Nyenzo-rejea 4: Nyimbo na hadithi kuhusu michakato
Nyenzo-rejea za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi
Hapa kuna wimbo wa kijadi wa Kiswahili unaofafanua michakato mbalimbali ambamo nafaka hupitia kabla ya kuliwa. Uliambatishwa katika kijitabu cha ‘Michakato na Uchakataji’. Wimbo huo unaweza kuingizwa kwenye kitabu cha mapishi. Hadithi zinafuatia, ambazo nazo zinatoka kwenye chanzo hicho hicho, zinaweza pia kujumuishwa kwenye kitabu hicho cha mapishi au cha mchakato.
Ninakipenda chakula
Chakula cha asubuhi,
Makande, uji na viazi
Ugunduzi wa mtama
Hapo zamani za kale palikuwa na mwanaume aliyekuwa na wake wawili. (Katika baadhi ya sehemu za Afrika, wanasema, ‘Mke mmoja – tatizo moja. Wake kumi na mbili – matatizo kumi na mbili!’) Mke mkubwa hakuweza kuwa na watoto, kwa hiyo alipogundua kuwa mke mdogo alikuwa mjamzito, aliona wivu sana. Lakini hakuwa na la kufanya.
Mume na mke mdogo wakapendana sana. Na hili likamfanya mke mkubwa aone wivu zaidi. Kwa hiyo mke mkubwa aliamua kusubiri mpaka baada ya mke mdogo kujifungua.
Lakini mtoto alipozaliwa, alikuwa ni mtoto wa kiume. Kwa mujibu wa mila, mke mkubwa alitakiwa kuwatunza mtoto mchanga na amariya (mke mdogo) kwa miezi michache. Mke mkubwa aliamua kwenda msituni kutafuta kitu cha kumpikia mke mdogo ambacho kingemdhuru. Alitarajia kwamba mke mdogo angekufa, na hapo angeweza kumlea mtoto mchanga kama mtoto wake mwenyewe.
Kule msituni, mke mkubwa aliona mmea ambao ulikuwa na vichwa vyenye punje zikuazo juu yake. Hajawahi kuona kitu kama hiki hapo awali. ‘Hii itamfanya alale, usingizi mzito hasa, kiasi kwamba hataweza kuamka siku itakayofuata. Kisha nitaandaa mazishi mazuri sana.’
Alipika mtama na kumlisha amariya. Alipata mshangao, amariya hakulala usingizi mzito wala kufa. Badala yake, alinenepa na kuonekana mwenye afya na kupendeza kila uchao. Vilevile, mtoto mchanga alinawiri.
Mke mkubwa alipoona matokeo ya kitu alichokuwa anakipika na kumlisha mke mdogo, aliamua kukionja yeye mwenyewe. Aliipenda ladha yake, na aliendelea kukipika na kukila kitu hicho kipya. Yeye pia, alianza kunenepa na kuwa na afya zaidi.
Sawa, mume alishindwa kujizuia kuona kuwa wake zake wawili walipendeza sana, na mtoto alikuwa na afya. Alitaka kukionja, kwa vyovyote kilivyo kitu hicho, ambacho wakeze walikuwa wanakula. Kwa hiyo, wote wakawa wanene na wenye afya.
Na, kwa hakika, katika kijiji, neno husambaa kwa haraka sana, Kabla muda haujapita, wanakijiji wote waliobaki walitaka kujua kitu ambacho familia hii ilikuwa inakula. Na ndivyo ikawa kwamba mtama ukagunduliwa.
Ugunduzi wa jibini
Hapo kale palikuwa na wanandoa vijana waliokuwa na kundi kubwa la ng’ombe na kundi kubwa la kondoo. Mume aliilisha familia yake kwa kukamua ng’ombe. Nyakati hizo, walihifadhi maziwa kwenye vibuyu.
Wanandoa hao wakati mwingine waligombana; na mke alionekana akikimbilia kwa mama yake, huku mumewe akikimbia kumfuata, kwa kufoka na kupiga ngumi hewani.
