Somo la 1
Mitazamo pogofu kuhusu jinsia, ingawa ni suala pana la kijamii, inaanzia nyumbani. Bila ya kuitambua, wazazi wengi katika familia zao huwatendea wavulana na wasichana namna tofauti –imeshakuwa kawaida kufanya namna hiyo; na wanaona hakuna sababu ya kubadili.
Matokeo yake, tabia hii yenye msimamo usiobadilika imesababisha, hususan kwa wasichana, kuamini kwamba hivi ‘ndivyo namna mambo yalivyo’ na hakuna chochote kinachoweza kufanyika hapo. Wavulana pia wanaikubali hali hii kwa sababu inaelekea kuwanufaisha.
Unaweza kuchunguza tofauti hizi pamoja na wanafunzi wako kwa kufanya kazi katika makundi ya jinsia moja ili kuwasaidia wanafunzi wako wazungumze kuhusu tabia na imani zao.
Katika Uchunguzi-kifani uliotangulia ( Moduli 2, Sehemu 2, Uchunguzi-kifani 2 ), mwalimu mmoja aliwaambia wanafunzi wake walete kanuni za familia darasani. Wakati walipoziwasilisha, darasa liliona kwamba kulikuwa na kanuni tofauti kati ya wavulana na wasichana. Mwalimu akaamua kuandaa masomo ya jinsia, baadaye katika muhula huo. Uchunguzi-kifani 1 unaonesha kilichotokea katika mojawapo kati ya masomo hayo.
Uchunguzi kifani ya 1: Kutumia mchezo wa kuigiza ili kuchunguza masuala ya kijinsia
Mwalimu aliunda orodha ya kanuni za kifamilia toka katika somo lililopita. Alifikiria kuhusu namna ya kuchunguza masuala yanayojumuisha utendewaji tofauti kwa wavulana na wasichana katika familia, na aliamua kwamba mchezo wa kuigiza ungekuwa ni mbinu nzuri ya kufundishia. Angalia Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumiaigizo-kifani/majibizano/mchezo wa kuigiza darasani kwa kupata mawazo.
Alilipanga darasa katika makundi ya ‘familia’ yenye ukubwa mbalimbali, huku wanafunzi wakiigiza nafasi mbalimbali za wanafamilia. Kundi moja lilikuwa na watu wane tu, kundi lingine lilikuwa na kumi na mmoja. Aliyaambia makundi yatunge mchezo unaohusu familia ili kuonesha jinsi wavulana na wasichana wanavyotendewa. Aliwapatia wanafunzi somo zima kuhusu mada hii na alizungukia kila kundi ili kuwasaidia na kuwapa moyo. Aliwauliza maswali kama ‘Kwa hiyo nini kitatokea baada ya hapo?’ ‘Unawezaje…?’
Aliwaagiza walete baadhi ya vitu ili kuweza kubainisha watu mbalimbali katika familia, na wafanye mazoezi ya michezo yao nyakati za mapumziko.
Katika vipindi vichache vilivyofuatia, kila kundi lilikuwa na zamu ya kufanya onesho la mchezo wao na baadaye darasa zima lilijadili wanayoyaona. Baada ya kutazama michezo yote na kuijadili, waligundua kwamba wasichana walikuwa na uhuru finyu zaidi wa kuchagua kuliko wavulana. Walipiga kura kuamua kama hali hii ni haki, na darasa lilikubali kwamba wavulana na wasichana lazima wapewe fursa sawa na wasinyimwe upataji wa shughuli na kazi kwa sababu za jinsia zao.
Shughuli ya 1: Kazi za makundi ya jinsia moja
Ili kuwasaidia wananfunzi wako kuchunguza na kufafanua hisia zao kuhusu majukumu ya kijinsia, shughuli hii inatumia makundi ya jinsia moja.
Andaa na wape hojaji katika Nyenzo-rejea 2: Jinsia –unafikiri nini? Kwa kila mwanafunzi na eleza kanuni kwa darasa zima.
Wape dakika kumi ili wakamilishe hojaji.
Kila mwanafunzi aoneshe majibu yake kwa jirani yake na wayajadili.
Panga darasa katika makundi ya jinsia moja ya kati ya wanafunzi watano na wanafunzi saba.
Kila kundi liandae orodha ya shughuli mbalimbali wanazozifanya:
katika siku za shule;
katika siku za wikiendi;
wakati wa likizo.
Makundi yawasilishe orodha ya shughuli zao –ambazo unaziandika ubaoni –kuunda orodha ya wasichana na nyingine ya wavulana.
Jadili orodha hizo pamoja na darasa. Uliza kuhusu usawa. Waulize kwa nini wanafikiri shughuli ziko tofauti.
Waambie wanafunzi waandike insha yenye kichwa ‘Ni kwa namna gani na kwa nini wasichana wanatofautiana na wavulana?’ Waambie watoe maoni yao wenyewe. Watoto wadogo wanaweza kuchora picha za shughuli wanazozifanya na kufanya ulinganifu miongoni mwao.
Sehemu ya 2: Njia za kuchunguza masuala ya kijinsia