Nyenzo-rejea ya 1: Mazoea ya Kuishi Kiafya

Taarifa ya msingi/Maarifa ya somo kwa mwalimu

Aina za vyakula

Ni muhimu kula na, kama ikiwezekana, kula mlo kamili.

Vyakula vinaweza kupangwa katika makundi ya namna nyingi mbalimbali; na hapa ipo mojawapo ambayo hutumiwa zaidi Afrika. Inaorodhesha makundi muhimu manne ya vyakula, na kila moja hutusaidia kwa namna tofauti:

  1. Nafaka – kundi hili huhusu vyakula kama mkate, mchele, mahindi na mtama. Ulaji wa vyakula hivi hutupa nguvu za kufanya kazi. Nafaka, ambayo ni wanga, hutupa nguvu.
  2. Matunda na mboga – kundi hili ni muhimu kwa sababu hutupatia vitamini na madini tunayohitaji ili tuwe na afya. Kula vyakula hivi hutusaidia tusipate magonjwa.
  3. Nyama, kuku, samaki, mayai, maharage na karanga – vyakula vyote hivi vina protini ndani yake. Protini husaidia kujenga misuli. Unahitaji protini ili ukue vizuri na uwe imara.
  4. Vyakula vitokanavyo na maziwa – hivi hujumuisha maziwa, jibini, na mtindi. Vyakula vya aina hizi vina madini mengi ya kalsiamu. Madini ya kalsiamu ni muhimu kwa sababu husaidia kujenga mifupa na meno imara.

Ulaji wa mchanganyiko wa vyakula hivi hutupa lishe nzuri. Ulaji wa aina moja tu ya vyakula kati ya hizi kila siku unaweza kusababisha matatizo ya kiafya. Hata hivyo, kupata walau chakula ni bora kuliko kukosa kabisa.

Watoto wengi hupenda kula peremende na sukari. Hii ni sawa kama watakula kwa kiwango kidogo, kwa vile sukari inawapatia nguvu. Lakini sukari nyingi ni mbaya kwa meno kwa sababu inaweza kusababisha meno kuoza. Vilevile, sukari nyingi inaweza kutufanya tuwe wanene.

Kuhifadhi chakula kwa usalama

Ili kuhifadhi chakula kwa usalama, kuna mambo mengi unayohitaji kufikiria.

Kwanza, vyakula vinaweza kuharibika au kuoza. Hivi huhusu aina nyingi za mbogamboga, samaki na nyama, lakini baadhi ya vyakula huchukua muda mrefu kuharibika kuliko vingine. Vinaoza kama vikiachwa wazi kwa muda mrefu. Vinapooza, vinaanza kunuka vibaya, na kama ukivila vinaweza kukufanya uugue.

Katika kuzuia vyakula fresh visioze, ni vema kuviweka katika sehemu ya nyumba yenye ubaridi au jikoni, mbali na joto na unyevunyevu. Njia nyingine ya kuzuia chakula fresh kisioze ni kukihifadhi. Hii huhusu ukaushaji wa nyama, samaki au mbogamboga ama kwenye jua kali au kwa moto.

Pili, baadhi ya vyakula, hususan vyakula vya kwenye makopo, vinaweza kuharibika kama vikiwekwa kwa muda mrefu na kutohifadhiwa vizuri.

Tatu, baadhi ya vyakula, hususan nyama, vinaweza kutusababishia maradhi kama vilipikwa kwa muda mrefu halafu vikapashwa moto, lakini havikupashwa moto vizuri. Ni vizuri kupika chakula ambacho utakila kwa siku moja tu. Ukikipasha moto chakula kilichokwishapikwa, hakikisha unakipasha moto vizuri.

Mwisho, wanyama, pamoja na wadudu wengi, vilevile hupenda vyakula, lakini wakigusa vyakula vyetu huacha vijidudu vya maradhi ambavyo hutusababishia magonjwa. Jaribu kuweka vyakula mbali na wanyama. Kama una boksi au kasha la kuhifadhia, hiyo ni bora zaidi.

Kwa nini tunasafisha mazingira yetu

Tunasafisha mazingira yetu ili tujilinde na uchafu na maradhi. Watu wanaweza kuugua kutokana na kushika vitu vingi mbalimbali. Vitu hivyo vinajumuisha:

  • wanyama na wadudu;

  • chakula kilichooza;

  • takataka;

  • kinyesi cha wanyama na binadamu;

  • madawa;

  • nguo chafu.

Kutokana na sababu hii, ni vema kuondoa vitu hivi kutoka katika sehemu tunazoishi, tunazokula au tunazolala. Unaweza kufanya hivi kwa urahisi kwa kusafisha mazingira yako kila siku na kukusanya takataka na uchafu katika sehemu moja mbali na unapoishi.

Mazoea mazuri ya usafi

Kuna namna nyingi za mazoea mazuri ya usafi unazoweza kuzifanya kila siku. Sababu za kufanya haya ni kutuweka katika usafi na kutulinda tusibebe maradhi.

Baadhi ya mazoea mazuri ni kama haya:

  • tuoge kila siku kama ikiwezekana;

  • tusafishe meno yetu kila siku kama ikiwezekana ;

  • tunawe mikono yetu kabla ya kula au kupika;

  • tunawe mikono yetu baada ya kutoka chooni;

  • tuweke nyumba zetu, nguo zetu na mazingira yetu katika hali ya usafi kadri iwezekanavyo;

  • kutojisaidia karibu na nyumba au jiko;

  • kutoacha vyakula wazi.

Namna bora za mazoezi

Zoezi la kawaida la aina yoyote ni kitu kizuri, lakini mara zote ni muhimu kujaribu kujenga tabia ya kufanya hivyo.

Aina ya mazoezi ambayo unaweza kuyafanya mara kwa mara hujumuisha:

  • kutembea au kukimbia shuleni;

  • kucheza michezo, k.v. kandanda;

  • kuogelea;

  • kufanya kazi shambani;

  • kazi za nyumbani.

Ni muhimu kujaribu kufanya mazoezi kila siku kwa sababu inasaidia kujenga misuli yako, moyo wako, na siha yako kwa ujumla. Kama hufanyi mazoezi mara kwa mara, utaona vigumu zaidi utakapojaribu kufanya hivyo. Utajiona dhaifu na kukosa pumzi.

Nyenzo-rejea 2: Ushauri kuhusu maonyesho ya darasani