Siku moja wakati walipokuwa wakigombana, mume alikuwa ameshika kimojawapo kati ya vibuyu vyenye maziwa mazito yenye malai. Wakati mke wake alipokimbia, mume alimkimbiza, kama kawaida. Lakini safari hii alisahau kuweka chini kibuyu cha maziwa mazito yenye malai. Kadri alivyokuwa akikimbia na kumfokea mkewe, alikunja ngumi yake huku akiwa amekishika kibuyu hewani. Kwa hakika, mume alikimbia upesi sana kiasi kwamba kibuyu cha maziwa kilitikisika kwa nguvu hasa.
Aliposhindwa kumkamata mkewe, hali ya kuwa ameishiwa na pumzi, mwanaume alikaa chini. Alikuwa anasikia joto na kiu baada ya kumkimbiza mke wake na kumfokea. Kwa hiyo aliweka kibuyu mdomoni ili anywe kinywaji cha maziwa mazito yenye malai. Lakini hayakuwa maziwa yaliyomwagika toka kwenye kibuyu. Yalikuwa vitu kama maji! Haya yote yalikuwa ni makosa ya mke wake!
Mume alipigwa na butwaa. Alikaa chini na kuangalia ndani ya kibuyu. Kitu gani kimetokea kwenye maziwa mazito yenye malai? Kwa nini yamegeuka kuwa kitu cha majimaji? Akajaribu kuweka funda lingine mdomoni. Ikawa hivyo hivyo. Akaweka mkono wake ndani ya kibuyu na kugundua kwamba kulikuwa na bonge fulani. Nina hakika unaweza kukisia kitu alichokiona. Ndiyo, ni sawa, ilikuwa ni bonge la jibini laini yenye mafuta. Wakati mume aliporamba vidole vyake, aliona kwamba bonge la kitu hicho lilikuwa na ladha nzuri. Ilikuwa kama mafuta.
Alirudi nyumbani kwake haraka, akatafuta mkate wa mahindi, na kuupaka kiasi cha mafuta toka kwenye kibuyu kwenda kwenye kibonge cha mkate. Mkate ulikuwa na ladha nzuri zaidi kuliko kawaida. Hasira yake ikayeyuka. Wakati mkewe aliporudi baada ya kitambo kidogo, alimwonesha kilichotokea, na alimpa kiasi cha mafuta ili ajaribu kukionja kwenye mkate.
Kwa muda mrefu baada ya hapo, kila jibini inapokuwa imemalizika, mume alianzisha ugomvi na mkewe ili aweze kuchukua kibuyu cha maziwa mazito yenye malai anapomkimbiza. Alielewa kwamba kwa namna hiyo, maziwa mazito yenye malai yatatengeneza jibini.
Siku moja wakati jibini kidogo sana ilikuwa imebakia, mke alichukua kibuyu cha maziwa mazito yenye malai na kukitikisa kwa nguvu kadri alivyoweza. Alikitikisa, na kukitikisa. Alipoacha kukitikisa zaidi, alikiweka chini. Unaweza kukisia alichokiona ndani ya kibuyu, huwezi? Aliona jibini, na kiasi cha majimaji ya maziwa.
Jioni hiyo mume aliporudi nyumbani, mkewe alimgeukia na kusema, ‘Labda kama tutatingisha kibuyu kilichojaa maziwa mazito yenye malai kwa nguvu, tutatengeneza jibini nyingi zaidi. Hivyo hatutalazimika kugombana tena.’
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwamba waliishi kwa raha mustarehe, na kuwa familia yenye afya kwa kupiga maziwa mazito yenye malai kutoka kwenye mifugo yao, na jibini, ambayo wamejifunza kuitengeneza.
Imetoholewa kutoka: Ngtetu, C. & Lehlakane, N., Inqolowa, The Discovery of Amazimba and The Discovery of Butter, Umthamo 3, University of Fort Hare
Nyenzo-rejea 3: Kutathmini barua za urafiki wa kalamu