Somo la 2

Ni muhimu kwa wanafunzi wako kuelewa kwamba, kama ilivyo kwa walimu wao, na wao pia wana majukumu katika darasa lao.

Kwanza, lazima uwe mfano mzuri wa kuigwa. Onesha heshima katika kazi zako: wahi kufika kazini; andaa na hudhuria masomo; sahihisha kazi za kufanya nyumbani (mazoezi), n.k. Usipotimiza majukumu yako, usitegemee wanafunzi wako watayatimiza yao.

Pili, washirikishe wanafunzi katika kudumisha ubora wa darasa. Hili linahusu kuwahusisha katika:

  • kusafisha ubao;

  • kuliweka darasa katika hali ya usafi na mpangilio mzuri;

  • kutunza vitabu na samani, na kadhalika.

Kama watalitunza darasa lao wao wenyewe, wataanza kulionea fahari.

Tatu, washirikishe katika kupanga mafunzo yao wenyewe kwa njia ya shughuli ambazo unawapa. Jambo hili huwajumuisha katika:

  • kudhihirisha tofauti kati ya muda wa kazi na muda wa kucheza;

  • kupanga kazi za vikundi na vipindi vya kujisomea;

  • kuangalia wengine wanavyofanya kazi, na kadhalika.

Njia ya kawaida ya kuanza kutekeleza hili ni kwa kuwateua wanafunzi kama viranja wa madarasa na viongozi wa makundi, wenye wajibu wa kusimamia majukumu mbalimbali. Lakini wanatakiwa kufahamu kinachohitajika kwa kila wajibu.

Kwa maelezo zaidi tazama Nyenzo-rejea 2: Kuwatumia viranja wa darasa .

Uchunguzi kifani ya 2: Stadi na majukumu katika darasa

Bwana Sambwa ni mwalimu mwandamizi mwenye darasa kubwa la viwango vingi tofauti. Ana kundi la viranja wa madarasa kuanzia viwango vya juu ambao wana majukumu madogo madogo darasani na pia wanawasaidia wanafunzi wadogo. Viranja hawa wanasimamia makundi yao ili yawe tayari mwanzoni mwa kila somo, wanatunza vitabu na wanasafisha ubao kila siku. Kwa kweli wanasaidia sana.

Siku ya Ijumaa, ambayo ni siku ya usafi wa darasa, Bwana Sambwa anawaambia viranja wake wa darasa kufanya kazi katika makundi yao kuanzia madarasa ya chini kuorodhesha maeneo yanayohitaji utekelezaji. Kila kundi litoe pendekezo moja, ambalo linaandikwa ubaoni.

Kila kundi linajitolea kusimamia shughuli moja, na kwa kusimamiwa na kiranja wa darasa, linafanya kazi hiyo kila Ijumaa wakati wa mapumziko mpaka mwisho wa muhula.

Mwisho wa wiki, kila kundi linaeleza mbele ya darasa, walichofanya na walipoweka vifaa. Vile vile, wanawapa wanadarasa mapendekezo kwa ajili ya wiki itakayofuata ili kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu au kusaidia kutatua matatizo.

Mwisho wa muhula, wanapitia maendeleo ya kila kundi, na darasa zima linapiga kura kuchagua kundi lililoshinda kuliko yote.

Shughuli ya 2: Kuteua viranja wa darasa

Panga jinsi utakavyotambulisha suala la viranja wa darasa ili kulisaidia darasa.

  • Tambulisha hoja ya viranja wa darasa kwa darasa zima. Fafanua jinsi mfumo wa viranja wa darasa utakavyofanya kazi, na jinsi utakavyomnufaisha kila mmoja.

  • Pamoja na darasa lako, jadili na andika orodha ya majukumu yote ya darasani ambayo yanahitaji kutekelezwa mwanzoni, katikati na mwishoni mwa kila siku.

  • Bainisha majukumu ambayo utayatekeleza wewe, nay ale yatakayofanywa na wanafunzi.

  • Kama darasa, amuaeni kuhusu idadi ya viranja wa darasa inayohitajika na fikiria namna ya kuwachagua. Unaweza kuwabadili viranja wa darasa kila wiki ili kila mmoja apate nafasi ya kuwa kiranja na kutekeleza wajibu wake kwa wengine.

  • Teua kundi la kwanza la viranja wa darasa na eleza majukumu yao. Mwisho wa wiki ya kwanza, ukiwa pamoja nao, pitia kazi zao mbele ya darasa.

  • Waambie wapendekeze majukumu mapya ambayo watayatekeleza.

Kuchagua viranja wa madarasa kuna athari gani katika mwenendo wa shughuli za darasa lako? Je, wanafunzi wanaupenda mfumo huu? Je, unahitaji kupitiwa, na labda kufanyiwa marekebisho na darasa?