Namba ya moduli 1: Kujenga Welewa wa Mahali

Sehemu ya 1: Uchoraji wa ramani kwa mazingira ya mahali hapo

Swali Lengwa muhimu: Kwa jinsi gani unaweza kutumia mazingira ya mahali hapo ili kujenga welewa wa wanafunzi kuhusu ramani na mahali?

Maneno muhimu: mazingira ya mahali hapo; ramani; kazi ya vikundi; alama;

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • umetumia nyenzo rejea za mahali hapo katika kukuza ujuzi wako kwenye ufundishaji kuhusu sura za mandhari zilizoko katika mazingira ya nyumbani na ya shuleni;
  • umetumia michezo ili kupanua welewa wa wanafunzi wako kuhusu ramani;
  • umetumia kazi ya kikundi kama mkakati wa kufundishia na kujifunzia katika kuyamudu madarasa makubwa na madogo.

Utangulizi

Wanafunzi wengi wana kiasi cha welewa wa eneo wanakoishi. Wanafahamu njia za kufika kwa haraka zaidi majumbani kwa marafiki zao au kwenye soko la mahali hapo. Unapojenga welewa wao wa mahali na, hususan, ujuzi wao wa kuchora ramani, kwa kawaida ni muhimu kuanza na kitu wanafunzi wanachokifahamu kabla ya kwenda kwenye kitu wasichokifahamu. Hii itawapa wanafunzi hali ya kujiamini, kwa sababu unatumia kitu ambacho tayari wanakifahamu.

Kutumia msingi wa kitu wanachokifahamu wanafunzi kuhusiana na sura za mandhari ya mazingira ya nyumbani na shuleni kwao, kutakurahisishia kuendelea na uchoraji wa ramani za mazingira ya mahali hapo ulio rasmi zaidi. Kufanya hivi kutakupatia mfululizo unaoeleweka wa kutalii alama zitumikazo katika uchoraji wa ramani. Shughuli zilizopo katika sehemu hii zitakusaidia kutia msukumo katika ujuzi wa wanafunzi wako kwenye uchunguzi na itawasaidia kuhawilisha maarifa kwenda kwenye alama rasmi za vielelezo. Vilevile, utajenga ujuzi wako katika kutumia kazi za vikundi kwenye darasa lako.