Nyenzo-rejea 2: Mgogoro wa ng’ombe wasababisha mapambano makali mwaka 2001’

Zaidi ya watu 400 wameyakimbia makazi yao Mashariki mwa Tanzania, mkoa wa Morogoro kwa kuogopa kuvamiwa na wafugaji wa Kimasai, baada ya mapambano ya kumwaga damu yaliyotokea tarehe 8 Desemba kati ya wafugaji na wakulima na kuacha watu 31 wengi wakiwa ni wanawake na watoto wakiwa wamekufa.

Mapambano kati ya Wamaasai wanaohamahama na wakulima mkoani Morogoro yalikuwa yakiendelea tangu mwishoni mwa Oktoba, lakini yalikuwa mabaya zaidi wakati wa siku nne za mapigano wiki iliyopita, Associated Press (AP) iliripoti siku ya Jumanne.

Associated Press ilisema kuwa shambulio la tarehe 8 Desemba lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa watu wawili wa kabila la Kimaasai na ng’ombe 35 ambako kulifanywa na wakulima. Mchanganyiko wa kulipiza kisasi pamoja na hasira kubwa ya kuchukuliwa mifugo yao kuliibua mgogoro mkubwa dhidi ya matumizi ya ardhi ambao haukuwa na suluhisho lililo wazi.

Gazeti la Kitanzania la Guardian toleo la Jumanne liliripoti kuwa mapigano yalianza baada ya wakulima wilayani Kilosa kuchukua kwa nguvu mifugo ambao walikuwa wakitangatanga mashambani mwao; wakulima walikuwa wakisubiri kulipwa fidia. Mazoea haya si mageni katika mkoa wa Morogoro, moja ya mikoa michache katika Tanzania isiyo na ukame sana, ambapo wafugaji na wakulima wanaishi pamoja. Kivutio cha ardhi ya malisho, kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, kimepelekea kuwepo kwa makundi ya mifugo ya Kimasai 250,000 katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Dk. E de Pauw, mshauri wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kwenye suala la matumizi ya ardhi aliliambia IRIN kwamba mgogoro umekuwa ukiendelea kwa miaka kumi hadi sasa. de Pauw alisema ‘Hakuna mpaka halisi unaotenga ardhi ya kilimo na ya ufugaji’. Alisema kuwa kutokana na wafugaji kumiliki idadi ya kutisha ya makundi ya ng’ombe kwa kule kulundikana kwao sana mkoani Morogoro, wanawachunga katika ardhi za kilimo, ama kwa kujua au kwa bahati mbaya, ambako kunachochea uhasama kwa upande wa wakulima.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la Afrika (PANA), serikali ya Rais Benjamin Mkapa imeweka nguvu mpya kwenye sekta ya mifugo. de Pauw alisema kuwa serikali imeunda sera ya kutenga maeneo ya wafugaji, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.

Wamaasai hufuata mtindo wa maisha wa nusu – unomadi wa kutoka eneo moja hadi jingine ili kutafuta malisho na maji. de Pauw aliliambia IRIN kuwa ‘Daima Wamasai wangependa kusaka ardhi bora [na] na hakuna wafugaji ambao wangependa kuwahamishia wanyama wao kwenye mikoa ambayo ina ukame. Mashindano ya kupata ardhi bora ni ya kuudhi hasa kipindi cha ukame.

Vyombo vya habari vya Tanzania vimeripoti kuwa sababu za kisiasa pia zinachangia katika tatizo hili. Gazeti la Guardian, toleo la Alhamisi, liliripoti kuwa wanavijiji wanadai kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO) ilikuwa imeshajua kuhusu huu mgogoro kati ya wafugaji wa Kimaasai na wakulima tangu mwaka 1997, wakati wawakilishi wa wakulima walipopeleka rufaa yao kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. Wanakijiji baadaye waliamua kuunda vikundi vya ulinzi wa jadi vilivyoitwa ‘sungusungu’.

‘Hata hivyo, sungusungu hawakufanya vizuri kwa sababu hawakupata ushirikiano wa polisi’, mwakilishi wa wakulima aliliambia The Guardian. Mkuu wa Wilaya wa Kilosa, Edith Tumbo, alisimamishwa kazi Jumatatu na Waziri Mkuu Frederick Sumaye, kwa mujibu wa Guardian.

Chanzo cha awali: EDC News 2001.

Nyenzo-rejea 1: Mgogoro wa kifamilia