Somo la 1
Kwa watu ambao hujifunza lugha katika mfumo wa kawaida wa darasani, misemo ambayo watu hutumia kila siku katika maingiliano yao mara nyingi huwa ni kitu cha mwisho kujifunza.
Zipo njia ambazo zinaweza zikatumika kuwasaidia wanafunzi wako kupata ustadi katika misemo na sentensi ambazo wanaweza kuzitumia pindi wanapokutana na watumiaji stadi wa lugha ya ziada. Kila seti ya misemo au sentensi zinatakiwa:
ziwe fupi na rahisi kujifunza;
ziseme kitu ambacho wanafunzi wanataka;
ziwe zinatumiwa na watu wengi;
ziwaruhusu wanafunzi kuanza majibizano na kujenga mahusiano;
ziwaruhusu wanafunzi kujifunza zaidi kuhusu lugha kutoka kwa watu wanaozungumza nao;
zisichochee majibu marefu toka kwa watu wengine.
Uchunguzi kifani ya 1: Kujifunza kiZulu kupitia katika mahusiano
Liz Botha aliyepo Mashariki mwa London, Afrika Kusini, alijifunza kiZulu kama lugha ya ziada kupitia mradi wa lugha za ndani uitwao TALK. Kauli-mbiu ya mradi wa TALK ilikuwa, ‘Jifunze kidogo, na utumie SANA!’
Alianza kwa kujifunza namna ya kusalimia kwa kiZulu, na kuwaeleza watu kuwa alikuwa anajifunza kiZulu. Alijifunza pia kuwataka wao wamsemeshe kwa kiZulu na kumsaidia katika zoezi lake la kujifunza lugha hiyo.
Aliwatafuta watu ambao anaweza kuzungumza nao kiZulu, na kubaini kuwa kuna idadi kubwa ya wazungumzaji wa kiZulu wanaofanya biashara ya kutembeza matunda na mbogamboga katika mtaa wa karibu na nyumbani kwake. Alifanya mazoezi ya sentensi zake kwao na kuanza kuwaelewa.
Alikuwa na rafiki aliyekuwa anamfundisha misemo mipya, na kujifunza kutoka kwake namna ya kuuliza bei ya kitu fulani na kukinunua. Hizi ndizo sentensi alizozitumia wakati uliofuata alipowaona rafiki zake wanaotembeza biashara.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda, alijifunza kujieleza kwao kuhusu yeye mwenyewe na familia yake. Baadaye aliwasimulia hadithi fupi kuhusu nini kilichotokea kwake siku moja kabla, au mwisho wa wiki. Mmoja wa watembeza biashara aliyeitwa Jabu, akawa rafiki yake wa karibu sana na kumfundisha maneno na sentensi nyingi. Mwishowe akawa anawasaidia watu wengine kujifunza kiZulu katika mradi wa TALK.
Shughuli ya 1: Kujenga mahusiano ya kujifunza lugha
Waulize wanafunzi wako ni wapi wamesikia lugha ya ziada ikizungumzwa. Ni watu gani pia wanaowafahamu kuwa wanaitumia vizuri? Ni nani wanaweza kuzungumza naye lugha ya ziada? Zingatia watu waliopo nje na ndani ya shule na pia watu ambao unaweza ukawaalika katika darasa lako. Fikiria ushirikiano na shule ya karibu kama unaweza kukuza mtagusano katika lugha ya ziada.
Sasa wanafunzi wako wanafahamu ni akina nani wanataka kuzungumza nao, pangilia mambo wanayotaka kusema nao.
Kwa utaratibu maalum, wasaidie kujifunza msamiati kama mradi wa muda mrefu. Weka uzito katika sauti na matamshi bayana.
Waache wafanye mazoezi wawiliwawili.
Mawazo juu ya vitu vya msingi vya kujifunza yanajumuisha:
salamu na kuagana;
kutaja na kuuliza majina na taarifa binafsi na za familia;
kueleza kuwa wao ni watu wanaojifunza lugha na kuwa wanahitaji msaada wa kujifunza;
kununua vitu;
kuzungumzia kuhusu hali ya hewa;
kuelezea mambo yalitokea jana;
kuomba radhi, kuomba kitu au jambo, kusifu, n.k
Wahimize wafanye mazoezi na watu waliowapendekeza (hapo juu).
Tenga muda fulani kila wiki ili kufuatilia maendeleo yao.
Je kuna mafanikio na matatizo gani wamekumbana nayo? Ni lugha ipi mpya wamejifunza?
Nini kingine walichojifunza?
Sehemu ya 5: Kusaidia ujifunzaji wa lugha ya ziada