya siku nne mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini, baadhi ya walimu wa Kiingereza/Kiswahili walisoma mashairi na hadithi kuhusu majina. Katika warsha hii, waandishi walieleza jinsi walivyopata hayo majina yao, kitu walichokipenda au ambacho hawakukipenda kuhusiana na majina yao na maneno ambayo yalihusiana na majina hayo. Kwa kweli walimu walifurahia kile walichokisoma na kuomba iwapo wangeweza kupatiwa nafasi ya kuweza kuandika mashairi au hadithi zinazohusu majina yao wenyewe wakati wa warsha.

Siku ya pili, kila mwalimu alimsomea mwenzake rasimu yake ya kwanza. Walipeana majibu ya kile walichokipenda na kile ambacho walifikiri kinafaa kiboreshwe, kwa mfano kwa kuongeza maelezo na kuchagua msamiati tofauti au alama za uakifishi.

Siku ya nne, wakiwa wameshafanyia kazi rasimu zao siku moja kabla, kila mmoja alikisomea kikundi kizima shairi au hadithi ambayo ilikuwa imekamilika. Kulikuwa na kicheko, kulikuwa na machozi na kulikuwa na makofi mengi.

Walipoambiwa waakisi uzoefu wao, walisema:

  • hakuna mtu aliyekuwa ‘amekwama’ kuhusiana na kitu/mada ya kuandikia;

  • wakati wengi wao waliandika kwa Kiingereza, walifurahia mara kadhaa kutumia maneno au virai vya Lugha ya Kiafrika ili kueleza wazo fulani;

  • walinufaika na matokeo ya rasimu zao za kwanza; walijisifu sana kutokana na toleo la mwisho; walifurahia kusikiliza hadithi/mashairi ya wengine;

  • mengi ya mashairi yalikuwa yanafanana na yale mashairi na zile nyimbo za jadi za kusifu.

Walimu waliamua kuwasomea wanafunzi mashairi na hadithi zao pamoja na mashairi na hadithi nyinginezo za majina katika kuwasaidia ili waweze kuandika kuhusu majina yao.

Shughuli ya 1: Kuandika rasimu ya mashairi au hadithi za majina

Ili kupata mawazo jinsi ya kuandaa shughuli hii, tumia Nyenzo-rejea 1: Kuandaa masomo juu ya mashairi ya majina au ya kusifu na Nyenzo-rejea 2: Mashairi na hadithi za majina au Nyenzo-rejea 3: Mashairi na hadithi za kusifu. Chagua ama mashairi/hadithi za majina au mashairi/hadithi za kusifu.

Waambie wanafunzi wapendekeze shairi/hadithi ya majina au shairi/hadithi ya kusifu itahusu nini.

Waambie wasikilize wakati wewe ukiwa unasoma shairi (ma)/hadithi uliyoandaa kwa sauti.

Waulize maswali kuhusu kile ulichowasomea.

Waambie wanafunzi wajadiliane na wenzao ama kuhusu kile wanachokijua kuhusu jina hili ulilowasomea, au kile wanachokijua kuhusu mtu, mnyama au kitu wanachotaka kukisifia.

Baadaye, waambie baadhi ya wanafunzi watoe ripoti ya mjadala wao darasani.

Waambie wanafunzi waandike rasimu ya kwanza ya shairi au hadithi kuhusu wao wenyewe au wanafamilia au kumsifu mtu, mnyama au kitu watakachokichagua.

Kusanya rasimu ili kutayarisha Shughuli Muhimu.

Je, kuandika mashairi/ hadithi za majina au za kusifu kunawapa wanafunzi mawazo ya kuandika?

Uliridhika na jinsi ulivyoendesha somo? Utafanya marekebisha gani wakati ujao?

Ukiwa na watoto wadogo zaidi, unaweza kuandika mashairi ya majina kwa pamoja, mkishirikishana mawazo na kutumia maneno yaliyozoeleka katika lugha inayotumika darasani.

Sehemu ya 4: Utumizi wa hadithi na ushairi