Namba ya moduli 1: Maendeleo ya Mtu Binafsi –Jinsi Kujiheshimu Kunavyoathiri Kujifunza

Sehemu ya 1: Njia za kuchunguza jinsi wanafunzi walivyo

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuwasaidia wanafunzi wajichunguze wao ni nani kwa njia makini na changamfu?

Maneno muhimu: usimamizi wa darasa; uulizaji maswali; kazi za vikundi; kufikiri; kukusanya data; heshima; umakinifu.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kukuza stadi zako katika kupanga darasa katika njia zitakazowasaidia wanafunzi kuheshimiana;;
  • kukuza stadi zako katika kuuliza maswali yanayofikirisha;;
  • kutumia njia mbalimbali za kukusanya data za kuwasaidia wanafunzi kujadili wao ni nani..

Utangulizi

Sote hujifunza kwa ufanisi zaidi tunapokuwa na utulivu na amani. Ukiwa mwalimu, mojawapo ya majukumu yako muhimu ni kukuza mazingira ya darasa yanayomwezesha kila mwanafunzi ashiriki kikamilifu na ajihisi kwamba anaheshimiwa na mawazo yake yanasikilizwa.

Sehemu hii inachunguza jinsi ya kufanikisha jambo hili kwa kuangalia njia mbalimbali za kupanga darasa. Utawasaidia wanafunzi kujifunza jinsi ya kuheshimiana kwa:

  • kuwasaidia waelewe wanavyofanana na wanavyotofautiana;

  • kuwaelekeza wabadilishane mawazo na hisia;

  • kuwapa kazi zitakazowawezesha kuulizana maswali na kusikiliza majibu.