Somo la 2
Sote huishi katika makundi au familia. Familia zetu ni sehemu ya makundi, kama vile vijiji au jamii. Ndani ya jamii tuna haki na wajibu. Hii maana yake ni kuwa inabidi kufanya mambo fulani ndani ya jamii na jamii lazima zifanye au zitufanyie mambo fulani. Nyenzo-rejea 2: Haki za mtoto itakusaidia kutayarisha mada hii.
Wanafunzi wanahitaji kukutana na wataalamu ambao wako tayari kuzungumza nao kuhusu maoni yao ya mada hii. Hii itawasaidia wanafunzi kuelewa wajibu wao katika jamii na kuwahamasisha kujifunza. Kabla ya mgeni kuja darasani kwako, ungependa kufikiria kupanga upya madawati ili kuifanya hali ya darasa kuwa vutivu. Hali hii itamfanya mgeni kujisikiavizuri na kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa sababu wanaweza kuona na kusikia vizuri zaidi. Kwa taarifa zaidi tazama Nyenzo-rejea muhimu: Kuwatumia wageni kutoka kwenye jamii husika kama nyenzo.
Uchunguzi kifani ya 2: Kutayarisha darasa ili kujadili majukumu ya jamii
Mwalimu Komba alitaka wanafunzi wake 48 wa darasa la nne kujadili kuhusu majukumu ya jamii. Aliamua kuwa jinsi darasa lilivyopangwa halisaidii kazi za majadiliano kwa hivyo alifanya mpango wa kurekebisha madawati yalivyopangwa.
Alijadiliana na mwalimu wake mkuu, ambaye alikubali mabadiliko hayo. Akisaidiwa na mwalimu mwenzake, aliunda makundi manane, kila moja likiwa na madawati matatu yaliyopangwa kukaliwa na wanafunzi sita. Kesho yake, wanafunzi walifurahi sana baada ya kuona mabadiliko ya darasa lao. Mwalimu Komba alieleza kuwa mpango wa darasa utawawezesha kuwa na majadiliano mengi zaidi.
Aliwataka wanafunzi wajadiliane, katika makundi yao, jamii inawapa nini - haki za watu wanaoishi katika jamii. Lakini kwanza aliwaeleza kuhusu kupeana zamu katika kujadiliana katika makundi yao na wasikilizane kwa kuheshimiana. Kila kundi lilitakiwa kutengeneza karatasi kubwa inayoonesha mambo mbalimbali yanayotolewa na jamii kama haki yao wakiwa wanajumuiya.
Wanafunzi wake walijua kuwa nao wana wajibu pamoja na haki. Hivyo, katika makundi yao walijadili wajibu wao katika jamii ni upi na baadaye waliandika maoni yao kwenye karatasi kwa rangi tofauti na kuonesha ufunguo. Makaratasi yote yalibandikwa ukutani ili makundi yaone maoni ya kila mmoja kabla ya kuwa na mjadala wa mwisho kuhusu ni maoni yapi yalikuwa yanaeleza haki na wajibu muhimu
Shughuli ya 2: Kuwatumia wataalamu kutoka katika jumuiya kuwahamasisha wanafunzi
Jadiliana na wanafunzi wako wajibu wao katika jamii.
Waongoze katika majadiliano yao kuhusu utunzaji wa mazingira, kuwaheshimu watu na mali, kusaidiana. Waweke wanafunzi katika makundi na watake wanafunzi kutengeneza karatasi kubwa (poster), andika shairi au hadithi au chora picha kuonesha maoni yao.
Jadili haki zao katika jamii- wasaidie waelewe kuwa wana haki ya kupata elimu, kupata huduma za afya, kuwa huru mitaani na mjumbani, na kutoa maoni yao.
Zungumzia viongozi na watu muhimu katika jumuiya. Orodhesha watu wote ambao wanasaidia katika jamii.
Amua ni yupi akaribishwe shuleni kuzungumzia kazi zake katika jamii. Anaweza kuwa kiongozi wa kijiji, kiongozi wa jamii, kiongozi wa siasa, nesi, mkutubi, afisa wa polisi au kiongozi wa dini.
Kwa msaada tazama Nyenzo-rejea Muhimu: Kuwatumia wanajamii kama nyenzo.
Baada ya ugeni, jadili na wanafunzi wako wamejifunza nini kuhusu kazi za mgeni.
Somo la 1