Somo la 2

Baadhi ya hadithi za kwanza wanazozisikia watoto ni zile ambazo zinahusu uzoefu wa maisha ya familia au wanajumuiya. Hadithi za maisha ya watu mashuhuri (wasifu wao) mara nyingi huchapishwa katika magazeti na hata katika muundo wa vichekesho, hivyo, kama wanazisikia au wanazisoma, wanafunzi wengi watakuwa wana fununu juu ya hadithi kuhusu maisha. Huu ni mwanzo mzuri ili kuamsha hamasa ya kusoma na kuandika.

Darasani, wanafunzi wanahitaji msaada kutoka kwa mwalimu wao na kutoka kwa wenzao wakati wanapojifunza kuzungumza, kusoma na kuandika –hasa kama lugha hii ni ya nyongeza. Uchunguzi Kifani 2 na Shughuli 2 zinaonesha jinsi unavyoweza kuwapatia wanafunzi fursa ya kusoma, kuzungumza, kufanya kazi pamoja katika vikundi vidogo na kuandika rasimu za kwanza za hadithi za maisha ya watu wanaowapenda.

Wanafunzi wanahitaji mifano ili kuwaendeleza kama waandishi. Makala wanazozisoma zinaweza kuwasaidia katika kupangilia uandishi wao na kuwasaidia katika miundo ya sentensi na msamiati. Wanafunzi wadogo watakuhitaji wewe ili ufanye nao kazi, uwaongoze katika uandishi wao na polepole wapanue msamiati wao.

Uchunguzi kifani ya 2: Kutumia mambo yanayowavutia wanafunzi ili kuendeleza stadi za usomaji na uandishi

Bw. Simoni Raphaeli aligundua kuwa, katika uwanja wa mpira, baadhi ya wavulana wa darasa la 6 –ambao hawakuonesha kuvutiwa na usomaji na uandishi wakati wa masomo ya Kiingereza –mara kwa mara walikaa pamoja ili kusoma gazeti la soka, Mwanaspoti. Walimwambia Bw. Simon kuwa wanafurahia kutafuta taarifa zinazohusu maisha ya wachezaji wanaowapenda.

Hali hii ilimpa Simoni wazo. Aliwauliza wanafunzi wa darasa lake kama wameshawahi kusoma magazeti na, kama wameshawahi kuyasoma, walifurahia kusoma kitu gani. Wengi walisema kuwa walijaribu kusoma hadithi kuhusu watu ambao waliwavutia, hata kama hawakuweza kuelewa maneno yote. Simon aliandaa mkusanyiko wa magazeti kwa ajili ya darasa. Kisha aliwauliza wanafunzi kuhusu mambo waliovutiwa nayo na kuwafanya wasome magazeti hayo. Nyota wa michezo ndio waliopendwa zaidi (hasa wachezaji wa soka, pia mpira wa kikapu, mbio na ndondi), wanamuziki, nyota wa filamu na TV, wakifuatiwa na wanamitindo, wanasiasa, viongozi wa jumuiya na wafanyabiashara maarufu.

Simoni aliwapanga wanafunzi kufuatana na yale mambo yaliyowavutia. Kulikuwa na vikundi kadhaa vya nyota wa michezo na wanamuziki! Alikipatia kila kikundi magazeti na kuviambia vikundi vitafute makala/picha kuhusu mtu mmoja aliyewavutia wanakikundi. Kisha, kama kikundi, walisaidiana kuandika sentensi fupi moja au mbili kuhusu maisha ya mtu huyo. Walitumia maneno yao wenyewe na pia msamiati kutoka kwenye makala. Waliandika kichwa cha habari chao wenyewe.

Simoni aliridhika kuona kuwa wanafunzi wengi walishiriki katika usomaji na, wengine wakiandika sana kuliko wengine, wote walishiriki. Kila kikundi kilifurahia kusoma na kukisomea kikundi kingine wasifu wa kikundi.

Shughuli ya 2: Usomaji na uandishi wa hadithi za maisha

Ili kuandaa shughuli hii tumia Nyenzo-rejea 4: Kuandaa msomo ya hadithi za maisha.

Waambie wanafunzi wasome kwa pamoja hadithi uliyoinakili ubaoni au kwenye karatasi. Au wasomee hadithi hiyo na eleza inahusu nini.

Jadilini sifa za hadithi za maisha (wasifu). Waulize wanafunzi wakuambie ni kategoria gani za watu (m.f. wachezaji wa taifa wa mpira wa miguu, wanamuziki wa jadi) ambao wanawapenda, na kwa nini.

Kipatie kila kikundi chenye mwelekeo wa aina moja magazeti mbalimbali ambayo yana makala kuhusu kategoria ambayo wanakikundi wanaipenda/wanaifurahia.

Waambie watafute makala kuhusu mtu kutoka katika kwenye kategoria waliyoichagua na watumie taarifa ili kuandika mambo mawili yanayomhusu mtu huyu (angalia Nyenzo-rejea 4 kwa mwongozo katika kuwasaidia wanafunzi wako kuweza kufanya kazi hii).

Kusanya rasimu hizi ili kuzitumia katika Shughuli Muhimu.

Kama darasa lako ni kubwa sana, ungeweza kufanya shughuli hii kwa kuhusisha nusu ya darasa au vikundi vidogo kwa zamu. Ungeweza pia kuwaweka wanafunzi katika vikundi kulingana na uwezo wao –ukichanganya wenye uwezo zaidi na wale wenye uwezo mdogo ili wasaidiane. Ukiwa na wanafunzi wadogo, unaweza kufanya kazi hii kama zoezi la darasa zima ambapo unawasaidia kunukuu mawazo yao na kushirikishana maneno yao.