Somo la 1
Kuwatia hamasa wanafunzi ili wawasiliane miongoni mwao kunahusu uandaaji wa shughuli wanazoweza kuzifanya pamoja, na ambazo ni ‘halisi’. Makundi yanasaidia kutiana moyo na yanawawezesha wanafunzi kujaribu lugha mpya.
Mawasiliano ‘halisi’ huhusisha ‘tofauti za taarifa’; kwa maneno mengine, wanafunzi hugundua kitu ambacho hawakukifahamu awali kutoka kwa wenzao. Zamani, wanafunzi wangeweza kuagizwa kumwuliza mwanadarasa mwenzao, ambaye jina lake wanalifahamu vizuri, ‘Jina lako nani?’ Hapa hakuna tofauti ya taarifa, kwa hiyo mawasiliano haya si ‘halisi’.
Uchunguzi-kifani 1 na Shughuli 1 zinaonesha jinsi utafutaji wa taarifa zinazokosekana unavyoweza kutumika kwa lengo la kuunda makundi au kazi za watu wawili wawili. Vile vile, angalia Nyenzo-rejea 1: Mifano zaidi kuhusu Shughuli za tofauti za taarifa .
Uchunguzi kifani ya 1: Shughuli za tofauti za taarifa katika kuunda makundi
Liz Botha wa East London, Afrika ya Kusini, alitaka kugawanya kundi la walimu 40 katika makundi manne, kwa namna ambayo ingewasaidia kuwasiliana miongoni mwao.
Alitafuta jumla ya picha 16 zote katika ukurasa mmoja wa kitabu (angalia Nyenzo-rejea 2: Mawazo katika picha ). Alitengeneza nakala nne za ukurasa huo na kukata picha kumi kutoka katika kila ukurasa ili apate makundi kumi yenye picha nne nne: viatu; bendera, nk. Kisha alizichanganya picha.
Walimu walipofika, alimpatia kila mmoja picha moja, na kuwaambia wasiioneshe kwa mtu yeyote. Kisha akawaagiza watembee kuzunguka darasa, wakiuliza maswali ya aina hii:
Swali: Una picha ya (n) …. ?
Jibu: Hapana, sina./Ndiyo, ninacho.
Waliendelea namna hii mpaka wakaunda kundi la watu wanne wenye picha zinazofanana.
Baada ya makundi kuundwa, wanavikundi wakaanza kusemezana, na wakagundua, kwa njia ya majadiliano, kwamba wana kitu kimoja kilicho sawa kwa wote: labda wote wanne wana dada wadogo, au wanapenda au hawapendi aina fulani ya chakula au muziki, nk.
Walifurahia mno shughuli hii, na waliikamilisha kwa kufahamiana zaidi miongoni mwao.
Ni kwa jinsi gani unaweza kufanya shughuli kama hii katika darasa lako?
Shughuli ya 1: Tafuta mwenzi wako
Andika orodha ya maneno yanayohusiana na somo la hivi karibuni (angalia Nyenzo-rejea 3: Maneno na maana ili kuona baadhi ya maneno).
Wape kila wanafunzi wawili wawili neno moja kutoka kwenye orodha na vipande vidogo viwili vya karatasi. Waambie waligawe neno lao katika sehemu mbili/nusu, na waandike nusu moja katika kila kipande miongoni mwa vipande hivyo vidogo vya karatasi.
Kusanya na changanya vipande vyote vya karatasi. Sasa mpe kila mwanafunzi nusu-neno.
Waambie wanafunzi wamtafute mwanafunzi ambaye ana nusu nyingine ya neno lao, na kisha wasimame naye.
Kundi la wanafunzi wawili wawili lisome maneno yao mbele ya darasa.
Kisha, kila kundi la wanafunzi wawili wawili liandike maana ya neno lao katika kipande kingine cha karatasi. Kusanya maana hizo na maneno yaliyo nusu.
Wape tena maneno yaliyo nusu na rudia mchakato wa kuoanisha.
Baadaye, taja kila maana kwa zamu na liambie kundi la wanafunzi wawili wawili likae chini litakaposikia maana ya neno lao. Mtu yeyote asiseme kama wamekaa chini kwa kukosea au kwa usahihi. Mwishoni maana zitafafanuliwa.
Jaribu mchezo huu tena na angalia kama wanaweza kuucheza kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
Je, shughuli hii iliwasaidia wanafunzi wako kuelewa maana za maneno? Unajuaje?
Sehemu ya 3: Kuunda Fursa za Mawasiliano